T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 05:55:34

Mwanachuo ashtaki Gavana Mutai akitaka Sh200,000 za malezi

GAVANA wa Kericho Dkt Eric Mutai ameshtakiwa mahakamani na mwanafunzi wa chuo kikuu akitaka aagize kumlipa Sh200,000 kila mwezi kwa matunzo ya mtoto wa mwaka mmoja anayesema alizaa naye. M.C, mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Kabianga, amemshutumu gavana huyo kwa kukwepa jukumu lake la mzazi kwa kukataa kutoa mahitaji ya mtoto huyo, ambaye anadai alizaliwa kutokana na uhusiano wao wa kimapenzi mwaka 2024. Bi M.C pia anataka Dkt Mutai ampe nakala ya kitambulisho chake cha kitaifa ili aweze kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo. Katika stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, mwanafunzi huyo anasema yeye na Dkt Mutai walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi mwaka 2024, ambao ulisababisha kuzaliwa kwa mtoto huyo Julai mwaka huo huko Kericho. Anadai amekuwa akilea na kutunza mtoto tangu kuzaliwa kwake na ndiye amekuwa akigharamia mahitaji yake bila msaada wa maana kutoka kwa gavana. Bi M.C anasema hana ajira wala chanzo cha mapato kwa sababu bado ni mwanafunzi na kwa sasa anategemea ndugu zake kumsaidia yeye na mtoto. Anadai kwamba juhudi zake za mara kwa mara za kumshawishi Dkt Mutai achangie mahitaji ya mtoto hazijafua dafu. "Katika matukio kadhaa tangu mtoto azaliwe, mlalamishi amelazimika kuwasiliana na kumsihi mshtakiwa achangie mahitaji ya mtoto, lakini mara kadhaa simu na jumbe zake hupuuzwa," inasema sehemu ya stakabadhi hizo. Kwa mujibu wa kesi hiyo, hali ilikuwa ngumu hadi Bi M.C akaondoka Kericho, ambako anaishi kwa kawaida, na kwenda kujisitiri nyumbani kwa dada yake huko Nakuru. Anasema dada yake amekuwa akimsaidia kupata mahali pa kuishi, chakula, matibabu na mahitaji mengine ya msingi akiwa na mtoto wake. Mwanafunzi huyo anadai pia kwamba kutokuwa na kitambulisho cha Dkt Mutai kumezuia mtoto kupata cheti cha kuzaliwa. Anasema hali hiyo imeathiri haki ya mtoto kupata uraia wa kutambuliwa nao. Kesi hiyo iliwasilishwa baada ya juhudi za wawili hao kufikia makubaliano kuhusu matunzo ya mtoto kushindikana. Bi M.C anasema baada ya kumtumia gavana barua ya kumtaka awajibike na kumjulisha kuhusu hatua za kisheria alizokuwa akizingatiwa, Dkt Mutai aliwasiliana naye akitaka suala hilo litatuliwe nje ya mahakama. Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, gavana alipendekeza kutoa Sh25,000 kila mwezi kwa matunzo ya mtoto. Hata hivyo, alikataa kiasi hicho akise ma hakitoshelezi mahitaji halisi ya mtoto. Kupitia mawakili wake, Bi M.C baadaye aliandaa makubaliano ya kugawana majukumu ya malezi na kuyawasilisha kwa mawakili wa gavana. Anasema Dkt Mutai aliwasilisha kesi katika mahakama ya hakimu Nakuru akimshutumu kwa kumzuia kumwona mtoto na kutofichua alikokuwa. Bi M.C amekanusha madai hayo. Anasema Dkt Mutai hajawahi kuonyesha nia ya kumwona mtoto tangu azaliwe wala kufanya juhudi za kupata taarifa kuhusu afya yake, alipo au hali yake kwa jumla. Anadai pia kuwa wakati mmoja alimpeleka mtoto katika makazi ya gavana akitarajia kupata msaada wa matunzo, lakini Dkt Mutai alikataa kumwona au kumshika mtoto huyo. Kulingana na madai yake, baadaye alikatazwa kurejea katika makazi hayo. Mwanafunzi huyo sasa anataka mahakama iamue kwamba haki za mtoto zimekiukwa na iamuru Dkt Mutai kulipa Sh200,000 kila mwezi kwa matunzo yake. Pia anataka gavana huyo awajibikie bima kamili ya matibabu ya mtoto. Katika uamuzi wa Septemba 14, mahakama iliagiza Dkt Mutai akabidhiwe karatasi za kesi ili ajibu madai yaliyowasilishwa dhidi yake. Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 28.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 04:55:40

Ruto atumia miradi ya maendeleo kujipigia debe kuelekea 2027

RAIS William Ruto anazidi kugeuza maeneo ya ujenzi kuwa majukwaa ya kisiasa, akizunguka nchini kuzindua, kukagua na kukamilisha miradi ambayo imekuwa msingi wa ajenda yake ya maendeleo. Rais ameweka mabilioni ya fedha katika miradi ya maendeleo akielekea uchaguzi wa 2027, akitegemea barabara, reli, nyumba, masoko, miradi ya maji na huduma za umma kuonyesha rekodi ya serikali yake. Mkakati huo ulidhihirika wakati wa ziara yake ya siku tano Nyanza iliyokamilika Alhamisi, ambapo alitembelea Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay, akikagua barabara na kuzindua miradi ya maji, afya, elimu na miundombinu. Ziara hiyo ilijumuisha barabara ya Mamboleo-Miwani-Chemelil-Muhoroni-Kipsitet na miradi ya maji ya Ziwa Victoria huko Kisumu, pamoja na barabara, madaraja, masoko na miradi ya maji Siaya, Migori na Homa Bay. Badala ya kutegemea miradi mikubwa pekee, Dkt Ruto anawasilisha mtandao wa uwekezaji unaolenga shughuli za kila siku za kiuchumi, zikiwemo barabara bora kwa wakulima na wafanyabiashara, masoko ya biashara ndogo, maji, nyumba za bei nafuu, umeme, hospitali na vyuo vya kiufundi. Kote nchini, serikali pia inaangazia barabara ya Rironi-Mau Summit, upanuzi wa reli ya SGR hadi Magharibi, nyumba za bei nafuu na mamia ya masoko ya kisasa. Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wanasema swali kuu ni iwapo miradi hiyo itasaidia kuongeza mapato ya familia kabla ya Wakenya kupiga kura mwaka 2027. Dkt Ruto mwenyewe anakiri kuwa gharama ya maisha bado ni changamoto kubwa nchini. Anasema miundombinu inapaswa kuunda ajira, kupunguza gharama ya kufanya biashara na kufungua masoko. Nyanza kwa mfano, miradi iliyokaguliwa na kuzinduliwa ni pamoja na, Daraja la Dhogoye, Hospitali ya Siaya, uwanja wa michezo na miradi ya maji. Homa Bay ina miradi ya barabara, masoko, maji, nyumba na miundombinu ya baharini, huku Migori ikiwa na miradi kadhaa ya barabara, umeme na masoko. Miradi mingine mikubwa ni barabara ya Rironi-Mau Summit na upanuzi wa SGR kutoka Naivasha kupitia Narok, Bomet, Kericho na Kisumu hadi Siaya, Kakamega, Busia na Malaba. Serikali pia inasukuma mpango wa nyumba za bei nafuu, huku Rais akisema inajenga nyumba 300,000, mabweni 180,000 ya wanafunzi na masoko 500 ya kisasa kwa gharama ya Sh93 bilioni. Kwa mujibu wa Rais, miradi hiyo pia inalenga kuunda ajira na kuweka fedha mifukoni mwa wananchi. Hata hivyo, wakosoaji wanasema takwimu za ujenzi pekee hazimaanishi moja kwa moja kuwa maisha ya familia yameimarika. Changamoto nyingine ni muda, kwani baadhi ya miradi mikubwa huenda isikamilike au kutoa manufaa yake yote kabla ya uchaguzi wa 2027. Kwa hivyo, mtihani wa miradi hiyo hautakuwa idadi ya miradi iliyozinduliwa pekee, bali pia iwapo itakamilika, itafanya kazi na kuleta manufaa yanayoonekana katika maisha ya kila siku ya Wakenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 02:55:24

Uhuru akejeli Ruto kuhusu dai kuwa yeye ni 'sponyo' wa Upinzani

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta jana alimkejeli Rais William Ruto kuhusu madai yake ya mara kwa mara kwamba anafadhili upinzani, kwa kujitaja mwenyewe kama "Sponyo". Bw Kenyatta alikuwa akizungumza katika mazishi ya Christine Waruguru, mama wa aliyekuwa Naibu Mdhibiti wa Ikulu George Kariuki, katika Kaunti ya Murang'a. Aliandamana na Naibu Kiongozi wa Jubilee Party na mgombea urais, Dkt Fred Matiang'i, pamoja na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro. Katika siku za hivi majuzi, Rais Ruto amekuwa akimtaja Bw Kenyatta kama mfadhili mkuu wa upinzani, wakati mwingine akimwita kiongozi wa waasi. Pia amekuwa akiita kundi la upinzani la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa "Linda Uhuru Kenyatta". Katika hafla hiyo ya mazishi, Bw Kenyatta alianza kutoa hotuba bila maandishi kabla ya kujizuia na kusema imekuwa hatari kwake kutoa mawazo yake hadharani bila maandalizi. "Imekuwa hatari kwangu kuzungumza,nisije nikatafsiriwa vibaya na vyombo vya habari, acha nifuate rambi rambi zangu nilizoandika," alisema. Baada ya kumaliza kusoma ujumbe wake wa rambirambi, alimalizia kwa kauli ya mzaha iliyowafanya waliohudhuria kuangua kicheko. "Hayo ndiyo machache kutoka kwa Sponyo," alisema. Hafla hiyo pia ilikuwa muhimu kisiasa kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa Bw Kenyatta kushiriki jukwaa moja na Bw Nyoro tangu uhusiano wao wa kisiasa uvurugike mnamo 2018. Wakati huo, Bw Kenyatta alikuwa akimuunga mkono Raila Odinga kumrithi katika uchaguzi mkuu wa 2022, huku Bw Nyoro akiwa miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya waliomuunga mkono Dkt Ruto, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais. Bw Nyoro alikuwa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Kiharu mnamo 2017 kwa tiketi ya Jubilee akiwa mshirika wa karibu wa Bw Kenyatta. Lakini mnamo 2018, uhusiano wao ulianza kuvurugika. Wakati wa harusi ya aliyekuwa Seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata, ambaye sasa ni gavana, Bw Kenyatta aliwashauri viongozi chipukizi, akiwemo Bw Nyoro, kutulia na kuanzisha familia. Muda mfupi baadaye, uhusiano wa kisiasa kati yao ulizidi kuwa mbaya, huku Bw Nyoro akikamatwa kwa madai ya kutofautiana kisiasa na baadaye akamjibu Bw Kenyatta vikali katika kampeni. Uwepo wa Bw Nyoro jana uliongeza hamu ya kisiasa katika hafla hiyo, hasa kutokana na ukaribu wake wa hivi majuzi na Dkt Matiang'i. Bw Kenyatta alimuidhinisha Dkt Matiang'i kuwa chaguo lake la urais kuelekea uchaguzi wa 2027 katika hafla iliyofanyika Murang'a Novemba 7, 2025. Tangu wakati huo, Bw Nyoro amekuwa akionyesha kumuunga mkono Dkt Matiang'i, hali ambayo imeibua mjadala kuhusu uwezekano wa wawili hao kushirikiana katika uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, jana watatu hao hawakutoa tangazo lolote rasmi kuhusu mpango wa kisiasa au tiketi ya pamoja. Badala yake, Bw Kenyatta alizungumzia umuhimu wa taifa kuwaheshimu mashujaa wake, akisema Kenya ina historia ya kutowatambua ipasavyo waliotumikia taifa. Alisema wanawake na vijana ni miongoni mwa mashujaa ambao wamekuwa wakipuuzwa zaidi. Dkt Matiang'i naye alikosoa baadhi ya viongozi wa kitaifa ambao alisema wamekuwa wakiwatukana wengine, kuwadanganya wananchi na kutoa kauli zisizo na maana. Kwa upande wake, Bw Nyoro alimsifu Bw Kenyatta na kuhusisha baadhi ya miradi ya maendeleo katika Kiharu na uongozi wa rais huyo wa zamani. "Baadhi ya barabara mnazoona Kiharu zilitokana na uongozi wako mzuri, mkuu wangu," alisema. Mbunge huyo pia alidokeza kuwa Bw Kenyatta bado ni mtu anayemshauri katika safari yake ya kisiasa. "Ninashukuru kwamba unatupa ushauri mzuri tunapokutafuta," alisema. Bw Nyoro aliwaomba Wakenya kuelewa msimamo wake wa sasa wa kisiasa, akisema yuko katika hatua ya kujijenga mwenyewe.

read more