T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 16 Aug 2026 08:55:16

Ruto afufua maono ya hayati Raila katika Ruwaza yake ya 2060

RAIS William Ruto alipozindua mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa Kenya baada ya Ruwaza ya 2030 wiki hii, aliutaja kama juhudi mpya za kuwapa mwongozo wa muda mrefu utakaonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Hata hivyo, nyuma ya kauli za kuunda mwongozo mpya wa maendeleo, unafanana pakubwa na pendekezo la aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuhusu Kongamano la Kitaifa la Vizazi ambalo lilizinduliwa miezi michache kabla ya kifo chake. Mipango yote miwili inaweka wananchi katikati ya maamuzi kuhusu mustakabali wa taifa. Pia inakusudia kuwahusisha vijana, wataalamu, viongozi wa kaunti, wanavyuo, sekta ya biashara, mashirika ya kiraia na viongozi wa kidini katika kujadili mwelekeo wa Kenya. Pendekezo la Raila lilijikita zaidi katika kutafuta suluhu kwa changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiutawala zinazokabili taifa. Kwa upande mwingine, mjadala wa Ruto unalenga kufafanua Kenya itakuwa taifa la aina gani baada ya kufikia mwisho wa mpango wa Ruwaza ya 2030. Licha ya tofauti hizo, misingi ya miradi hiyo inaonekana kufanana kwa kiasi kikubwa. Yote inatokana na imani kuwa mustakabali wa Kenya haupaswi kuamuliwa na wanasiasa wachache katika mikutano ya Nairobi pekee. Ruto amependekeza mchakato wa kitaifa utakaowahusisha wadau kutoka sekta mbalimbali ili kuamua dira mpya ya taifa. Kwa mujibu wa vyanzo vya Ikulu, Gavana wa Kisumu Profesa Anyang' Nyong'o amepewa jukumu la kuongoza timu itakayobuni mfumo wa majadiliano hayo. Timu hiyo itapendekeza namna mashauriano yatafanyika kutoka mashinani hadi kiwango cha kitaifa. Muundo huo unafanana pakubwa na mpango ambao Raila alikuwa amependekeza mwaka 2025. Akizungumza katika mahojiano akiwa nyumbani kwake Karen Julai 19, 2025, Raila alisema kongamano hilo lingeanzia katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuendelea hadi ngazi za wadi, maeneo bunge na kaunti. Hatimaye, wawakilishi wangekutana katika kongamano kubwa la kitaifa la takribani wajumbe 3,000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi. "Hilo lingekuwa baraza halisi la wananchi," alisema Raila wakati huo. Alisisitiza kuwa wananchi wa kawaida walipaswa kupewa nafasi ya kueleza changamoto zao na kuamua vipaumbele vya taifa kabla ya wanasiasa kuingilia mchakato huo. Kwa upande wake, Ruto alipokuwa akizindua mjadala huo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC), alisisitiza mara kadhaa kwamba si mradi wa serikali bali wa wananchi. "Huu si mradi wa serikali. Huu ni mradi wa wananchi," alisema Rais. Aliongeza kuwa serikali itatoa jukwaa na rasilimali lakini haitawalazimisha wananchi maamuzi ya kufanya. Kauli hiyo inaendana kwa kiwango kikubwa na mawazo ambayo Raila alikuwa ametetea kuhusu umuhimu wa wananchi kutumia mamlaka yao ya kikatiba kuamua hatima ya taifa. Raila alipendekeza kwamba nusu ya wajumbe katika mikutano ya mashinani wawe vijana hasa wa kizazi cha Gen Z. Naye Ruto amesema mjadala wa baada ya Ruwaza ya 2030 lazima uzingatie maslahi ya vijana ambao watarithi Kenya ya baadaye. Hata hivyo, kuna tofauti muhimu. Kongamano la Raila lilizaliwa wakati taifa lilikuwa linakabiliwa na malalamishi kuhusu utawala, ukosefu wa ajira, ufisadi na madai ya ukatili wa polisi. Hivyo lilikuwa na mwelekeo wa kisiasa na kikatiba zaidi. Kwa upande mwingine, mjadala wa Ruto umejikita katika maendeleo ya muda mrefu na namna ya kuhakikisha Kenya inabaki na mwongozo mmoja hata baada ya mabadiliko ya serikali. Naibu Rais Kithure Kindiki na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wah wamependekeza kwamba mwongozo huo mpya upewe msingi wa kisheria ili serikali zijazo zisibadilishe mwelekeo wa taifa kila baada ya uchaguzi. Hata hivyo, changamoto kubwa kwa utawala wa Ruto itakuwa kuwashawishi wakosoaji kwamba mchakato huo ni wa kweli na haujalenga kuendeleza ajenda za kisiasa za serikali iliyopo madarakani. Baadhi ya viongozi wa upinzani tayari wanataka ukaguzi wa kina wa utekelezaji wa Ruwaza ya 2030 kabla ya kuanzishwa kwa mpango mwingine mpya. Kifo cha Raila Odinga Oktoba 2025 kilikatiza ndoto ya kongamano lake la kitaifa kabla ya kutekelezwa. Sasa mjadala wa Ruto kuhusu Kenya baada ya Ruwaza ya 2030 unaonekana kufufua kwa namna fulani baadhi ya mawazo hayo, lakini kwa sura mpya ya maendeleo na mipango ya muda mrefu ya taifa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 16 Aug 2026 09:55:37

Wakenya 40,000 wamefariki katika ajali za barabarani miaka 10-Ripoti

AJALI  za barabarani zimeendelea kuwa tishio kubwa Kenya, huku zaidi ya watu 40,000 wakifariki katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kulingana na takwimu za serikali. Jana, huzuni ilitanda eneo la Nthongoni, Kaunti ya Makueni, baada ya ajali mbaya ya barabarani kusababisha vifo vya watu saba na kujeruhi zaidi ya 60. Abiria walikuwa wakielekea sherehe ya kulipa mahari katika kijiji cha Inyoni, safari iliyotarajiwa kuwa ya furaha ikageuka kuwa ya majonzi. Kiongozi wa jamii Joseph Kyonda alieleza kuwa alipoteza majirani sita na kuomba msaada wa kifedha kwa mazishi yenye heshima. Basi dogo lenye viti 46 lilikuwa limebeba watu 71 wakati ajali ilitokea. Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti, Harvey Mulei, alisema Hospitali ya Matiliku ilipokea majeruhi 28 na Hospitali ya Rufaa ya Makueni ikapokea 36. Manusura walieleza kuwa taa za gari zilikatika kabla ya kuacha barabara na kutumbukia shimoni. Haya yanajiri huku takwimu zikionyesha kuwa miundombinu duni ya barabara, ukosefu wa madaraja ya watembeao kwa miguu na alama za trafiki na uzembe wa madereva na watembea kwa miguu ni sababu nyingi zinazochangia ongezeko la vifo na majeraha barabarani. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko inavyoonyeshwa na takwimu rasmi. WHO inaeleza kwamba, Kenya huhesabu tu vifo vinavyotokea mara moja baada ya ajali, huku wengi wanaofariki hospitalini siku au miezi kadhaa baadaye wakiachwa nje ya rekodi hizo. Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu Kenya (KNBS), watu 114,466 walihusika katika ajali za barabarani kati ya 2021 na 2025. Katika kipindi hicho, watu 22,894 walifariki huku zaidi ya 90,000 wakijeruhiwa.  Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) inasema ongezeko la idadi ya watu, magari na msongamano wa trafiki limefanya hali kuwa mbaya zaidi.

read more