T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 05:55:32

Ngono, pombe, sigara zapigwa marufuku wakati wa tohara za Bukusu

KWA miezi mitano ijayo, maeneo ya Magharibi mwa Kenya yataingia katika msimu wa tohara za kitamaduni, huku wanaume wanaotekeleza jukumu hilo wakijitenga na maisha ya kawaida na kufuata kanuni kali. Wanaume hao wanaojulikana kama Ngariba kwa Kiswahili, na Omukhebi kwa lugha ya Bukusu, huamini kwamba tohara ni ibada muhimu ya kumfanya mvulana aingie katika utu uzima. Katika kipindi hicho, maisha yao hutawaliwa na nidhamu, kujinyima na uwajibikaji mkubwa. Hakuna kufanya ngono. Hakuna kuvuta sigara au kutumia dawa za kulevya. Hakuna kunywa pombe. Hakuna kuhudhuria mazishi. Na zaidi ya yote, hawapaswi kukiuka kanuni zinazohusiana na kisu kitakatifu kinachojulikana kama Lukhembe. Wanaotekeleza tohara hiyo wanaamini kwamba kuvunja kanuni hizo kunaweza kuathiri mchakato wa tohara na uponaji. Siminu Wekesa, aliye na tajriba kuhusu tohara, anasema marufuku hayo yanalenga kulinda heshima ya kiroho ya tohara, maadili ya jamii na usalama wa wavulana wanaopitia desturi hiyo. "Katika kipindi tunachowashughulikia wavulana katika tohara, haturuhusiwi kushiriki ngono hadi wavulana waanze kupona mwezi Oktoba kwa sababu ni kama kwenda vitani. Ukirejea au kuvunja kanuni hii, itachukua muda mrefu kwa watoto kupona kama inavyotarajiwa," anasema Bw Wekesa. Marufuku ya ngono pia inawahusu wanaume wanaoshughulikia Busaa, kinywaji cha kienyeji ambacho hutumika katika sherehe za kitamaduni. Kifo pia kinaweza kumlazimisha Omukhebi kujiondoa katika shughuli hizo. Ngariba anayefiwa na mtu wa karibu wa familia, hasa mke, anatarajiwa kusitisha shughuli hizo na kufanyiwa tambiko la kujitakasa kabla ya kurejea mwaka unaofuata. Uvutaji sigara na matumizi ya dawa nyingine za kulevya pia hauruhusiwi wakati wa msimu huo. Wapashaji tohara wanasema baadhi ya masharti hayo yanalenga pia kuwalinda wavulana dhidi ya maambukizi na matatizo mengine ya kiafya. Rajab Kituyi, aliyeanza kupasha tohara mwaka wa 1982, anasema pombe hairuhusiwi kwa sababu shughuli hiyo inahitaji mikono thabiti, umakini na uwezo mzuri wa kuona. "Haturuhusiwi kunywa pombe, ili kuepuka matitizo ya kuona au kushindwa kushikilia kisu vizuri wakati wa tohara," anasema. Omukhebi anatarajiwa kufanya kazi hiyo kwa usahihi mkubwa. Tohara isiyofanyika vizuri inaweza kumletea aibu na unyanyapaa Ngariba pamoja na mvulana, huku imani za kitamaduni pia zikihusisha makosa hayo na madhara ya kiroho. Kanuni hizo pia zinahusu uhusiano kati ya vizazi vya watoa tohara. Marufuku hiyo inalenga kuhifadhi heshima na uhusiano kati ya vizazi vya ngariba. Kisha kuna Lukhembe, kisu kitakatifu kinachotumiwa katika tohara. Kwa mujibu wa Bw Wekesa, kukiangusha kisu hicho, iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi, ni ukiukaji mkubwa wa kanuni. Ngariba anapaswa kusitisha shughuli mara moja na kusubiri msimu unaofuata. "Ukiangusha kisu, sitisha shughuli zako hadi msimu unaofuata. Ukipuuza na kuendelea na tohara, utaleta aina fulani ya mkosi," anasema. Ngariba anapaswa kuondoka kimya kimya na kuepuka kueleza yaliyotokea njiani kuelekea nyumbani. Bw Wekesa anasema akiulizwa maswali, anapaswa kujibu neno moja pekee, "Ahoro". Ngariba pia wanatarajiwa kuwa watu wenye maadili mema, wenye nidhamu na wanaoweza kuwa mifano kwa jamii. Pia hawapaswi kuwa na historia ya uhalifu. Kwa jamii ya Bukusu, tabia ya mtu anayemshughulikia mvulana inaweza kuathiri namna anavyoingia utu uzima. Hasira, ugomvi na mabishano pia hayaruhusiwi. Wakati wa msimu wa tohara, watoa tohara wanatarajiwa kubaki watulivu hata wanapochokozwa. Pamoja na kanuni hizo za kitamaduni, kuna umuhimu wa usafi na viwango vya kisasa vya usalama. Bw Wekesa, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wapashaji Tohara Kaunti ya Bungoma, anasema wazazi wanapaswa kuhakikisha mtu anayefanya tohara amepata mafunzo na cheti kutoka serikalini. "Usafi si jambo la kujadiliwa wakati wa tohara. Walioidhinishwa pekee ndio wanaoruhusiwa kufanya shughuli hiyo, na yeyote anayefanya bila cheti atachukuliwa hatua za kisheria," anasema. Ngariba wanapaswa kudumisha usafi wa mwili, kukata kucha ziwe fupi, kuvaa vizuri na kuhakikisha mazingira pamoja na vifaa vinavyotumiwa ni safi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 06:55:12

Seneti yapinga uamuzi wa mahakama kuwa ilikiuka haki za Gachagua

SENETI imewasilisha rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba maseneta walikiuka haki ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ya kusikilizwa kwa haki wakati wa mchakato wa kumtimua mamlakani. Seneti pia inapinga fidia ya Sh50 milioni ambayo Mahakama Kuu ilimpa Gachagua kwa ukiukaji huo wa haki zake. Rufaa hiyo iliwasilishwa mwezi mmoja baada ya Gachagua mwenyewe kukata rufaa kupinga sehemu kubwa ya uamuzi wa Mahakama Kuu, ikiwemo uamuzi uliothibitisha kutimuliwa kwake na kuidhinisha Profesa Kithure Kindiki kuwa mrithi wake. Hata hivyo, Gachagua hakupinga sehemu ya uamuzi iliyosema haki zake zilikiukwa wala fidia ya Sh50 milioni. Seneti, kupitia Spika wake na Seneti yenyewe, inalenga kubatilisha sehemu za uamuzi wa Juni 8 zilizowalaumu maseneta kwa kukataa ombi la kuahirishwa kwa kikao cha mchakato wa kumtimua Gachagua na kuamuru alipwe fidia. Katika hati yake ya rufaa, Seneti inataka Mahakama ya Rufaa ibatilishe au ibadilishe maagizo hayo pamoja na kuamuru gharama ya kesi ilipwe. Seneti inasema majaji walikosea walipoamua kwamba uamuzi wake wa kukataa kuahirisha mchakato huo ulikiuka haki ya Gachagua ya kusikilizwa kwa haki. Inasema majaji hawakutathmini ipasavyo masharti ya Katiba katika Ibara ya 47 na 50 na hawakutambua kwamba Seneti ilitumia mamlaka yake ya kufanya uamuzi kuhusu ombi hilo. Seneti pia inasema majaji walikosea baada ya kukiri kwamba Gachagua alipewa nafasi ya kujitetea, lakini baadaye akawalaumu maseneta kwa kuendelea na mchakato huo baada ya yeye kutofika. Kwa mujibu wa Seneti, Gachagua alipewa muda zaidi kwa ombi la mawakili wake na Bunge lilikuwa na wajibu wa kukamilisha mchakato wa kumtimua bila kuchelewa. Seneti pia inawashutumu majaji kwa "kunyakua mamlaka ya kufanya uamuzi" ya Seneti na kutumia tathmini yao wenyewe kuamua iwapo ombi la kuahirisha kikao lilipaswa kukubaliwa. Hati hiyo inasema ombi la kuahirisha mchakato liliwasilishwa kwa kura na likakataliwa baada ya maseneta kuzingatia mazingira yaliyokuwepo wakati huo. Seneti pia inapinga uamuzi kwamba kutokuwepo kwa Gachagua kulihalalishwa na ugonjwa. Inasema hakuna ushahidi uliowasilishwa mbele yake wakati huo kuthibitisha kwamba alikuwa mgonjwa. "Majaji walikosea kisheria na kimantiki walipoamua kwamba kutokuwepo kwa Gachagua kulihalalishwa kwa sababu ya ugonjwa, licha ya kwamba hakuna ushahidi uliowasilishwa mbele ya Seneti wakati huo kuthibitisha ugonjwa huo uliodaiwa," inasema rufaa hiyo. Seneti sasa inataka Mahakama ya Rufaa ibatilishe uamuzi kwamba haki za Gachagua za kusikilizwa kwa haki zilikiukwa na pia iondoe agizo la kulipa Sh50 milioni. Mzozo huo ulitokana na mchakato wa kumtimua Gachagua uliofanyika Oktoba 2024 baada ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse kuwasilisha hoja iliyokuwa na malalamishi 11 dhidi yake. Bunge la Kitaifa liliidhinisha hoja hiyo na kuiwasilisha Seneti, ambayo ilithibitisha mashtaka matano kabla ya kumwondoa Gachagua afisini. Gachagua na watu wengine baadaye walipinga mchakato huo, wakidai kwamba haukuhusisha ushiriki wa kutosha wa umma, kulikuwa na upendeleo, taratibu za Bunge zilikiuka Katiba na haki zake zilikiukwa. Mahakama Kuu ilikataa malalamishi yao mengi na kuthibitisha kutimuliwa kwake, pamoja na uteuzi na kuidhinishwa kwa Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais. Hata hivyo, majaji walipata kasoro katika namna Seneti ilivyoshughulikia utetezi wa Gachagua. Walibaini kuwa Seneti iliendelea na mchakato huo baada ya Gachagua kuugua kabla hajatoa ushahidi mwenyewe.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 07:55:54

Askofu, mbunge watofautiana kuhusu mchango wa Ruto matangani

IBADA ya mazishi ya marehemu Mchungaji Silvanus Mwakoma katika eneo la Kirutai, Voi, iligeuka kuwa uwanja wa malumbano ya kisiasa baada ya Mbunge wa Taveta John Bwire na Askofu Mkuu Liverson Mng'oda kutofautiana kuhusu mchango wa Rais William Ruto kwa familia ya marehemu. Katika hotuba yake, mbunge huyo alimsifu marehemu kama mfuasi wa Rais Ruto na serikali yake. Alitaja miradi kadhaa ya serikali katika kaunti hiyo, akisema Rais Ruto amekuwa akichangia maendeleo ya Taita-Taveta. Bwire pia alitangaza mchango wa Sh500,000 kutoka kwa Rais Ruto, huku yeye mwenyewe akitoa Sh100,000. Hata hivyo, wakati wa mahubiri, Askofu Mng'oda alikosoa vikali kauli hizo, hasa kuhusu maendeleo ya serikali katika eneo hilo. Askofu huyo alilalamikia hali ya barabara na ukosefu wa maji, akipinga picha ya maendeleo iliyokuwa imewasilishwa na mwanasiasa huyo. Pia alikosoa namna mchango huo ulivyotangazwa, akidai ulitolewa kwa mtindo wa majivuno na madai ya kustahili sifa. Katika kauli iliyowashangaza waombolezaji, Mng'oda aliishauri familia kutotumia fedha hizo kusomesha watoto wa marehemu na hata kupendekeza zirudishwe ikiwa ingewezekana. Lakini familia haikuunga mkono msimamo huo. Katika hotuba ya shukrani, ndugu wa marehemu aliishukuru serikali kwa mchango wa Sh500,000 na Bwire kwa Sh100,000. Alisema fedha hizo zitatumika kuwasaidia watoto wa marehemu. Malumbano hayo yalifanya mazishi hayo kugeuka kutoka hafla ya kuaga marehemu hadi mjadala kuhusu siasa, maendeleo na matumizi ya mchango wa Sh600,000.

read more