T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 11:05:02

Himizo kilimo cha kuhifadhi afya ya udongo na nishati ya jua kuunganishwa ili kupunguza gharama

MABADILIKO ya tabianchi yanaendelea kubadilisha kwa kasi mifumo ya kilimo nchini Kenya, huku misimu ya mvua na ukame ambayo wakulima walitegemea ikizidi kuwa isiyotabirika. Ukame unadumu kwa muda mrefu, mvua ikichelewa au kunyesha kwa muda mfupi, huku joto linaloongezeka likiharibu rutuba ya udongo. Wakati huohuo, gharama ya mafuta ya petroli, mbolea na pembejeo nyingine imepanda kutokana na misukosuko inayoendelea katika nchi za Milki za Kiarabu, na kufanya uzalishaji wa chakula kuwa ghali zaidi. Wataalamu sasa wanapendekeza kuunganisha kilimo kinachofufua hadhi ya udongo, kwa Kiingereza Regenerative Agriculture (RA) na matumizi ya nishati ya jua, yaani productive use of renewable energy (PURE) katika uzalishaji ili kujenga mifumo ya chakula inayostahimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi. Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa kuhusu Regenerative Agriculture (RA) na Productive Use of Renewable Energy (PURE) ulioandaliwa na SNV kwa ushirikiano na AGRA, majuzi, Qureish Noordin, Kiongozi wa Kiufundi wa Regenerative Agriculture AGRA, alisema afya ya udongo na nishati safi lazima viende sambamba. [caption id="attachment_191143" align="aligncenter" width="300"] Qureish Noordin, Kiongozi wa Kiufundi wa Regenerative Agriculture AGRA wakati wa mahojiano Jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Regenerative Agriculture hulenga kurejesha afya ya udongo kupitia matumizi ya mbolea zenye kaboni, mzunguko wa mazao, kilimo mseto, kilimo cha miti, nyasi za boji (mulching) na usimamizi bora wa rutuba ya udongo," Qureish akasema. Kwa upande mwingine, nishati ya jua inaweza kuendesha pampu za umwagiliaji mimea na maji mashamba kwa kutumia mifereji, mashine za kukausha nafaka, mashine za kupura, vifaa vya kupooza maziwa na maghala ya mifumo ya baridi, hivyo kupunguza gharama na hasara baada ya mavuno. Utafiti wa SNV katika kaunti saba mapema kwa huu, 2026, ulionyesha kuwa gharama kubwa za teknolojia zilichangia asilimia 35 ya changamoto za matumizi, ukifuatiwa na mahitaji ya wafanyakazi kwa asilimia 22 na ukosefu wa maarifa kwa asilimia 20. "Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 79 ya wakulima hutumia samadi ya mifugo, asilimia 74 hulima mazao mseto, huku asilimia 73 wakifanya mzunguko wa mazao (crop rotation)," akadokeza Judith Libaisi kutoka SNV. Hata hivyo, matumizi ya kilimo cha miti na kilimo cha kuhifadhi udongo bado ni madogo. [caption id="attachment_191144" align="aligncenter" width="300"] Judith Libaisi kutoka SNV wakati wa mahojiano Jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Libaisi alisema wakulima wanahitaji teknolojia pamoja na mafunzo ya kilimo, matengenezo, huduma baada ya mauzo na ushauri wa kitaalamu ili kupata manufaa kamili. Kwa mkulima Esther Wariara kutoka Githunguri, Kiambu, matumizi ya pampu ya sola yamepunguza gharama za umwagiliaji kwa karibu asilimia 50, akisema sasa anatumia karibu Sh250 kwa siku badala ya Sh500. "Kilimo hakiwezi kufanyika bila nishati," alisema Dkt Kiplimo Lagat, Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Nandi, wakati wa hafla ya Regenerative Agriculture (RA) na Productive Use of Renewable Energy (PURE) iliyofanyika Jijini Nairobi Julai 2026. Waziri huyo wa Kaunti (CEC), aidha, alisisitiza kuwa nishati safi ya jua inaweza kusaidia kuziba pengo la uzalishaji wa chakula nchini Kenya na Afrika, ikizingatiwa kuwa wakulima wanapotumia sola kupampu maji na pia kukausha mazao ili kurefusha muda wa kudumu hupunguza gharama ya uzalishaji kwa kiwango kikubwa.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 12:02:06

Watengenezaji wa chakula cha mifugo wahamasisha kilimo cha mahindi ya manjano kuziba pengo la malighafi

MABADILIKO ya tabianchi, ukame wa muda mrefu na mvua zisizotabirika vinaendelea kuathiri uzalishaji wa mazao nchini Kenya, hali inayowasukuma watengenezaji wa chakula cha mifugo kuhimiza kilimo cha mahindi ya manjano ili kupunguza utegemezi wa malighafi kutoka nje na gharama za uzalishaji. Chama cha Watengenezaji wa Chakula cha Mifugo Kenya (AKEFEMA) kinaitaka serikali, watafiti na wakulima kuhamasisha uzalishaji wa mahindi ya manjano kwa ajili ya chakula cha mifugo, huku mahindi meupe yakitengwa zaidi kwa matumizi ya binadamu. "Malighafi huchangia kati ya asilimia 70 na 80 ya gharama ya kutengeneza chakula cha mifugo. Kenya bado inaagiza malighafi nyingi kutoka nje, licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha sehemu kubwa humu nchini," alisema Mwenyekiti wa AKEFEMA Joseph Karuri. [caption id="attachment_191153" align="aligncenter" width="300"] Mahindi shambani yakiendelea kukua. Picha|Sammy Waweru[/caption] Karuri alisema mahindi ndiyo chanzo kikuu cha virutubisho vya wanga (carbohydrates) katika chakula cha mifugo, lakini uhaba wa mahindi kwa matumizi ya binadamu unalazimisha wafugaji kushindana na watu kwa nafaka hiyo. Chama hicho pia kinataka kuongezwa kwa uzalishaji wa alizeti, soya, pamba na canola, ambazo mabaki yake baada ya kukamua mafuta hutumika kama chanzo muhimu cha protini katika chakula cha mifugo. Karibu asilimia 80 ya malighafi hizo za protini huagizwa kutoka Tanzania, Uganda, Malawi na Zambia. Kenya hutumia takriban magunia milioni saba ya mahindi ya kilo 90 kila mwaka kutengeneza chakula cha mifugo, sawa na tani 630,000. Ingawa uwezo wa viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo ni karibu tani milioni nne kwa mwaka, uzalishaji halisi ni tani milioni 2.5 pekee kutokana na uhaba wa malighafi. [caption id="attachment_191155" align="aligncenter" width="300"] Mkulima akikagua shamba lake la mahindi katika kaunti ya Kiambu. Picha|Sammy Waweru[/caption] Karuri alisema kuboresha lishe ya mifugo ni muhimu kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai. Kenya huzalisha karibu lita bilioni tano za maziwa kwa mwaka, lakini ng'ombe mmoja hutoa wastani wa lita saba hadi nane kwa siku. Aidha, AKEFEMA pia inahimiza matumizi ya teknolojia ya Near Infrared (NIR), inayowezesha kuchanganua ubora wa malighafi ndani ya dakika tano hadi 10 na kusaidia wataalamu kutengeneza mchanganyiko sahihi wa chakula. Makamu Mwenyekiti wa AKEFEMA, Dkt David Murumba, alisema teknolojia hiyo inaweza kupunguza upotevu wa malighafi wakati wa uundaji wa malisho, kuongeza ufanisi na kuboresha afya ya mifugo. [caption id="attachment_191156" align="aligncenter" width="300"] Chama cha Watengenezaji wa Chakula cha Mifugo Kenya (AKEFEMA) kinaitaka serikali, watafiti na wakulima kuhamasisha uzalishaji wa mahindi ya manjano kwa ajili ya chakula cha mifugo. Picha|Sammy Waweru[/caption] Katibu Mkuu wa AKEFEMA, Dkt Wilfred Kamau, alisema uwekezaji katika mashine za kisasa, wataalamu na mikopo nafuu ni muhimu kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye bei ya maziwa, mayai na nyama ya nguruwe kwa walaji pia itashuka.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 02:55:48

Mgogoro: Ajabu wakifariki saa 3 baada kuoana

WALIANZA maisha yao ya ndoa saa 10 jioni Agosti 9, 2026, lakini kufikia saa moja na nusu usiku siku hiyo wote walikuwa wamefariki. Patrick Mwangi, 28, na Jackline Wambui, 25, walikuwa wameanza maisha yao ya ndoa katika Kijiji cha Nyerere, Murang'a, lakini ikawa ndoa ya muda mfupi zaidi kuwahi kushuhudiwa na baadhi ya wakazi. Polisi wanachunguza vifo hivyo, ambavyo mwanzoni vilionekana kuwa mauaji yaliyotekelezwa na mmoja wao kisha akajiua. Inadaiwa Mwangi alimnyonga Wambui kwa kamba alipokuwa amelala, kabla ya kutoka nje ya nyumba iliyokuwa imekusudiwa kuwa makazi yao mapya na kujinyonga. Wapenzi hao walikuwa wamechumbiana kwa takriban miaka mitatu, kipindi kilichojaa migogoro kiasi kwamba wazazi wao walilazimika kuingilia kati mara kadhaa kuwapatanisha. Mwangi alikuwa mwendesha bodaboda, huku Wambui akifanya kazi za vibarua mara kwa mara. Mama ya Mwangi, Bilha Wangare, alisema bado hawezi kuelewa uhusiano wa wawili hao. "Ulikuwa upendo ulioonekana kama uchawi. Wote walikuwa na mapenzi makali ambayo ilikuwa vigumu kuelewa. Nilishiriki katika mikutano mingi ya kuwapatanisha ili wasameheane. Nadhani neno linalowafaa ni wapenzi wapumbavu," alisema. Kwa mujibu wake, waligombana kwa sababu ya mambo mbalimbali, ikiwemo simu, pesa na burudani. Wambui aliwahi kulalamika kwamba Mwangi hakumpeleka kujivinjari mara kwa mara kama alivyotaka. Mwangi naye alimshutumu kwa kuiba Sh100,000 kutoka kwake. Wambui pia alilalamika kwamba Mwangi alikuwa akiwasaidia wazazi wake kifedha kupita kiasi, akitaka familia yake ipewe kipaumbele. Mwaka huu, alianza kumtaka Mwangi amkabidhi cheti cha umiliki cha pikipiki yake na hati miliki ya shamba la ekari 0.1 alilonunua Makuyu, Maragua. Wakati huo hawakuwa wakiishi pamoja, lakini mara kwa mara Wambui angelala katika nyumba ndogo ya Mwangi. Katika juhudi za kuwapatanisha, Bi Wangare aliwaita kwenye kikao Agosti 4 na kupendekeza waanze kuishi pamoja. Mwangi alitaka Wambui kwanza azae mtoto wake, huku Wambui akitaka cheti cha pikipiki na hati ya kumiliki shamba. Hatimaye walikubaliana kwamba Mwangi angemfungulia biashara katika soko la Irembu, naye akakubali kwamba angepata mimba haraka iwezekanavyo. Baada ya Wambui kuondoka, Mwangi alimkabidhi mama yake hati hizo akisema hamwamini. Mnamo Agosti 6, Wambui alimpigia simu Bi Wangare na kumwambia alikuwa ameamua kuolewa na Mwangi na angehamia kwake Agosti 9. Saa 10 jioni siku hiyo, Wambui alifika na kumkuta Mwangi akimsubiri. Baada ya muda mfupi, Mwangi alimbeba kwa kwenye pikipiki na wakaondoka. Walirejea karibu saa moja jioni. Bi Wangare alisema Wambui alionekana mchovu, mwenye usingizi na kama aliyelewa. Muda mfupi baadaye, Mwangi aliingia nyumbani kwa wazazi wake na kuzungumza nao. Alisalimia kila mmoja na kuwaaga. Kabla ya kuondoka, alimwambia mama yake kwamba Wambui alikuwa ameweka picha ya mwanaume mwingine kwenye mitandao ya kijamii na pia kumtumia picha hiyo. Alidai Wambui alikuwa amemwambia kwamba asipomtunza vizuri, angemwacha aende kwa mwanaume huyo. Baada ya Mwangi kuondoka, Bi Wangare alisema alipata hisia za ajabu. Alichukua tochi na kumtafuta mwanawe.Alimwita Wambui pia, lakini hakukuwa na jibu. Mlango wa nyumba ya Mwangi ulikuwa wazi. Alimulika nyuma ya nyumba na kumwona mwanawe akiwa amejinyonga. Alipiga mayowe, na mumewe Samuel Kimani pamoja na majirani wakafika. Walipoingia ndani ya nyumba, walimkuta Wambui pia amefariki. Miili hiyo ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Maragua Level Four. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Murang'a Cleti Kimaiyo alisema vifo hivyo vinachunguzwa, ingawa kwa mtazamo wa awali vilionekana kuwa mauaji yaliyofuatwa na kujiua. Alisema polisi wako tayari kufuatilia mwelekeo mwingine iwapo ushahidi mpya utaibuka. Shangazi ya Wambui, Tabitha Njoki, alisema kifo hicho kimeacha familia katika mshangao. Wambui alikuwa mama wa mtoto wa kike wa miaka mitano. "Aliniambia kwamba alikuwa akihamia( kwa Mwangi) kuolewa. Sikujua kwamba angekuwa katika ndoa kwa zaidi ya saa tatu tu. Mungu atuhurumie," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 03:55:58

Jumwa aingia boksi ya Kalonzo baada ya kutema UDA

ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia, Aisha Jumwa amejiunga rasmi na chama cha Wiper Patriotic Front, akisema yuko tayari kukabiliana na vyama vinavyounga mkono serikali jumuishi katika uchaguzi wa 2027. Bi Jumwa alipokelewa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika eneo la Kakuyuni, Kilifi, ambapo aliahidi kufanya kampeni za kuimarisha upinzani Pwani na nchini. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza nguvu za Wiper katika eneo la Pwani, huku Bi Jumwa akihusishwa na mipango ya kuwania kiti cha ugavana wa Kilifi mwaka wa 2027. Bw Musyoka alimkaribisha Bi Jumwa na kuahidi kumuunga mkono katika kinyang'anyiro hicho. Kalonzo alisema kujiunga kwa Bi Jumwa kutaimarisha upinzani katika eneo la Pwani. Bi Jumwa alisema wakazi wa Kilifi wamechoshwa na siasa za serikali jumuishi na wanapaswa kuunga mkono upinzani. "Hakuna tena serikali jumuishi katika Kaunti ya Kilifi kwa sababu wao ni wasaliti," alisema. Alisema atashirikiana na Wiper kuipaka Pwani "rangi ya samawati" kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Musyoka aliwaonya viongozi wa upinzani dhidi ya kuvunja muungano wao na kujiunga na Serikali ya Kenya Kwanza, akisema hatua hiyo itakuwa usaliti kwa Wakenya wanaotaka mabadiliko katika uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka alisema viongozi wa upinzani lazima wabaki pamoja na kuweka kando maslahi yao binafsi wanapojenga muungano wenye nguvu wa kumkabili Rais William Ruto. Aliwafananisha viongozi watakaoacha muungano huo na mke wa Lutu katika Biblia, ambaye aligeuka kuwa nguzo ya chumvi baada ya kugeuka nyuma licha ya kuonywa. "Wenzangu katika upinzani... tukikubaliana na kuungana, na mmoja wetu aamue kurudi nyuma, atageuka kuwa chumvi," alisema Kalonzo huko Kakuyuni, Kilifi. Kalonzo alisema upinzani unahitaji kuimarisha ushawishi wake Pwani na nchini kote ili kuondoa serikali ya Kenya Kwanza madarakani. Alisema vijana waliofikisha miaka 18 wanapaswa kupata vitambulisho na kujisajili kama wapiga kura katika zoezi la usajili wa watu wengi litakalofanyika Novemba.

read more