T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 14:59:24

ODM yaanza kujivumisha ikilenga kudumisha umaarufu wake Nairobi

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kaunti ya Nairobi kimeanzisha kampeni ya kuimarisha umaarufu wake mashinani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hii ni siku chache baada ya kushiriki mkutano wa pamoja na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto, uliofanyika Naivasha, Nakuru. Katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi Alhamisi, ulioongozwa na mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema wataimarisha ngome za ODM jijini Nairobi huku wakihamasisha wapiga kura kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa urais. "Mikakati yetu ni kulinda ngome za ODM huku tukihamasisha wapiga kura kumuunga mkono rais. Tutatumia mitandao yetu ya mashinani, matawi na viongozi wa wadi kuhakikisha makubaliano ya kisiasa tuliyofikia yanageuzwa kuwa kura," akasema Bw Aladwa. Viongozi hao walisema wataendelea kujenga na kuimarisha ODM huku wakitekeleza majukumu yaliyoafikiwa chini ya Serikali Jumuishi. "Ujumbe kutoka Nairobi ni kuwa ODM itabaki imara, itashinda viti zaidi na kutimiza ahadi zake. Nawahimiza viongozi wote wa matawi na maafisa wa chama kubaki pamoja, wawe wenye nidhamu na kuzingatia malengo ya chama. Tuipange Nairobi, tuimarishe ngome zetu, tushinde viti zaidi na kutimiza ahadi zetu," akasema. Kwa mujibu wa Bw Aladwa, ushindi katika uchaguzi wa 2027 utategemea mipango madhubuti na uhamasishaji wa wapigakura mashinani. Alisisitiza umuhimu wa kampeni za amani na kuheshimu wagombea wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa. "Hakuna haja ya matusi. Tunamwambia Rigathi Gachagua aache kumtusi Rais na awe tayari kukabiliana naye katika uchaguzi wa 2027," akasema. Viongozi hao pia walitangaza kuwa mbali na kudai nafasi ya Naibu wa Rais itengewe ODM, chama hicho pia kitataka nafasi ya Gavana wa Nairobi pamoja na viti vingine vya kisiasa. "Tumekubaliana kwamba tunaanza na kiti cha Naibu Rais, ugavana Nairobi, diwani na viti vingine vyote vya kuchaguliwa vipewe ODM. Hatutaruhusu kugawana maeneo hapa; ODM iendelee kushikilia nafasi zake katika maeneobunge ambayo kwa sasa ina nguvu," akasema Bw Aladwa. Alisema chama kinaunga mkono Ruwaza ya 2060 iliyozinduliwa Jumatano, akisema Kenya inahitaji mpango wa muda mrefu wa maendeleo baada ya Ruwaza ya 2030. Kiongozi wa vijana Stazo Omung'ala alisema wanachama wa ODM wataunga mkono uamuzi wa kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, kwamba ODM haitawasilisha mgombea wa urais katika uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 14:05:10

Funzo kutoka kwa tume ya Chebukati ni kwamba IEBC isiogope maoni kinzani

MGAWANYIKO uliokumba IEBC baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 haukuwa tu mzozo wa kisiasa, bali dalili ya mgororo uliokuwa umetokota ndani ya tume. Kilichotikisa imani ya umma si tofauti za kimaoni miongoni mwa makamishna, bali namna tofauti hizo zilivyojitokeza hadharani wakati Wakenya wakisubiri taasisi iliyopaswa kuzungumza kwa sauti moja kutoa mwelekeo muhimu. Hakuna taasisi ya kidemokrasia inayopaswa kuogopa maoni tofauti. Kinachodhoofisha taasisi ni kuyaficha, kuyanyamazisha au kuyasukuma hadi yalipuke mbele ya umma. Uwazi hujenga uaminifu, huku ukimya na kuficha tofauti zikizalisha mashaka. IEBC mpya inapaswa kujifunza kutokana na yaliyotokea mnamo 2022. Mwenyekiti si mmiliki wa tume, wala makamishna si watazamaji. Sheria imeweka tume ya pamoja ambayo maamuzi yake yanapaswa kujengwa kupitia majadiliano, uwajibikaji na kuheshimiana. Tofauti za kitaaluma zinapaswa kushughulikiwa ndani ya vikao vya tume, badala ya kujitokeza hadharani wakati wa kutangaza matokeo. Funzo kutokana na tume ya Wafula Chebukati si kwamba makamishna hawapaswi kutofautiana. Ni kwamba, tofauti hizo zinapaswa kusimamiwa kwa uwazi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria kabla hazijageuka kuwa mgogoro wa kitaifa. Uchaguzi haujengwi kwa kura pekee; hujengwa pia kwa imani ya wananchi kwa mwamuzi. IEBC ikipoteza imani hiyo, hata uchaguzi ulioendeshwa kwa usahihi unaweza kutiliwa shaka. Utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na kuheshimu maoni ya ndani ndio msingi wa kurejesha na kulinda imani hiyo. Ondieki ni mwalimu wa Kiswahili

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 13:22:38

Rafiki yangu wa kiume alinitafutia kazi, sasa mume amekasirika

Shangazi. Nina rafiki wa kiume ambaye tumejuana tangu chuo kikuu. Hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yetu na mume wangu anamjua. Hata hivyo, baada ya rafiki huyo kunisaidia kupata nafasi ya kazi, mume wangu alianza kumshuku. Sasa anataka niache kabisa kuwasiliana naye. Anasema mwanaume na mwanamke hawawezi kuwa marafiki bila mmoja kuwa na nia tofauti. Mimi sitaki kumpoteza rafiki yangu, lakini pia sitaki ndoa yangu iwe na mashaka kila siku. Nimechanganyikiwa. Urafiki wa watu wa jinsia tofauti unawezekana, lakini mipaka yake lazima iwe wazi, hasa ndani ya ndoa. Jiulize kama mawasiliano yako na rafiki huyo yangeonekana ya kawaida iwapo mume wako angekuwa karibu. Epuka siri, mazungumzo ya usiku yasiyo ya lazima au ukaribu unaoweza kuonekana kama uhusiano wa kimapenzi. Wakati huo huo, mume wako hapaswi kutumia wivu kukutenga na kila mtu. Binti yangu anachafuka mno, ni kawaida? Nina binti wa miaka 15 ambaye ni mwerevu sana darasani lakini chumba chake kinaonekana kama eneo lililopigwa na kimbunga. Nguo ziko kila mahali, vitabu vimetapakaa na hata vikombe vya chai hukaa humo kwa siku kadhaa. Kila nikimwambia asafishe, anasema ataifanya baadaye lakini hachukui hatua yoyote. Nimeanza kuogopa kuwa tabia hii itamfuata hadi utu uzima. Nifanyeje? Vijana wengi hupitia Tatizo kama hilo. Badala ya kumfokea kila siku, msaidie kuona umuhimu wa usafi na mpangilio katika maisha ya kila siku. Weka matarajio ya wazi na majukumu maalum. Pia mfundishe kwa mfano badala ya maneno pekee. Usafi wa mazingira hujenga nidhamu, uwajibikaji na hata afya ya akili. Tabia hizi hujengwa taratibu kupitia mwongozo unaofaa. Mwanangu amekuwa mkora sana Nilianza kumpa mwanangu aliye chuoni pesa kila wiki kwa ajili ya chakula na usafiri. Baada ya muda niligundua kwamba baadhi ya matumizi aliyokuwa akiniambia hayakuwa ya kweli. Alikuwa akisema pesa zimetumika kununua vitabu, kumbe alikuwa akitumia sehemu yake kupiga sherehe. Nifanyeje. Uongo wake unapaswa kushughulikiwa, lakini lengo liwe kumfundisha uwajibikaji, si kumwangamiza. Mkae chini mtengeneze bajeti na umweleze wazi kiasi utakachompa na matumizi yanayotarajiwa. Badala ya kumtumia pesa bila mpango, unaweza kumshirikisha katika kupanga mahitaji yake. Pia mfundishe kuwa uhuru unaambatana na uwajibikaji. Akifanya makosa, lazima akabiliane na matokeo yake. N'nahofu kufika umri wa kuzeeka Shangazi, nimefikisha miaka 50 na nimeanza kuona mabadiliko mengi mwilini. Nguvu zimepungua na sura si kama zamani. Wakati mwingine nahisi kama thamani yangu inapungua kadri ninavyozeeka. Hali hii inanihuzunisha. Nifanyeje? Kuzeeka si adhabu bali ni zawadi ambayo wengi hawakupata. Uzuri wa ujana hupungua, lakini hekima, uzoefu na utulivu huongezeka. Angalia maisha uliyojenga, watu uliowagusa na changamoto ulizoshinda.

read more