T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 04:55:55

Jiandae kwa mwaka mgumu, Kalonzo amuonya Ruto

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Party, Kalonzo Musyoka, amemuonya Rais William Ruto kwamba mwaka wake wa mwisho mamlakani utakuwa mgumu, huku upinzani ukiahidi kuongeza ukosoaji wa serikali kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka alisema sauti ya upinzani itabadilika na kuwa kali zaidi katika siku 365 zijazo, huku akimshutumu Rais Ruto kwa kukiuka Katiba na kushindwa kutekeleza ahadi za manifesto ya Kenya Kwanza. "Tutaweka kila kitu wazi na kuwaeleza Wakenya jinsi Rais Ruto amekiuka Katiba na kufanya kinyume na manifesto yake," alisema. Kiongozi huyo wa Wiper alianza ziara ya siku tano Pwani Jumatano, akitarajiwa kuzuru Kwale, Kilifi, Mombasa na Taita-Taveta. Alianza ziara hiyo kwa kuhudhuria mkutano mkuu wa kila mwaka wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) huko Diani, Kwale, kabla ya mikutano ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya Pwani. Bw Musyoka pia alitumia ziara hiyo kushinikiza serikali kutatua mzozo wa kidiplomasia kati ya Kenya na Sudan uliosababisha kusimamishwa kwa uuzaji wa bidhaa za Kenya, ikiwemo chai. Sudan ilisimamisha uagizaji wa bidhaa kutoka Kenya Machi 2025 baada ya Nairobi kuandaa mkutano wa viongozi wa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), hatua ambayo Khartoum ilisema ilikuwa kuingilia masuala yake ya ndani. Kabla ya marufuku hiyo, Sudan ilikuwa ikiagiza takriban kilo milioni 35 za chai ya Kenya kila mwaka, zenye thamani ya dola milioni 69. Bw Musyoka alisema amekutana na Balozi wa Sudan nchini Kenya, Kamal Gubara, na kujadili namna ya kumshawishi Rais wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kuondoa marufuku hiyo. "Tulipatana kwamba atapeleka mazungumzo kwa viongozi wa juu ili kuomba Rais Burhan aondoe marufuku na kuwezesha biashara kati ya Kenya na Sudan," alisema. Bw Musyoka pia aliishutumu serikali kwa madai ya kuruhusu bandari ya Mombasa kutumiwa kuingiza silaha zinazolengwa Sudan, akisema hatua hiyo imechangia kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa East Africa Tea Trade Association George Omuga, alisema zaidi ya kilo milioni 3.44 za chai zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 10.3 bado zimekwama katika maghala ya Mombasa. Alisema chai hiyo ilikuwa imechanganywa na kufungashwa maalum kwa ajili ya soko la Sudan na hivyo ni vigumu kuipeleka katika masoko mengine. Bw Omuga alisema kufunguliwa kwa soko la Sudan kutawasaidia wakulima, wafanyabiashara na wauzaji wa chai nchini Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 03:55:52

Ruto aiga Kibaki kuzindua ruwaza ya maendeleo

RAIS Mwai Kibaki alipozindua mpango wa Ruwaza ya Kenya 2030 mwaka 2008, aliipa nchi mwelekeo wa maendeleo wa muda mrefu. Karibu miongo miwili baadaye, Rais William Ruto sasa anataka Wakenya waamue taifa litachukua mkondo gani baada ya 2030. Akizindua rasmi mdahalo wa kitaifa kuhusu Mustakabali wa Kenya Baada ya Ruwaza ya 2030 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi jana, Dkt Ruto alisema taifa linahitaji mwongozo mpya wa maendeleo wa muda mrefu unaotokana na matarajio ya wananchi badala ya mahitaji ya kisiasa ya muda mfupi. Rais alisema serikali itatoa jukwaa na rasilimali za kuwezesha mchakato huo, lakini itaacha Wakenya wenyewe waamue maudhui na mwelekeo wa ruwaza hiyo mpya. "Tofauti na miradi ya kawaida ya serikali, huu si mradi wa serikali. Huu ni mradi wa wananchi," alisema Dkt Ruto.Alisisitiza kuwa serikali haitadhibiti mjadala huo. "Serikali haitaongoza mazungumzo. Tutatoa jukwaa ili wananchi waamue," alisema huku akiwahimiza Wakenya kuwasilisha mawazo mbalimbali kuhusu mustakabali wa nchi. Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa kisiasa, magavana, wafanyabiashara, viongozi wa kidini, wanaharakati wa kijamii, wasomi, wanafunzi na watoto, ambao walitoa maoni tofauti kuhusu Kenya wanayotamani kuona siku zijazo. Miongoni mwa walioibua hisia nyingi alikuwa Adrian Ombuni mwenye umri wa miaka saba. "Ndoto yangu kwa Kenya ni kuona shule nzuri kwa watoto wote, hospitali bora kwa kila mtu, maji safi kwa kila nyumba, barabara safi kila mahali na ajira kwa vijana," alisema. Ingawa Adrian ni mdogo mno kuelewa siasa au sera za kiuchumi, kauli yake ilielezea kwa urahisi changamoto kuu ya mjadala huo — jinsi ya kubadilisha ndoto za kitaifa kuwa maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi wa kawaida. Mwanaharakati Daisy Amdany alisema ifikapo mwaka 2060, Adrian atakuwa na umri wa miaka 41. "Kenya inayojadiliwa leo si ya viongozi walio madarakani pekee, bali ya Adrian na mamilioni ya vijana watakaorithi taifa hili," alisema. Katika hotuba yake, Rais Ruto alimpongeza Kibaki kwa kuanzisha Ruwaza ya 2030, akisema iliwezesha Kenya kuwa na malengo ya wazi ya maendeleo pamoja na mfumo wa kupima mafanikio. Hata hivyo, alikiri kuwa utekelezaji wa baadhi ya nguzo za ruwaza hiyo haukufanikiwa kikamilifu. "Katika nguzo zote, ni ile ya uchumi ambayo hatukufanya vizuri vya kutosha," alisema. Mwenyekiti wa Bodi ya Utekelezaji wa Ruwaza ya 2030, Dkt Emmanuel Nzai, alitetea mpango huo akisema umebadilisha nchi kwa kiwango kikubwa. "Ruwaza ya 2030 imebadilisha Kenya. Huu si uvumi, ni ushahidi wazi," alisema huku akitaja miradi mikubwa kama ukanda wa usafirishaji wa LAPSSET. Kwa upande wake, Gavana wa Kisumu Prof Anyang' Nyong'o, ambaye alikuwa miongoni mwa wataalamu waliohusika kuandaa Ruwaza ya 2030, alisema ni muhimu kuanza sasa kupanga maisha ya Kenya baada ya mwaka 2030. Alisema taifa linahitaji kujadili namna ya kujenga uchumi wenye mapato ya juu, thamani kubwa na uwezo wa kukabiliana na misukosuko huku wananchi wengi wakinufaika. Taarifa zinaonyesha kuwa Prof Nyong'o ataongoza timu ya sekta mbalimbali itakayounda ramani mazungumzo hayo yatakayopelekwa hadi ngazi ya mashinani. Mojawapo ya mada zilizojitokeza kwa nguvu katika mkutano huo ni haja ya kulinda mipango ya maendeleo dhidi ya mabadiliko ya kisiasa kila baada ya uchaguzi. "Kenya ni kubwa kuliko uchaguzi wowote. Uchaguzi si suala la uhai au kifo," alisema Rais Ruto. Alionya kuwa viongozi wengi hufikiria uchaguzi ujao badala ya kizazi kijacho, hali ambayo huathiri utekelezaji wa mipango ya muda mrefu. Naibu Rais Prof Kithure Kindiki alisema mojawapo ya changamoto kubwa katika mataifa yanayoendelea ni kuvurugwa kwa sera kila serikali mpya inapoingia madarakani. "Kero kubwa kwa nchi nyingi za Afrika ni kusitishwa kwa sera zilizowekwa na tawala zilizopita," alisema.

read more