T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 18 Nov 2026 06:55:42

Ni kubaya: Chuo Kikuu cha Moi chageukia kilimo cha miwa kujimudu kifedha

CHUO Kikuu cha Moi, ambacho kinakabiliwa na changamoto kubwa kifedha, kimeanzisha kilimo cha miwa kwa kiwango kikubwa kama njia ya kujiongezea mapato na kupunguza kutegemea fedha za serikali. Chuo hicho tayari kimepanda miwa katika ekari 750 na kina mipango ya kuongeza eneo hilo hadi ekari 1,500. Mradi huo unaogharimu Sh105 milioni, unalenga kugeuza ardhi kubwa ya chuo kuwa chanzo cha mapato, kusaidia shughuli za masomo na kutoa ajira kwa wakazi wa maeneo jirani. Naibu Chansela wa Chuo hicho Profesa Kiplagat Kotut, alisema wameamua kutumia rasilimali ya ardhi waliyonayo kujipatia mapato badala ya kutegemea mgao wa serikali pekee. [caption id="attachment_194032" align="alignnone" width="2000"] Chuo Kikuu cha Moi. Picha|Maktaba[/caption] "Lengo letu kuu ni kuhakikisha chuo kinaendesha shughuli zake bila matatizo. Ili kufanikisha hilo, ni lazima tujipatie fedha za kutosha kupitia miradi yetu," alisema Profesa Kotut. Alisema chuo kina takriban ekari 3,000 na kinapanga kutumia karibu nusu yake kulima miwa ili kukabiliana na changamoto za kifedha, huku kikisaidia pia masomo ya kilimo na uhandisi. Akizungumza Jumanne alipokagua maendeleo ya shamba hilo, alisema mradi huo ulianzishwa baada ya mashauriano na kampuni za kusaga miwa, wadau wa kilimo na wakazi wa eneo hilo. Chuo hicho kinashirikiana na West Kenya Sugar Company, ambayo inatoa utaalamu na ushauri kuhusu utunzaji wa mimea. Kampuni hiyo pia itanunua miwa itakapokomaa na kuisaga. Meneja wa shamba, Bw Tobias Okeno, alisema gharama ya kuandaa na kupanda ekari moja inakadiriwa kuwa Sh70,000, ingawa inaweza kubadilika kutokana na hali ya hewa na mazingira ya shamba. Alisema aina nane za miwa zinazokomaa kwa nyakati tofauti zimepandwa katika ekari hizo 750, ili kubaini zile zinazofaa zaidi eneo hilo. "Tunatarajia kuvuna shamba lote kufikia Juni mwaka ujao. Tunafanya utafiti kubaini aina ya miwa inayofanya vizuri zaidi katika eneo hili," alisema Bw Okeno. Chuo kinakadiria kupata wastani wa tani 40 za miwa kwa ekari. Kwa bei ya sasa ya Sh5,500 kwa tani, mavuno hayo yanaweza kuleta mapato ya takriban Sh220,000 kwa ekari, kabla ya kutoa gharama za uzalishaji na uendeshaji. Mbali na mapato, mradi huo tayari umeanza kutoa nafasi za kazi kwa wakazi na wanafunzi. Profesa Kotut alisema mamia ya wakazi wameajiriwa katika shughuli za kupanda na kupalilia miwa. Wanafunzi pia wamepata nafasi za kufanya kazi shambani na kulipwa, hata wakati wa mgomo wa wahadhiri. Alisema mradi huo unalenga kujenga uhusiano mzuri kati ya chuo na jamii inayokizunguka kwa kutoa fursa za kiuchumi. Chuo pia kinapanga kupanua kilimo biashara kwa kuanzisha mashamba ya kahawa na chai, pamoja na miradi ya tufaha na parachichi. Mradi wa tufaha ulianzishwa Mei 2021 katika eneo la karibu ekari 100. Chuo kinaendelea kufanya utafiti kuhusu aina mbalimbali, zikiwemo MUA52, ambayo Profesa Kotut alisema inakuzwa na taasisi hiyo. Uvunaji mwingine wa tufaha unatarajiwa kufanyika Februari mwaka ujao, ingawa mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri ratiba ya mavuno. Kwa upande wa parachichi, chuo kinashirikiana na Safaricom. Kulingana na Okeno, miche ya kwanza ilipandwa Novemba mwaka jana na mingine Machi mwaka huu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 18 Nov 2026 05:55:40

Mzozo waanika maelezo ya ndani kuhusu nyumba za Buxton

MZOZO kati ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa na kampuni ya GulfCap Real Estate kuhusu mradi wa nyumba za bei nafuu wa Buxton Point umefichua maelezo ya ndani kuhusu makubaliano ya kimkataba kati ya pande hizo mbili. Imebainika kuwa, pande hizo mbili zilikubaliana kaunti iwe na haki ya kupata asilimia 10 ya nyumba za makazi na maeneo ya biashara katika mradi huo, ambayo ni sawa na karibu nyumba 180 kati ya jumla ya 1,800 zilizopangwa kujengwa. Wiki iliyopita, Kaunti ilitangaza kusimamisha shughuli za ujenzi ikilalamikia ukiukaji wa mkataba, hatua iliyofanya mkandarasi kwenda mahakamani kupinga hatua hiyo. Hata hivyo, Novemba 12, Mahakama ya Mazingira na Ardhi Jijini Mombasa, ilikataa kutangaza kuwa ombi lililowasilishwa na kampuni ya Buxton Point Apartments Limited lilikuwa la dharura, na ikaahirisha uamuzi kuhusu ombi la kusimamisha utekelezaji wa notisi hiyo hadi baada ya kusikiliza pande zote. Buxton Point Apartments Limited ni kampuni tofauti iliyoanzishwa na GulfCap kwa madhumuni maalumu ya kutekeleza mradi wa ukarabati na ujenzi upya wa makazi ya Buxton. Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha kuwa, kampuni hiyo ndiyo inatekeleza ujenzi kwa ardhi yenye nambari ya usajili Mombasa Block XVII/1821, iliyokuwa ikijulikana awali kama Mombasa Block XVII/1776, chini ya makubaliano kati yake na Kaunti yaliyotiwa sahihi Januari 15, 2020. Chini ya makubaliano hayo, mkandarasi alipewa jukumu la kutekeleza na kukamilisha mradi huo, huku kaunti ikitakiwa kutoa hatimiliki iliyounganishwa na isiyo na madeni au vikwazo vya kisheria, pamoja na vibali na idhini zinazohitajika. Makubaliano hayo pia yalieleza kuwa wapangaji wa zamani wangezingatiwa katika ugawaji wa nyumba za makazi kupitia mpango wa kununua nyumba kwa awamu, kwa masharti nafuu. Hata hivyo, mjenzi anasisitiza kuwa, mpango huo ulikusudiwa kutekelezwa katika awamu ya tatu, ilhali mradi kwa sasa uko katika awamu ya pili. Aidha, makubaliano hayo yalitaka kampuni hiyo kujenga huduma za kijamii zikiwemo kituo cha shughuli za kijamii, hospitali na shule ya chekechea (ECDE), ambazo zingekabidhiwa mwishoni mwa awamu ya tatu. Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani, msimamizi wa eneo la ujenzi, Bw Aboud Said Khalifa, alisema kuwa kampuni hiyo tayari imejenga ECDE, ambayo kwa sasa inatumika kama ofisi ya eneo la ujenzi hadi mradi utakapokamilika na kuanza kutumika kwa madhumuni yake ya kielimu. Nyaraka za mahakamani zinaonyesha kuwa makabiliano ya hivi karibuni yalichochewa na mkutano uliohusisha maafisa wa kaunti na wapangaji wa zamani Novemba 10, baada ya mwaliko wa mkutano wa mashauriano kutolewa Oktoba 30. Kwa mujibu wa Bw Khalifa, mkutano huo uligeuka kuwa wa hadhara ambapo afisa wa kaunti anayesimamia idara husika alidai kuwa kituo cha jamii na ECDE vikabidhiwe mara moja, licha ya ratiba iliyokubaliwa katika mkataba. Mjenzi huyo anadai kuwa, afisa huyo pia aliwachochea wapangaji wa zamani dhidi ya kampuni hiyo kabla ya Kaunti kutoa notisi ya utekelezaji muda mfupi baada ya mkutano huo. Notisi hiyo iliishutumu kampuni hiyo kwa kuendeleza ujenzi bila vibali vinavyohitajika kutoka kwa kaunti na kukiuka mipango ya majengo iliyoidhinishwa. Pia ilitaja migogoro kati ya msanidi, wapangaji wa zamani na serikali ya kaunti. Hata hivyo, kampuni hiyo inasema notisi hiyo haikubainisha kazi mahususi za ujenzi zilizodaiwa kufanywa bila idhini, masharti ya ujenzi yaliyokiukwa au msingi wa kitaalamu uliotumiwa kutoa hatua hiyo ya utekelezaji. Mjenzi pia anasisitiza kuwa alikuwa amepata kibali cha ujenzi na mipango ya majengo iliyoidhinishwa kabla ya kuanza kazi, na alikuwa akiendelea kuwasiliana na maafisa wa kaunti kuhusu hali ya vibali vyake. Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha kuwa kampuni hiyo iliwasilisha ombi la kufanya upya au kurekebisha vibali vyake kupitia mfumo wa kielektroniki wa mipango ya kaunti Februari 2024, chini ya nambari ya kumbukumbu AAA8456. Katika mkutano wa ufuatiliaji uliofanyika Septemba 25, 2026, Mkurugenzi wa Mipango ya Ujenzi wa Kaunti alirudisha ombi hilo kwa msanifu wa mradi ili kuwasilisha nyaraka zaidi. Kesi hiyo itatajwa Januari 20, 2027, kuthibitisha iwapo maagizo ya korti yametekelezwa.

read more