T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 18 Sep 2026 06:55:18

DPP akataa mpelelezi wa Uingereza kutoa ushahidi katika kesi ya ulanguzi mihadarati

KIONGOZI wa Mashtaka ya Umma ameaomba mpelelezi wa zamani wa kitengo cha polisi cha Uingereza (Scotland Yard) azuiliwe kutoa ushahidi katika kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya methamphetamine yenye thamani ya Sh8.2 bilioni iliyowakabili raia sita wa Iran. Upande wa mashtaka ulisema mpelelezi huyo wa zamani, Bw Kevin Hurley, hakuhusika katika kukamatwa kwa dawa hizo wala uchunguzi wa kesi hiyo, hivyo hakuwa na msingi wa kutoa ushahidi kuhusu masuala yaliyohusiana na kesi hiyo. Bw Hurley alikuwa miongoni mwa mashahidi ambao washtakiwa hao walikuwa wamepanga kuwaita ili kupinga ushahidi wa upande wa mashtaka. Ushahidi wake ulitarajiwa kuangazia namna dawa hizo za kulevya zilizodaiwa kukamatwa katika Bahari Hindi zilivyopaswa kukusanywa, kuhifadhiwa, kutambuliwa, kuhamishwa, kupimwa, kuchunguzwa katika maabara na hatimaye kuwasilishwa mahakamani. Ushahidi wake pia ulilenga kuchunguza iwapo dawa hizo zilishughulikiwa ipasavyo tangu zilipokamatwa baharini, zilipokabidhiwa kwa mamlaka za Kenya, zilipohifadhiwa, kupimwa uzito, kuchukuliwa sampuli na hatimaye kuwasilishwa mahakamani. Upande wa mashtaka ulipinga vikali ushahidi wake, ukisema Bw Hurley hakuwa akiwasilishwa kama shahidi mtaalamu na akauliza msingi wake kutoa ushahidi kuhusu masuala yaliyohusiana na kesi hiyo. Hata hivyo, washtakiwa, kupitia kwa wakili wao, walipinga hoja hiyo wakisema upande wa mashtaka haukutoa sababu za msingi kisheria kumzuia Bw Hurley kutoa ushahidi kabla ya mahakama kumsikiliza. Wakili wa washtakiwa alisema Bw Hurley hatatoa ufasiri wa sheria za Kenya wala kusimulia kilichotokea wakati wa kukamatwa kwa dawa hizo. "Atatoa maoni yake ya kitaalamu kuhusu iwapo taratibu zilizotumika kushughulikia dawa hizo zinazodaiwa kuwa za kulevya zilifuata viwango vinavyotambulika vya utunzaji, uhifadhi na uwasilishaji wa ushahidi," akaeleza. Mahakama itaamua wiki ijayo kama Bw Hurley atakubaliwa kutoa ushahidi wake au la. Jaseem Darzadeh Nia, Nadeem Jadgal, Hassan Baloch, Raheem Baksh, Imran Baloch na Imtiyaz Daryay wanakabiliwa na shtaka la kuhusika katika ulanguzi wa kilo 1,036.044 za methamphetamine zenye thamani ya takriban Sh8.2 bilioni. Wiki iliyopita, Mahakama ya Shanzu iliamua kuwa watu hao wana kesi ya kujibu baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi unaowataka washtakiwa hao kujitetea. Mahakama ilisema ushahidi huo ulihusisha operesheni iliyofanyika katika bahari kuu na ulihusisha meli iliyodaiwa kubeba zaidi ya tani moja ya methamphetamine. Upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa mashahidi 12, wakiwemo wanajeshi wa Jeshi la Wanamaji waliohusika katika kukamatwa kwa dawa hizo, wataalamu kutoka Maabara ya Serikali na nyaraka mbalimbali za ushahidi. Washtakiwa hao walikiri kosa walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, lakini baadaye walikanusha shtaka hilo. Walidai kupitia mkalimani kuwa dawa hizo zilikuwa na uzito wa takriban kilo 800, wakisema wachunguzi walihesabu pia uzito wa vifungashio. Pia walidai kuwa methamphetamine ilikuwa halali nchini mwao na haikukusudiwa kutumiwa vibaya. Washtakiwa hao wamekuwa kizuizini tangu walipokamatwa mwaka jana baada ya kunyimwa dhamana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 18 Sep 2026 05:55:21

Ruto amponda tena Uhuru akimlaumu kuvunja makubaliano ya 'Yangu kumi na Yako kumi'

RAIS William Ruto amemshambulia tena mtangulizi wake, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akimlaumu kwa kusaliti makubaliano ya kisiasa waliyofikia walipokuwa washirika na sasa kufadhili siasa za upinzani dhidi ya serikali yake. Dkt Ruto alisema yeye na Bw Kenyatta walikubaliana kuwa Rais huyo wa zamani angeongoza kwa miaka 10 kabla ya kumkabidhi yeye uongozi wa nchi kwa miaka mingine 10. Hata hivyo, alidai Bw Kenyatta alipuuza makubaliano hayo ulipofika wakati wake wa kugombea urais na badala yake akamuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022. "Hukutimiza. Badala yake, ulifanya kazi dhidi yangu," Rais alisema alipokuwa akizungumza Sindo. Dkt Ruto alisema alimuunga mkono Bw Kenyatta katika chaguzi nne na kusimama naye alipohitaji msaada wa kisiasa. "Nilikuunga mkono katika chaguzi nne na nikakulinda. Ulipofika wakati wako wa kunisaidia, hukufanya hivyo hata kwa siku moja. Lakini baadaye Mungu alinisaidia kuwa Rais wa watu wa Kenya," alisema. Hata hivyo, Rais alisema hamlaumu Bw Kenyatta kwa kutomuunga mkono, akisema ilikuwa haki yake ya kidemokrasia kumuunga mkono mgombea aliyemtaka. Lakini alimshutumu kwa kuhujumu serikali ya Kenya Kwanza na kufadhili siasa za upinzani. "Unashusha hadhi ya afisi ya Rais mstaafu. Unashusha hadhi yako mwenyewe kama mtu," alisema. Kauli hizo zilitolewa muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kuunga mkono sheria inayowazuia marais wastaafu kushikilia nyadhifa za uongozi katika vyama vya kisiasa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka madarakani. Hata hivyo, mahakama haikuwazuia kuwa wanachama wa vyama au kushiriki shughuli za kisiasa. Bw Kenyatta ametangaza ataacha uongozi wa Jubilee kufuatia uamuzi huo. Dkt Ruto pia alikosoa rekodi ya kiuchumi ya serikali iliyotangulia, akidai serikali yake ilirithi uchumi uliokuwa katika hali mbaya. "Tumelipa sehemu kubwa ya madeni na kupunguza mfumuko wa bei. Pia tumeongeza mara mbili akiba yetu ya fedha za kigeni," alisema. Alidai pia serikali yake imeajiri walimu 100,000, kujenga madarasa 23,000 na kufanya mabadiliko katika sekta ya afya. Kauli za Rais zilijiri akimaliza ziara ya siku tano Nyanza, ambapo alitembelea Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori, akizindua miradi na kutangaza mipango mingine ya thamani ya mabilioni ya pesa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 18 Sep 2026 04:55:57

Kenya Kwanza yazidisha presha kwa Natembeya

MUUNGANO wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto, umeanzisha kampeni kali ya kisiasa ya kuteka Kaunti ya Trans Nzoia kutoka kwa upinzani, hatua inayoongeza presha kwa Gavana George Natembeya huku makundi hasimu yakipambana kudhibiti kaunti hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula na msaidizi wa karibu wa Rais, Farouk Kibet, wamefika Kaunti hiyo kueneza ujumbe wa mafanikio ya serikali na wakati huohuo kuunga mkono wanaotajwa kuwa wapinzani wa gavana huyo. Tofauti na mwaka 2022 aliposhinda kwa kishindo, Bw Natembeya sasa anakabiliwa na mazingira mapya ya kisiasa. Gavana huyo wa chama cha DAP-K ametofautiana na kiongozi wa chama hicho, Eugene Wamalwa, na ameashiria kuondoka kwake. Tangu wakati huo amekuwa karibu na mrengo wa upinzani wa Linda Mwananchi unaohusishwa na Seneta wa Nairobi, Bw Edwin Sifuna. "Ninatafuta muhula wa pili kwa sababu bado nataka kukamilisha nilichoanzisha kubadilisha kaunti hii," amesema mara kadhaa kwenye majukwaa yake ya kisiasa. Mabadiliko hayo ya kisiasa yametoa nafasi kwa Kenya Kwanza kuimarisha ushawishi wake Magharibi mwa Kenya na kutafuta mgombea mwenye uwezo wa kumpa changamoto gavana huyo. Wiki iliyopita, Mabw Wetang'ula na Kibet walizuru kaunti hiyo katika shughuli za kuwawezesha wanawake na waendesha bodaboda. Shughuli hizo ziliashiria ujumbe mmoja wa kisiasa: Kenya Kwanza inataka kuteka Trans Nzoia mwaka 2027. Katika mikutano hiyo, Bw Wetang'ula alimtangaza Balozi wa Kenya katika UN-Habitat, Bi Susan Nakhumicha, kama mgombea anayefaa kumpinga Bw Natembeya, huku Bw Kibet akimuunga mkono Mbunge wa Kiminini, Bw Maurice Kakai Bisau. Kuibuka kwa Bi Nakhumicha kumepatia siasa za ugavana sura mpya. Mnamo Juni 2026, Bw Wetang'ula alimuidhinisha waziwazi kuwania ugavana na kuwataka wanasiasa wengine wa Kenya Kwanza kumuunga mkono. "Nimewasiliana na wakazi wa wadi zote 25 na wengi wanatamani mabadiliko. Wanahisi wamevunjwa moyo na uongozi wa sasa na ninafahamu jinsi ya kuokoa kaunti hii nikichaguliwa gavana," amesema Bi Nakhumicha. Hata hivyo, chama cha UDA kinakabiliwa na changamoto ya ndani kwa kuwa viongozi kadhaa wanawania tiketi hiyo. Mbali na Bi Nakhumicha, wanaowania ni Bw Maurice Bisau, aliyekuwa Mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa, na Bw Isaac Kogo. "Gavana wa sasa ameshindwa kuleta maendeleo. Amejikita zaidi katika kujenga taswira yake ya kisiasa badala ya kutimiza wajibu wake," amesema Bw Bisau. Kwa upande wake, Dkt Wamalwa amesema: "Kaunti yetu imebaki nyuma kimaendeleo kutokana na uongozi mbovu. Rekodi yangu ya maendeleo tangu nikiwa Mbunge wa Kiminini inajieleza yenyewe." Wakati huo huo, maendeleo yameibuka kuwa silaha kuu ya kisiasa. Viongozi wa Kenya Kwanza wanajivunia mradi wa nyumba za bei nafuu wa Sh15 bilioni, zaidi ya kilomita 300 za barabara za lami, masoko ya kisasa na mipango ya kuboresha Hospitali ya Kaunti ya Kitale kwa Sh1 bilioni. "Tunahakikisha hakuna eneo linaloachwa nyuma kimaendeleo, na hatutaacha kaunti hii isimamiwe vibaya," alisema Bw Wetang'ula mjini Endebess. Ikiwa na wapiga kura karibu 400,000 waliosajiliwa, Trans Nzoia imekuwa muhimu kwa pande zote mbili. Kwa Rais Ruto, kushinda katika kaunti hiyo kutaimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena. Kwa Bw Natembeya, kushinda muhula wa pili kutathibitisha kuwa ushawishi wake wa kisiasa umeendelea licha ya kutengana na DAP-K.

read more