T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 17 Nov 2026 04:55:51

Gachagua atangaza mapambano makali ya DCP ugavana wa Nairobi

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza kampeni kali za kuhakikisha chama chake cha DCP kinatwaa kiti cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Gachagua amesema DCP itatoa mgombeaji atakayefanikisha mageuzi na kurekebisha changamoto zinazokabili jiji kuu, huku akipuuza uwajibikaji wa Gavana wa sasa Johnson Sakaja na utendakazi wa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri. Kufikia sasa, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya ndiye mwanasiasa pekee ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti hicho kupitia tiketi ya DCP. Bw Gakuya, ambaye yuko katika muhula wake wa tatu bungeni, ni mshirika wa karibu wa Bw Gachagua, ingawa kiongozi huyo hajatangaza hadharani kama anamuunga kwa ugavana. "Gavana atakayeirekebisha Nairobi atatoka DCP na nilimwambia Sakaja kwamba alikuwa akitumiwa kunipiga vita na kwamba hatimaye angetumiwa kisha kutupwa. Hata aliapa kiapo cha kisheria kuunga kuondolewa kwangu mamlakani lakini baadaye akajiondoa. Sasa ametupwa na Karauri kuletwa," akasema Bw Gachagua, akionekana kumrejelea Rais William Ruto kama aliyemtumia gavana huyo. "Ndani ya ODM, (Rais William Ruto) anamuunga mkono Aladwa. Sasa Sakaja hana pa kuenda. Agosti mwaka ujao, wafuasi wangu watakuja kumwondoa madarakani. Kwa kuwa sasa umeachwa, basi umeisha," akaongeza. Bw Gachagua alikuwa akizungumza wakati wa kufungua rasmi ofisi za DCP jijini Nairobi. Mnamo Disemba mwaka jana, Bw Gachagua alitangaza mpango wa kugawana maeneo ya kisiasa kati ya DCP na chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka. Chini ya mpango huo, DCP ingetoa wagombeaji wa ugavana, useneta na mwakilishi wa kike, huku viti 17 vya ubunge na 85 vya uwakilishi katika Bunge la Kaunti vikigawanywa kati ya vyama hivyo viwili. Mpango huo ulilenga kuhakikisha vyama hivyo vinapata viti vingi jijini. Matamshi ya hivi punde ya Bw Gachagua yanaashiria ushindani mkali unaotarajiwa katika kinyang'anyiro cha ugavana, huku wanasiasa wenye ushawishi wakijiandaa kuwania wadhifa huo muhimu. Mbali na Bw Sakaja, Bw Gakuya na Bw Karauri, wengine wanaonyemelea ugavana ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Makadara George Aladwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku. Ushindani huo umechangiwa zaidi na mabadiliko ya hivi karibuni ya miungano ya kisiasa. Bw Sakaja alihama hivi majuzi kutoka UDA na kujiunga na ODM. Naye Bw Karauri, aliyechaguliwa kama mgombeaji huru, alipokelewa katika UDA na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wah pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan Omar. Kwa upande wake, Bw Owino ametangaza kuwa atawania ugavana kupitia tiketi ya chama cha Mwananchi, ambacho pia kinapanga kusimamisha wagombeaji wa viti vya uwakilishi katika Bunge la Kaunti. Uamuzi huo unamweka nje ya vyama na miungano minne inayozidi kuathiri siasa za Nairobi, ambavyo ni ODM, Linda Mwananchi, UDA na DCP. Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki pia amejikuta katika mzozo na baadhi ya viongozi wa jamii yake ya Waluo kuhusu azma yake ya kuwania ugavana. Katika mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha redio nchini, Bw Owino alilalamika kuwa baadhi ya watu kutoka jamii yake wanapinga azma yake licha ya kile alichokitaja kuwa uaminifu na kujitolea kwake kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 17 Nov 2026 03:55:28

Kinyang'anyiro cha mabilionea? Tathmini yaonyesha unahitaji karibu Sh20bn kampeni ya urais

WAGOMBEAJI wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027 wanakabiliwa na gharama kubwa za kuendesha kampeni za kitaifa, huku makadirio yakionyesha kuwa shughuli hizo zinaweza kugharimu kati ya Sh10 bilioni na Sh20 bilioni. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeweka kiwango cha juu cha matumizi ya kampeni za urais kuwa Sh6.1 bilioni. Hata hivyo, kiwango hicho kinahusu kipindi rasmi cha kampeni cha miezi miwili, ilhali wagombeaji wengi wameanza kujitangaza na kutafuta uungwaji mkono mapema. Prof Karuti Kanyinga, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, anakadiria kuwa kampeni madhubuti za urais zinaweza kugharimu Sh14 bilioni. Wagombeaji wanahitaji kufikia wapigakura katika kaunti zote 47 na maeneobunge 290 ya uchaguzi. Haja ya kujenga mitandao ya kimataifa na kutafuta michango imewafanya baadhi ya viongozi wa upinzani kuelekea Amerika, ambako kuna idadi kubwa ya Wakenya wanaoishi ughaibuni. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alirejea nchini Oktoba 20 baada ya ziara ya siku 50 nchini Amerika, ambako alikutana na Wakenya na kuendesha shughuli za kuchangisha fedha. Kiongozi wa Linda Mwananchi, Edwin Sifuna anapanga ziara ya wiki mbili kuanzia Novemba 20, huku Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akiahirisha ziara yake nchini Amerika hadi Februari 2027. Viongozi wengine, akiwemo Dkt Fred Matiang'i na Jimmy Wanjigi, wameajiri kampuni za Amerika kupiga jeki kampeni zao na kuimarisha mitandao ya kimataifa. Amerika ni mahali muhimu kwa sababu ya idadi ya Wakenya wanaoishi huko. Benki Kuu ya Kenya ilikadiria kuwa fedha zilizotumwa nchini kutoka ughaibuni zilifikia Sh650 bilioni mnamo 2023. Msomi Prof Macharia Munene naye anasema wagombeaji wanahitaji kujenga uhusiano na wafadhili wakubwa ili kufanikisha kampeni zao. "Si lazima mtu awe bilionea, lakini anahitaji kuwa na uwezo wa kupata mabilioni. Hii inamaanisha kuwa na mitandao. Pia inasaidia kuwa na kiasi fulani cha pesa zako mwenyewe," akasema. "Unahitaji kuwashawishi matajiri wakuamini ili waweke pesa katika kampeni zako. Lazima kuwe na mchanganyiko wa mvuto wa kisiasa na uwezo wa kupata rasilimali," akaongeza. Aliyekuwa Waziri Moses Kuria, ambaye alishiriki katika kampeni za Rais William Ruto mnamo 2022 na za Rais mstaafu Uhuru Kenyatta 2013 na 2017, alisema kampeni za urais ni shughuli ghali ambazo maandalizi yake huanza miaka kadhaa kabla ya uchaguzi. "Lazima uwe mgombeaji mwenye nafasi ya kushinda. Watu wanahitaji kukuona kama mmoja wa wanaoongoza kabla ya kuwekeza pesa zao, na pia kutaka kujua kama unaweza kutekeleza ajenda zao," akasema BwKuria. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, aliyeshiriki katika kampeni za urais za 2017 na 2022, alisema uchapishaji wa fulana, kofia, mabango na vifaa vingine vya matangazo unaweza kugharimu Sh500 milioni. Pia alisema maandalizi ya mawakala wa uchaguzi ni sehemu nyingine kubwa ya matumizi. Kenya inatarajiwa kuwa na vituo 55,393 vya kupigia kura 2027. Mgombeaji atakayeteua mawakala wawili katika kila kituo na kuwalipa Sh2,000 kila mmoja atahitaji angalau Sh221 milioni. "Kuandaa mkutano wa kampeni huenda kusiwe ghali sana kwa sababu hulipi watu kuhudhuria, lakini unaweza kutumia Sh2 milioni kwa maandalizi kama jukwaa, mfumo wa sauti na viti," akasema Bw Sakaja. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema wagombeaji wanapaswa kuwa na rasilimali zao ili kuepuka kutegemea wafadhili kupita kiasi. "Ikiwa huna pesa zako za kuendesha mipango yako, utakwama. Lazima uwe na fedha zako mwenyewe," akasemaBw Kioni aliongeza kuwa wafanyabiashara wengi hupendelea kuwekeza kwa wagombeaji wanaoonekana kuwa na nafasi ya kushinda. Hata hivyo, Bw Kuria alisema ufadhili wa wagombeaji wa upinzani umekuwa mgumu kutokana na uchunguzi wa serikali.

read more