T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 23:55:17

Tangazo la Sifuna kuwa atwania urais latikisa ODM na Upinzani

TANGAZO la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa atawania urais mnamo 2027 linaendelea kubadili mwelekeo wa siasa za upinzani na ODM, huku viongozi wengi wakianza kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi anaouongoza. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa Kaunti ya Taita Taveta mwishoni mwa wiki, Bw Sifuna alisema licha ya kupokonywa nyadhifa za ukatibu mkuu wa ODM na kiranja wa wachache, anaamini vijana watampa nafasi ya kuwa rais 2027. "Wameninyang'anya kila cheo nilichopewa na Baba, lakini vijana wanasema watanipa cheo cha H.E," akasema. Miongoni mwa viongozi ambao wamebadili msimamo ni Seneta wa Kisii Richard Onyonka, ambaye awali alikuwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i. Bw Onyonka ameonekana mara kadhaa katika mikutano ya Linda Mwananchi na hadharani ameahidi kumuunga mkono Bw Sifuna ikiwa atawania urais. "Mdogo wangu na rais ajaye ni Edwin Sifuna. Ukifika wakati wa kupiga kura nitampigia kura. Nawaona wengine wanatetereka nikisema hivyo lakini sote katika upinzani tuko pamoja," akasema akiwa Voi. Bw Onyonka alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Matiang'i alipozindua azma yake ya urais mnamo 2025. Hata hivyo, hakuhudhuria ziara ya Dkt Matiang'i huko Keumbu, ambako wafuasi wa Linda Mwananchi walivamiwa. Viongozi wengine wa Gusii wanaohusishwa na mrengo huo ni wabunge Clive Gisairo, Anthony Kibagendi na Obadiah Barongo. Ndani ya ODM, mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang' walitumia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou kuikosoa serikali, wakisema viongozi wanapaswa kuwasikiza wananchi na kuheshimu maamuzi yao badala ya kutumia vitisho au rushwa. Kauli zao zimezua hisia kwamba wanaegemea upande wa Linda Mwananchi, ingawa hawajatangaza rasmi msimamo wao. Wakati huo huo, Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata alikosolewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumuunga mkono mgombea wa Linda Mwananchi katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Mchanganuzi wa masuala ya siasa Martin Andati anasema hatua hiyo ilionyesha kuwa siasa za eneo la Mlima Kenya zinaendelea kubadilika, huku viongozi wakitafuta miungano mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Shinikizo pia zinaongezeka kwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, huku baadhi ya wabunge wa Ukambani wakihusishwa na shughuli za Linda Mwananchi. Duru hata hivyo zinaashiria kuwa lengo la wabunge hao ni kuhakikisha Mabw Kalonzo na Sifuna wanashirikiana katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa wabunge wa Wiper wanaohusishwa na mrengo huo ni Joshua Kimilu, Patrick Makau na Danson Mwashako. Katika Magharibi mwa Kenya, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anaendelea kushirikiana na Linda Mwananchi na anapanga mikutano ya kisiasa Trans Nzoia na Bungoma. Ni katika mikutano hiyo ambapo Bw Sifuna anatarajiwa kutawazwa kuwa kigogo wa siasa za Magharibi na kupewa baraka za kuwania urais.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 22:55:50

Ruto arejea nyumbani kujitetea, anuia kurejesha ufuasi unaodaiwa kudidimia

RAIS William Ruto anatarajiwa kuzuru eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa wiki ijayo huku kukiwa na malalamishi yanayoongezeka kutoka kwa wakazi wanaodai serikali yake imepuuza eneo hilo licha ya kuwa ngome yake kuu ya kisiasa. Kwa miaka mingi, kaunti za Bomet, Kericho pamoja na sehemu za Narok na Nakuru zimekuwa ngome ya Rais Ruto. Hata hivyo, miaka minne baada ya kuingia mamlakani, baadhi ya wakazi na viongozi wa mashinani wanasema ahadi nyingi za maendeleo hazijatekelezwa, huku miradi mikubwa ikipelekwa katika maeneo yaliyounga mkono upinzani. Malalamishi hayo yalijitokeza wazi baada ya viongozi kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa kumtembelea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, wakidai jamii ya Kipsigis imetengwa kimaendeleo, ajira na uteuzi wa nyadhifa serikalini. Bw Gachagua alitabiri kuwa Rais Ruto angelazimika kuzuru eneo hilo kutuliza hali, jambo ambalo sasa limethibitishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot. Bw Murkomen alisema rais atazindua na kukagua miradi ya barabara, maji na nyumba za gharama nafuu, huku akisisitiza kuwa madai ya kutengwa kwa eneo hilo hayana msingi. "Rais atafika Kusini mwa Bonde la Ufa kuzindua miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, maji na nyumba za gharama nafuu. Sote tujitokeze kumpokea," akasema Bw Murkomen katika Shule ya Upili ya Tenwek. "Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa watu ambao hawaelewi miradi ambayo serikali imetekeleza eneo hili. Serikali imefanya mengi na itaendelea kufanya mengi siku zinazokuja," akaongeza. Bw Cheruiyot pia alisema ziara hiyo itaonyesha miradi iliyofadhiliwa na serikali na kuzima madai kuwa Kusini mwa Bonde la Ufa imepuuzwa. "Wiki chache zijazo, Ras atakuwa hapa kuzindua miradi ya maendeleo na kuzima madai kuwa eneo hili limetengwa," akasema Bw Cheruiyot katika hafla ya umma Bomet. Hata hivyo, wakazi wengi wanasema hali halisi ni tofauti. Wanalalamikia kucheleweshwa kwa miradi muhimu kama Bwawa la Bosto, fidia na makazi ya zaidi ya familia 21,000 zilizoondolewa katika Msitu wa Mau, pamoja na barabara kadhaa ambazo zimekwama kwa miaka licha ya ahadi za serikali. Barabara ambazo zimetajwa ni pamoja na Chebole–Siongiroi–Chebunyo, Silibwet–Kiptagich–Olenguruone na Sotik–Cheplanget–Roret, ambazo wakazi wanasema ziko katika hali mbaya. Pia kuna malalamishi kuhusu kusimama kwa ujenzi wa Uwanja wa Riadha ya Bomet, pamoja na kucheleweshwa kwa upanuzi wa viwanja vya ndege vya Kerenga na Itembe. Mzozo wa ardhi wa Angata Barikoi nao umeongeza hasira za wakazi. Baadhi yao wanadai kuna njama za kuwanyang'anya ardhi waliyoimiliki kwa muda mrefu, huku wakilaumu serikali kwa kutumia polisi badala ya kutafuta suluhu. Mzozo huo ulivuta hisia za kitaifa baada ya watu sita kuuawa wakati wa maandamano. Ukosefu wa ajira pia ni chanzo kingine cha malalamishi. Vijana wanadai nafasi za kazi katika taasisi za serikali sasa zinauzwa ilhali hawana maelfu ya pesa zinazoitishwa. Hivi majuzi watu wanne walifikishwa mahakamani Bomet wakituhumiwa kuuza barua bandia za ajira za Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC). Bw Gachagua ameendelea kutumia hali hiyo kuishutumu serikali, akidai jamii ya Kipsigis imewekwa kando licha ya kumuunga mkono Rais Ruto kwa dhati mnamo 2022. Ziara ya rais katika South Rift inatarajiwa kuwa mtihani muhimu wa kisiasa huku akijaribu kurejesha imani ya ngome yake ya kisiasa.

read more