T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 22:55:50

Ruto arejea nyumbani kujitetea, anuia kurejesha ufuasi unaodaiwa kudidimia

RAIS William Ruto anatarajiwa kuzuru eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa wiki ijayo huku kukiwa na malalamishi yanayoongezeka kutoka kwa wakazi wanaodai serikali yake imepuuza eneo hilo licha ya kuwa ngome yake kuu ya kisiasa. Kwa miaka mingi, kaunti za Bomet, Kericho pamoja na sehemu za Narok na Nakuru zimekuwa ngome ya Rais Ruto. Hata hivyo, miaka minne baada ya kuingia mamlakani, baadhi ya wakazi na viongozi wa mashinani wanasema ahadi nyingi za maendeleo hazijatekelezwa, huku miradi mikubwa ikipelekwa katika maeneo yaliyounga mkono upinzani. Malalamishi hayo yalijitokeza wazi baada ya viongozi kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa kumtembelea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, wakidai jamii ya Kipsigis imetengwa kimaendeleo, ajira na uteuzi wa nyadhifa serikalini. Bw Gachagua alitabiri kuwa Rais Ruto angelazimika kuzuru eneo hilo kutuliza hali, jambo ambalo sasa limethibitishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot. Bw Murkomen alisema rais atazindua na kukagua miradi ya barabara, maji na nyumba za gharama nafuu, huku akisisitiza kuwa madai ya kutengwa kwa eneo hilo hayana msingi. "Rais atafika Kusini mwa Bonde la Ufa kuzindua miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, maji na nyumba za gharama nafuu. Sote tujitokeze kumpokea," akasema Bw Murkomen katika Shule ya Upili ya Tenwek. "Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa watu ambao hawaelewi miradi ambayo serikali imetekeleza eneo hili. Serikali imefanya mengi na itaendelea kufanya mengi siku zinazokuja," akaongeza. Bw Cheruiyot pia alisema ziara hiyo itaonyesha miradi iliyofadhiliwa na serikali na kuzima madai kuwa Kusini mwa Bonde la Ufa imepuuzwa. "Wiki chache zijazo, Ras atakuwa hapa kuzindua miradi ya maendeleo na kuzima madai kuwa eneo hili limetengwa," akasema Bw Cheruiyot katika hafla ya umma Bomet. Hata hivyo, wakazi wengi wanasema hali halisi ni tofauti. Wanalalamikia kucheleweshwa kwa miradi muhimu kama Bwawa la Bosto, fidia na makazi ya zaidi ya familia 21,000 zilizoondolewa katika Msitu wa Mau, pamoja na barabara kadhaa ambazo zimekwama kwa miaka licha ya ahadi za serikali. Barabara ambazo zimetajwa ni pamoja na Chebole–Siongiroi–Chebunyo, Silibwet–Kiptagich–Olenguruone na Sotik–Cheplanget–Roret, ambazo wakazi wanasema ziko katika hali mbaya. Pia kuna malalamishi kuhusu kusimama kwa ujenzi wa Uwanja wa Riadha ya Bomet, pamoja na kucheleweshwa kwa upanuzi wa viwanja vya ndege vya Kerenga na Itembe. Mzozo wa ardhi wa Angata Barikoi nao umeongeza hasira za wakazi. Baadhi yao wanadai kuna njama za kuwanyang'anya ardhi waliyoimiliki kwa muda mrefu, huku wakilaumu serikali kwa kutumia polisi badala ya kutafuta suluhu. Mzozo huo ulivuta hisia za kitaifa baada ya watu sita kuuawa wakati wa maandamano. Ukosefu wa ajira pia ni chanzo kingine cha malalamishi. Vijana wanadai nafasi za kazi katika taasisi za serikali sasa zinauzwa ilhali hawana maelfu ya pesa zinazoitishwa. Hivi majuzi watu wanne walifikishwa mahakamani Bomet wakituhumiwa kuuza barua bandia za ajira za Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC). Bw Gachagua ameendelea kutumia hali hiyo kuishutumu serikali, akidai jamii ya Kipsigis imewekwa kando licha ya kumuunga mkono Rais Ruto kwa dhati mnamo 2022. Ziara ya rais katika South Rift inatarajiwa kuwa mtihani muhimu wa kisiasa huku akijaribu kurejesha imani ya ngome yake ya kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 21:55:13

Wahuni wa wakubwa? Hakuna aliyekamatwa kwa ghasia Ol Kalou licha ya ufichuzi

ZAIDI ya siku nne baada ya ghasia zilizoshuhidiwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou, hakuna mwanasiasa, mfadhili au mmiliki wa magari yanayodaiwa kutumiwa na watu wenye silaha walioficha nyuso zao ambaye amekamatwa au kuhojiwa. Hali hii imezua maswali kuhusu iwapo wanasiasa wanaochochea vurugu wako juu ya sheria licha ya visa vya uhuni kushuhudiwa peupe. Siku ya uchaguzi, Julai 16, maelfu ya wapigakura walikumbana na kundi la wanaume waliovalia barakoa waliokuwa wakizunguka kwa magari ya kifahari, wakifyatua risasi hewani, kurusha vitoza machozi na kuwashambulia wapigakura, wanahabari na hata baadhi ya maafisa wa polisi. Uchunguzi uliofichua yaliyotokea unaonyesha magari hayo yalikuwa na nambari za usajili zinazozua utata. Miongoni mwao ni Toyota Land Cruiser yenye nambari KDL 477Q, ambayo rekodi za Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) zinaonyesha imesajiliwa kwa jina la John Njuguna Wanjiku, jina ambalo ni sawa na la Mbunge wa Kiambaa anayejulikana kama Ka-Wanjiku. Mbunge huyo alikiri kuwa gari lake lilikuwa Ol Kalou lakini akakanusha kuhusika katika vurugu zozote za uchaguzi. Aidha, gari jingine lililotumiwa na watu hao lilikuwa na nambari KDW 600Q, ilhali rekodi za NTSA zinaonyesha nambari hiyo imesajiliwa kwa gari aina ya Toyota Probox linalomilikiwa na kampuni ya Vipingo Industries. Kampuni hiyo ilisema haina Land Cruiser nyeusi, hali inayoashiria matumizi ya nambari bandia. Licha ya ushahidi huo na video zilizosambaa zikionyesha vurugu, polisi walikuwa bado hawajawahoji wamiliki wa magari hayo wala watu waliorekodiwa wakihusishwa na utoaji rushwa na makosa mengine ya uchaguzi. Uchunguzi wa Idara ya Upelelezi nchini (DCI) pia unaonekana kukwama. Kikosi maalumu kutoka makao makuu ya DCI Nairobi kilikuwa bado hakijaanza kazi rasmi huku kikisubiri malalamishi yaandikwe na waathiriwa. Duru kutoka DCI zilisema wachunguzi wanahitaji kwanza kupata taarifa zilizonakiliwa katika vituo vya polisi kabla ya kuwaita walalamishi kutoa ushahidi. Maafisa hao pia wanatarajiwa kuchunguza maandalizi ya kiusalama yaliyowekwa kabla ya uchaguzi huo mdogo. Kabla ya upigaji kura, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alikuwa ametangaza kuwa zaidi ya maafisa 1,000 walikuwa wametumwa Ol Kalou kuimarisha usalama. Wachunguzi wanatarajiwa kukagua taarifa za kijasusi, picha za kamera za CCTV na mienendo ya magari yaliyonaswa kwenye kamera yakizunguka eneo hilo ili kubaini waliohusika. Kampeni za uchaguzi huo mdogo pia ziligubikwa na ghasia huku upinzani na serikali wakirushiana lawama. Mnamo Julai 12, lori la kampeni la mgombea wa DCP lilivamiwa na kuchomwa moto katika eneo la Chokereria na watu waliokuwa na silaha. Mkazi wa Ol Kalou, John Kuria, alisema yeye ni mmoja wa walionusurika katika kisa hicho. "Walikuwa wamejihami kwa bunduki na waliturushia vitoza machozi kabla ya kutushambulia. Tunataka waliohusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani," akasema Bw Kuria. Siku moja kabla ya uchaguzi, gari la Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega pia lilivamiwa, huku polisi wakipata risasi iliyotumika katika eneo la tukio. Wanahabari nao hawakusazwa. Katika kituo cha kupiga kura cha Shule ya Msingi ya AC, watu sita waliokuwa wamevaa barakoa waliwashambulia wanahabari wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kuwaibia vifaa vya kazi. Mpigapicha wa NTV, George Kieru alipokonywa kamera na kupigwa, huku mwandishi Fabiola Akinyi akinyang'anywa simu kwa kutishiwa bunduki. "Walifika kwa magari ya kifahari, wakaanza kutushambulia na kulazimisha George kufuta picha kabla ya kumpora kamera," alisema Mhariri wa NMG Kanda ya Kusini mwa Bonde la Ufa Brygettes Ngana. Bw Kieru alisema alipigwa hadi kujeruhiwa mkono na mgongo, huku Bi Akinyi akieleza kuwa alielekezewa bunduki tumboni kabla ya kuporwa simu yake. Mpiga picha wa gazeti la Star Enos Teche pia alivamiwa na kuibiwa kamera alipokuwa akirekodi ghasia karibu na Shule ya Msingi ya St Joseph's Catholic. Mkurugenzi wa DCI, Amin Mohamed alisema uchunguzi utawalenga waliotekeleza uvamizi na waliopanga, kufadhili na kuchochea vurugu hizo. Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amesema hakuna atakayesazwa iwapo atapatikana na hatia, iwe ni mwanasiasa, afisa wa usalama au mtumishi wa serikali. Hata hivyo, viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wanasiasa wa upinzani wanasema hatua hizo zitakuwa na maana tu ikiwa waliohusika watafikishwa mahakamani. Kiongozi wa DP Justin Muturi alionya kuwa vurugu za Ol Kalou zinaweka msingi hatari kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Licha ya mazingira hayo ya hofu na vitisho, mgombea wa DCP Sammy Kamau alishinda uchaguzi huo kwa kura 35,440, akimshinda mgombea wa UDA Samuel Nyagah, aliyepata kura 5,450. Sasa macho yote yanaelekezwa kwa DCI kuona kama uchunguzi huo utawagusa waliohusika kupanga na kufadhili ghasia hizo au utaishia kwa wavamizi wa kawaida pekee.

read more