T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 14:40:20

Afrika yatakiwa kuwekeza zaidi kwenye ubunifu wa kilimo

AFRIKA inapaswa kuendelea kuwekeza katika ubunifu wa kilimo na kuharakisha matumizi ya teknolojia zilizothibitishwa ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula, kupunguza uagizaji wa vyakula kutoka nje na kujenga mifumo imara ya chakula inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa Harvesting the Future Africa Summit uliofanyika Nairobi mwezi Juni mwaka huu, 2026, ambapo viongozi wa serikali, taasisi za utafiti, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wafadhili walisisitiza umuhimu wa kupeleka teknolojia zilizofanikiwa kwa wakulima wengi badala ya kusalia katika hatua ya utafiti. Mkutano huo uliandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) pamoja na washirika wake wakati ambapo sekta ya kilimo barani Afrika inakabiliwa na ukame wa muda mrefu, gharama za juu za uzalishaji, changamoto za upatikanaji wa mbolea, migogoro na kuyumba kwa uchumi. Mkurugenzi Mkuu wa CIMMYT, Bram Govaerts, alisema lengo ni kuhakikisha ubunifu wa kilimo unachangia usalama wa chakula, ajira na ukuaji wa uchumi. "Teknolojia zilizofanikiwa zinapaswa kuwafikia wakulima wengi na kwa haraka zaidi," akasema. [caption id="attachment_190349" align="aligncenter" width="300"] Mtambo wa kuosha maparachichi kwenye kiwanda. Picha|Sammy Waweru[/caption] Naye Dkt Agnes Kalibata, mwanachama wa Bodi ya CIMMYT, alisema Afrika tayari ina mifano mingi inayoonyesha jinsi sayansi inavyoweza kuongeza uzalishaji wa kilimo, lakini wadau wanahitaji kupewa raslimali za kutosha ili kufanikisha juhudi hizo. "Kinachohitajika zaidi ni raslimali kuonyesha sayansi na teknolojia zinafanya kazi," Agnes akapendekeza. Washiriki wa mkutano huo wa Harvesting the Future Africa Summit walitaja mbegu bora, mbinu za kilimo himilivu kwa tabianchi, teknolojia za kuboresha afya ya udongo, huduma za ushauri wa kidijitali na mifumo bora ya mbegu kuwa miongoni mwa ubunifu unaowasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku wakiongeza mavuno na mapato. Aidha, walieleza kuwa kuimarisha sekta ya kilimo kutasaidia kuzalisha ajira, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa chakula na kukuza uchumi wa nchi za Afrika. Ripoti ya hivi majuzi ya uchambuzi wa mifumo ya chakula inaonyesha Kenya inakabiliwa na upungufu wa mayai bilioni tano, lita bilioni 6.5 hadi 7.5 za maziwa, tani 340,000 za samaki na tani 5,500 za asali kila mwaka. [caption id="attachment_190350" align="aligncenter" width="300"] Avokado kwenye kiwanda. Picha|Sammy Waweru[/caption] Ripoti hiyo iliyofadhiliwa na Financial Sector Deepening Kenya (FSD Kenya) chini ya mradi wa Green Finance for Youth Employment (GFYE) na kutolewa Mei 2026, inadokeza kuwa Kenya hutumia kati ya Sh288 bilioni na Sh500 bilioni kuagiza chakula kutoka nje kila mwaka. CIMMYT inasisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za utafiti, kampuni za mbegu, mashirika ya wakulima na washirika wa maendeleo ni muhimu ili kuhakikisha teknolojia zinazobuniwa zinawafikia wakulima na kuongeza uzalishaji wa chakula barani Afrika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 13:46:00

Teknolojia nafuu ziwafikie wakulima

WABUNIFU wa teknolojia za kilimo na mabadiliko ya tabianchi wamehimizwa kuibuka na bunifu faafu, rahisi kutumia na endelevu zinazokidhi mahitaji ya wakulima wa mashamba madogo. Wakulima wa mashamba madogo wanakadiriwa huzalisha zaidi ya asilimia 75 ya chakula nchini Kenya. Mkurugenzi Mkuu wa KickStart International, Peter Juma, anasema wakulima hawakubali teknolojia kwa sababu ni mpya, bali kwa kuwa zinatatua changamoto halisi, zinapatikana kwa gharama nafuu na huwaletea faida. "Teknolojia hukubalika ikiwa ni nafuu – kifedha, inatatua tatizo halisi na inajilipa yenyewe," alisema. Alisema hayo majuzi wakati wa kongamano la Kenya Editors Guild (KEG) Press Club jijini Nairobi, lililowaleta pamoja wanahabari wa kilimo, wahariri, watafiti, wabunifu, watunga sera, wakulima na wadau wengine kujadili namna ya kujenga kilimo kinachostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi. [caption id="attachment_190344" align="aligncenter" width="300"] Apu ya kuuza chakula na bidhaa za shambani. Picha|Sammy Waweru[/caption] Juma alisema licha ya juhudi za kuhimiza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kilimo, wakulima wengi bado wanahitaji teknolojia rahisi kutumia, kutunza na kumudu. "Teknolojia zinapaswa pia kuzingatia mahitaji ya wanawake kwa kuwa nyepesi na zinazobebeka kwa urahisi," alielezea. Alitaja pampu za maji zinazotumia nishati ya jua na mashine za kilimo kuwa miongoni mwa teknolojia ambazo bado ni ghali kwa wakulima wengi. Kwa mfano, alisema pampu za maji huuzwa kati ya Sh40,000 na Sh200,000, hali inayozifanya zisifikie wakulima wengi wa mashamba madogo. Juma aliwataka wabunifu kuzingatia uwezo wa wakulima kifedha, ili teknolojia wanazobuni ziweze kuwasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Washiriki wa kongamano la Kenya Editors Guild (KEG) Press Club walikubaliana kuwa Kenya haina upungufu wa utafiti, kukosa takwimu za tabianchi wala suluhisho za kilimo. [caption id="attachment_190345" align="aligncenter" width="300"] Maji yaliyopampiwa. Pampu za maji zinazotumia nishati ya jua na mashine za kilimo zinatajwa kuwa miongoni mwa teknolojia ambazo bado ni ghali kwa wakulima wengi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Changamoto kubwa, walitaja ni kuhakikisha maarifa hayo yanageuzwa kuwa hatua zinazotekelezeka na zinazoweza kutumiwa kwa urahisi na wakulima. Mwanachama wa Baraza Kuu la Kenya Editors Guild, Agnes Mwangangi, alisema wanahabari wana jukumu kueleza simulizi za athari na suluhisho za mabadiliko ya tabianchi, kuwawajibisha viongozi na kusaidia wananchi kuelewa masuala hayo. "Vijana, kwa mfano, wanaongoza katika ubunifu wa teknolojia za kilimo na ujuzi wao wa kidijitali unapaswa kutumiwa kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza njaa nchini," Agnes alihimiza.

read more