T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 03:55:54

Ruto alivyokutana na janga linaloendelea la uhuni katika mkutano wake Emurua Dikirr

GHASIA za kisiasa zilitia doa ziara ya Rais William Ruto katika Kaunti ya Narok Jumatano, baada ya watu wasiopungua sita kujeruhiwa kwa mishale huku wengine kadhaa wakipata majeraha katika mapigano kati ya wafuasi wa Mbunge wa Emurua Dikirr, David Keter na mpinzani wake wa kisiasa Bernard Ng'eno. Fujo hizo zilitokea katika kituo cha biashara cha Mamboleo kabla ya hafla ya rais kuanza, hali iliyomlazimu Dkt Ruto kuwakemea viongozi hao hadharani na kuwataka kumaliza tofauti zao za kisiasa mara moja. Wafuasi wa pande hizo mbili walikabiliana kwa kutumia silaha kali ikiwemo mishale. Afisa mmoja wa polisi kutoka Narok, aliyeomba kutotajwa jina alithibitisha tukio hilo na kusema vurugu vilisababishwa mapigano kati ya vikundi vya wafuasi wa viongozi hao wawili kabla ya Rais kuwasili. Kwa mujibu wa afisa huyo, waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya St Clare's Kaplong katika Kaunti jirani ya Bomet, huku mmoja akihamishiwa Hospitali ya South Rift mjini Kericho kwa matibabu maalumu. Mmoja alikuwa na mshale uliopenya karibu na taya na alitarajiwa kufanyiwa upasuaji. Wengine walijeruhiwa miguuni, mkononi, begani na mmoja alinusurika kupoteza jicho baada ya mshale kupenya karibu na paji la uso. Vurugu hizo zilimfanya Rais Ruto kutoa onyo kali dhidi ya siasa za uhasama. Katika mikutano yake mbalimbali, aliwataka viongozi kuacha tofauti zao na kuzingatia maendeleo ya wananchi. "Aina ya tofauti za kisiasa zinazochochea vurugu, majeraha na umwagaji damu hazipaswi kuruhusiwa. Ghasia hizi lazima zikome mara moja," alisema Rais. Aliwataka viongozi kutambua kuwa uchaguzi unapokwisha, wajibu wao ni kuwaunganisha wananchi badala ya kuwagawanya. Rais pia alimhimiza Mbunge Keter kuchukua jukumu la kuwaleta pamoja wakazi wa Emurua Dikirr na kuzima migawanyiko iliyojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa Mei mwaka huu. Wafuasi wa Ng'eno walionekana wakipeperusha vitambaa vya rangi ya samawati wakati wa mikutano ya rais huku wale wa Keter wakionyesha rangi za chama cha UDA, jambo lililoonyesha wazi mgawanyiko uliopo katika eneo hilo. Dkt Ruto pia alimpongeza Ng'eno kwa kubaki ndani ya chama cha UDA licha ya kushindwa katika kura za mchujo na kumhimiza kuendelea kushirikiana na viongozi wengine kwa manufaa ya wananchi. Katika kura za mchujo za UDA zilizofanyika Machi 27, Keter alipata kura 13,749 dhidi ya kura 13,394 za Ng'eno. Baadaye katika uchaguzi mdogo wa Mei 14, Keter alishinda kiti hicho kwa kura 18, 266. Tukio hilo limeibua upya wasiwasi kuhusu ongezeko la makundi ya wahuni wa kisiasa huku taifa likielekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 02:55:01

Linda Mwananchi inaponyoka Sifuna? Msajili asema 'Linda' na 'Mwananchi' yashachukuliwa

MSAJILI wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou, amefichua kuwa vyama viwili vinavyobeba maneno muhimu yanayotumiwa na vuguvugu la Linda Mwananchi Movement tayari vimo katika mchakato wa usajili wa vyama vya kisiasa. Ufichuzi huo unaweza kutatiza juhudi za Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na washirika wake za kubadilisha vuguvugu hilo kuwa chama cha kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Moja ya vyama hivyo ni Liberty National Democratic Alliance Party, kinachojulikana kwa kifupi kama LINDA Party. Chama kingine ni Mwananchi Party. Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), LINDA Party iliwasilisha jina hilo mnamo Novemba 15, 2024. Majina mengine yaliyowasilishwa pamoja na ombi hilo ni Liberty National Democratic Party (LNDP) na Liberty Democratic Alliance (LDA). Tangu wakati huo, chama hicho kimeendelea kupitia mchakato wa usajili. Viongozi wake ni Phenasio Thuku ambaye ni kiongozi wa chama, Karen Majanga anayehudumu kama Katibu Mkuu na Purity Ndanu ambaye ni Mweka Hazina wa Kitaifa. Msajili huyo pia alithibitisha kuwa ombi la kuhifadhi jina la Mwananchi Party liliwasilishwa na Pius Onyango mwezi Julai 2026 na bado linaendelea kufanyiwa tathmini. Bw Lorionokou alisisitiza kuwa chama ambacho jina lake limehifadhiwa hakiwezi kuchukuliwa au kubadilishwa na mtu mwingine bila kufuata taratibu za kisheria. Katika mahojiano maalumu, Bw Lorionokou alisema wazi kuwa Linda Mwananchi Movement si chama cha kisiasa kilichosajiliwa. "Linda Mwananchi Movement haijasajiliwa kama chama cha kisiasa. Ukweli ni kwamba si chama cha kisiasa kwa sasa," alisema. Kuhusu amri ya hivi majuzi ya Jopo la Mahakama la kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), msajili huyo alisema kuwa haijazuia michakato ya usajili ambayo tayari ilikuwa imeanza. Alifafanua kuwa mahakama ilizuia tu ofisi yake kushughulikia maombi mapya yanayohusiana na jina la Linda Mwananchi kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa. "Hukumu hiyo ilizuia msajili kuhusu maombi mapya yanayohusiana na Linda au Mwananchi Movement. Maombi yaliyokuwa tayari katika mfumo yataendelea kushughulikiwa kama kawaida," alisema. Matamshi hayo yanamaanisha kuwa mchakato wa usajili wa LINDA Party na ombi la Mwananchi Party bado unaendelea. Akizungumzia Pius Onyango, aliyewasilisha ombi la Mwananchi Party, Bw Lorionokou alisema ofisi yake haiwezi kuhusisha mtu huyo na mrengo wa kisiasa wa Seneta Sifuna au mwanasiasa mwingine yeyote bila ushahidi rasmi. "Hatuwezi kuhusisha mwombaji na kundi lolote la kisiasa isipokuwa taarifa hizo ziwe sehemu ya maombi yaliyowasilishwa," alisema. Aidha, alikumbusha kuwa vyama vyote vinavyotaka kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 vinapaswa kuwa vimekamilisha usajili wao kufikia Oktoba 15, 2026. Alisema usajili wa chama cha kisiasa si jambo rahisi kama wengi wanavyodhani. Mbali na kuhifadhi jina, waombaji wanapaswa kuwasilisha katiba ya chama, itikadi zake, kuwa na makao makuu na ofisi katika kaunti 24, pamoja na kusajili angalau wanachama 1,000 katika kila mojawapo ya kaunti hizo. Hata hivyo, hakufunga kabisa mlango kwa Linda Mwananchi Movement kufanikisha mchakato huo kabla ya muda uliowekwa, akisema kila kitu kitategemea jinsi watakavyotimiza masharti ya kisheria. Msajili huyo pia alipuuza madai kutoka kwa baadhi ya viongozi wa upinzani kwamba ofisi yake inatatiza usajili wa vyama vinavyoonekana kuunga mkono upinzani. Alisema tangu aingie afisini Oktoba 13, 2025, idadi ya vyama vilivyosajiliwa imeongezeka kutoka 91 hadi 99, jambo ambalo linaonyesha kuwa sheria zinatumika kwa usawa kwa wote.

read more