T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 23:55:36

Korti yawazima Wetang'ula, Kingi kushiriki kampeni za Ruto Tutam

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi wanakabiliwa na kesi ya kikatiba inayoweza kubadili mipaka ya ushiriki wa viongozi wa Bunge katika siasa za uchaguzi. Hii ni baada ya Mahakama Kuu kuwazuia kwa muda kushiriki kampeni za kumrejesha Rais William Ruto mamlakani mwaka wa 2027 kwa kutumia mamlaka ya nyadhifa zao. Mahakama ilitoa amri za muda zinazowazuia wawili hao kutumia mamlaka, hadhi, ushawishi au heshima ya afisi zao za kikatiba kuandaa, kuendesha, kuunga mkono au kuendesha kampeni za kisiasa hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa. Kesi hiyo iliwasilishwa na shirika la kiraia la Vocal Africa, ambalo linasema kushiriki kwa maspika hao katika kampeni za kisiasa kunadhoofisha uhuru wa Bunge na kuvunja mpaka uliowekwa na Katiba kati ya Bunge na Serikali Kuu. Mahakama ilitambua kesi hiyo kuwa ya dharura na kuagiza maspika hao kuwasilisha majibu yao ndani ya siku tatu za kazi. Kesi hiyo itatajwa Julai 16 kwa maelekezo zaidi. Mbali na Wetang'ula na Kingi, walioshtakiwa ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Mwanasheria Mkuu. Katika kesi yake, Vocal Africa inasema Katiba iliunda Bunge kama mhimili huru unaopaswa kusimamia Serikali Kuu, na hivyo viongozi wake hawapaswi kuonekana kama viongozi wa kampeni za kisiasa. "Katiba iliunda Bunge ambalo lingesimama bega kwa bega na Serikali Kuu, si kuwa nyuma yake. Iliwakabidhi maspika wa bunge mamlaka ya kikatiba, si kwa manufaa ya kisiasa ya chama; iliwapa jukumu la kulinda na kuongoza taasisi ya Bunge, si kuendesha kampeni za uchaguzi," zinasema stakabadhi za kesi hiyo. Shirika hilo linadai kuwa kati ya Juni na mapema Julai mwaka huu, Bw Wetang'ula alihudhuria mikutano ya kisiasa Likoni (Mombasa), Emuhaya (Kakamega) na Eldoret (Uasin Gishu), ambako alidaiwa kuhimiza wananchi kumuunga mkono Rais Ruto na ajenda za serikali ya Kenya Kwanza. Naye Bw Kingi anatuhumiwa kushiriki mikutano ya uhamasishaji wa kisiasa Mombasa na maeneo mengine ya Pwani. Kwa mujibu wa walalamishi, hatua hizo zimeibua mgongano kati ya wajibu wa maspika hao wa kuongoza Bunge kwa njia isiyoegemea upande wowote na shughuli zao za kisiasa, jambo ambalo limepunguza imani ya umma kwa uhuru wa Bunge. "Mamlaka ya kikatiba ya Bunge hayawezi kutekelezwa ipasavyo ikiwa maafisa wa kikatiba waliokabidhiwa jukumu la kuongoza mabunge yote mawili watajitokeza hadharani kama viongozi wa kampeni za kisiasa au watetezi wa kuchaguliwa tena kwa Serikali ile ile ambayo Bunge lina wajibu wa kusimamia na kuwajibisha kwa mujibu wa Katiba," walalamishi wanasema. Vocal Africa inasema kwamba haipingi haki ya maspika hao kuwa na misimamo ya kisiasa binafsi, bali inapinga matumizi ya mamlaka na heshima ya afisi zao za kikatiba katika kampeni za uchaguzi. Shirika hilo linaomba mahakama itoe amri ya kudumu ya kuwazuia kutumia nyadhifa zao kwa shughuli za kampeni, itangaze kuwa vitendo hivyo vinakiuka Katiba na misingi ya uongozi bora, uadilifu na imani ya umma, na pia iamuru IEBC pamoja na EACC kuchunguza madai hayo na kuwasilisha ripoti zao mahakamani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 22:55:56

Sababu za uchaguzi wa Ol Kalou kugeuka kufa kupona kati ya Uhuru, Ruto na Gachagua

UCHAGUZI mdogo wa ubunge wa Ol Kalou unaotarajiwa kufanyika Julai 16 umegeuka kutoka kuwa uchaguzi wa kawaida wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na marehemu mbunge David Kiaraho hadi kuwa uwanja muhimu wa kupima nguvu za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Ingawa wananchi wanatarajiwa kumchagua mbunge mpya, wachambuzi wa siasa wanasema uchaguzi huo sasa ni kipimo cha ushawishi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya. Kura hiyo itapima Rais William Ruto na Naibu Rais Kithure Kindiki kwa upande mmoja, huku aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta wakitazamiwa kwa makini upande mwingine. Wadadisi wanasema matokeo yataonyesha ni kiongozi gani bado anaungwa mkono na wakazi wa Mlima Kenya na ni nani ana nafasi nzuri kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka 2027. Ingawa wagombea ni tisa, ushindani mkubwa umejikita kati ya mgombea wa UDA Muchina Nyaga, anayepigiwa debe na Rais Ruto na Profesa Kindiki; Douglas Kamau Ngotho wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua; na Wilson Kigwa wa Jubilee anayehusishwa na Bw Kenyatta pamoja na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i. Kwa Rais Ruto, uchaguzi huu ni mtihani wake mkubwa wa kwanza Mlima Kenya tangu uhusiano kati ya serikali yake na sehemu ya viongozi wa eneo hilo uharibike kufuatia kuondolewa madarakani kwa Bw Gachagua mwaka 2024. Rais alipata karibu asilimia 87 ya kura za Mlima Kenya katika uchaguzi wa 2022, hivyo ushindi wa UDA utakuwa ushahidi kuwa bado ana ushawishi mkubwa eneo hilo. Lakini iwapo UDA itashindwa, wachambuzi wanaamini hali hiyo itaimarisha madai kwamba ngome yake ya kisiasa katika Mlima Kenya inaendelea kuyeyuka na kulazimisha Ikulu kutathmini upya mikakati yake kabla ya uchaguzi mkuu. Mchambuzi wa siasa John Okumu anasema ushindi wa upande wowote utatoa nguvu mpya katika pambano la kuwania uungwaji mkono wa Mlima Kenya. "Endapo mgombea wa Rais atashinda huku Bw Gachagua na Bw Kenyatta wakishindwa, kutakuwa na maswali iwapo kambi hizo mbili za upinzani zinaweza kuendelea kutekeleza mikakati tofauti katika Mlima Kenya," alisema. Hata hivyo, kampeni zimeibua maswali mapya ndani ya serikali. Ingawa Prof Kindiki ndiye anayechukuliwa kuwa msimamizi mkuu wa siasa za Mlima Kenya kwa niaba ya Rais, uratibu mkubwa wa kampeni umeonekana kufanywa na Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri. Bw Kiunjuri alipuuzilia mbali madai kuwa serikali iko katika hali ya hofu. "Tulipoanza kampeni mgombea wetu alikuwa na uungwaji mkono wa takriban asilimia tisa. Kila ongezeko la asilimia limetokana na kazi ya timu zetu mashinani. Kwa sasa sisi ndio tunaongoza," alisema. Lakini Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia alihoji kwa nini Bw Kiunjuri ndiye anayeonekana kuongoza kampeni za serikali Ol Kalou. Kwa Prof Kindiki, uchaguzi huu ni mtihani wa kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya Rais Ruto tangu achukue nafasi ya Bw Gachagua. Wachambuzi wanasema matokeo mabaya yatazua maswali kuhusu uwezo wake wa kuimarisha ngome hiyo muhimu kisiasa. Seneta wa Murang'a Joe Nyutu alisema uchaguzi huo ni kipimo muhimu kwa Naibu Rais. "Uchaguzi huu unapima kama Prof Kindiki anaweza kuhamasisha Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto. Mustakabali wake wa kisiasa unategemea uwezo wake wa kuonyesha anaweza kuleta kura kutoka eneo hili," alisema. Hata hivyo, mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire alisema nafasi ya Prof Kindiki serikalini haina tishio lolote. Bw Gachagua anachukulia uchaguzi huo kama mtihani wa kwanza wa nguvu za chama chake cha DCP tangu kuondolewa kwake mamlakani. Ushindi utampa hoja kuwa ndiye kiongozi mkuu wa kisiasa wa Mlima Kenya na unaweza kuwashawishi viongozi zaidi kuhama kutoka UDA kwenda DCP. "Tutashinda kiti hiki. Serikali imeingiwa na hofu na inaweza hata kutaka kuahirisha uchaguzi. Lakini wananchi wa Nyandarua watazungumza kupitia kura," alisema Bw Gachagua. Kwa Bw Kenyatta, ushindi wa mgombea wa Jubilee Wilson Kigwa utakuwa thibitisho kwamba bado ana ushawishi wa kisiasa na kwamba anaweza kuhamisha uungwaji mkono huo kwa Dkt Matiang'i kuelekea uchaguzi wa urais wa 2027.

read more