T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 27 Aug 2026 04:55:45

Gachagua sasa 'ammaliza' Uhuru Mlimani na Nairobi

CHAMA cha DCP kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kinazidi kujitokeza kama tishio kubwa kwa Jubilee, chama cha aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, huku kikivamia ngome zake za kisiasa za Mlima Kenya na Nairobi. Huku Uchaguzi Mkuu wa 2027 ukikaribia, Jubilee imepata pigo jingine, viongozi wake kadhaa waliochaguliwa wakitangaza kuhamia DCP. Mbunge wa Kamukunji Yusuf Hassan ndiye wa hivi punde kuondoka Jubilee, hatua inayoonyesha kuwa ushindani kati ya vyama hivyo haupo katika eneo la Mlima Kenya pekee. Nairobi, wabunge wote watatu waliochaguliwa kwa tiketi ya Jubilee wametangaza kuwa watatetea viti vyao kwa tiketi ya DCP. Hao ni Bw Hassan, Mark Mwenje wa Embakasi Magharibi na Amos Mwago wa Starehe. Mlima Kenya, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, aliyedhaminiwa na Jubilee, pia amehamia DCP. Viongozi wengine wa Jubilee, wakiwemo wabunge walioteuliwa Sabina Chege, Aden Keynan (Eldas), Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi), John Waluke (Sirisia) na Racheal Nyamai (Kitui Kusini), wameegemea Serikali Jumuishi. Kuhama huku kunaweza kudhoofisha uwezo wa Bw Kenyatta kujadiliana kisiasa kuelekea 2027 na kumfanya Bw Gachagua kuwa mhusika mkubwa katika siasa za upinzani. Akizungumzia hatima ya Jubilee, Bw Kega alisema wazi kuwa chama hicho kimekufa kisiasa Mlima Kenya na Nairobi. "Hakuna Jubilee Mlima Kenya na Nairobi. Tatizo linaloikabili Jubilee ni ukosefu wa uongozi. Tulipojaribu kufanya mabadiliko, yalipingwa, na sasa mnaona kinachotokea. Kila mtu anaondoka," akasema Bw Kega. Hata hivyo, Naibu Kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alipuuza kuhama kwa viongozi hao, akisema wengi wao hawakuwa waaminifu kwa chama hicho na walikitumia tu kupata nyadhifa serikalini. "Si hasara mpya kwetu kwa sababu hawajawahi kujitambulisha na Jubilee. Kwa kweli, ni fursa kwetu kutafuta vijana ambao wamejitolea kuwa nguzo wa chama," akasema Bw Kioni. Alidai kuwa DCP inaonekana kujishughulisha zaidi na kupambana na Jubilee kuliko UDA. Bw Gachagua, hata hivyo, alitangaza Jumanne kuwa DCP imechukua usukani wa siasa za Nairobi baada ya Bw Hassan kujiunga na chama hicho. "Ninataka kutangaza leo kwamba DCP imechukua Nairobi," akasema kiongozi huyo wa DCP. Naibu kiongozi wa DCP Cleophas Malala alisema kuhama kwa Bw Hassan ni ushahidi kuwa chama hicho kinageuka kuwa na sura ya kitaifa, huku Katibu Mkuu John Methu akiahidi uteuzi wa haki kwa wagombeaji. "Nimejiunga na DCP kwa sababu ni chama kinachotaka mabadiliko halisi," akasema Bw Hassan. Kwa kuhama huku, vita vya kisiasa kati ya DCP na Jubilee vinaonekana kuingia katika hatua mpya, huku Nairobi na Mlima Kenya zikitarajiwa kuwa maeneo muhimu ya mapambano kuelekea 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 27 Aug 2026 05:55:06

Muhoozi kuwania urais 2031 akisema babake, Rais Museveni, atamuunga mkono

KAMPALA, Uganda: MKUU wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa Rais Yoweri Museveni, ametangaza kuwa atawania urais katika uchaguzi wa mwaka 2031. Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 52, kwa muda mrefu ametajwa kuwa mrithi anayetarajiwa wa baba yake mwenye umri wa miaka 81, ambaye ametawala Uganda kwa miongo minne. Mkuu huyo wa jeshi pia anafahamika kwa jumbe zake zenye utata kwenye mtandao wa kijamii wa X, zikiwemo tishio la kumkata kichwa kiongozi mkuu wa upinzani, Bobi Wine. Katika ujumbe mmoja kati ya mfululizo wa machapisho aliyoweka X Jumanne usiku, Kainerugaba alisema alikuwa tayari kuwania wadhifa wa juu zaidi nchini humo. "Nitawania wadhifa wa juu zaidi nchini mnamo 2031. Na tutashinda kwa neema ya Mwenyezi Mungu," akasema Kainerugaba. Aliongeza kuwa kwa kuungwa mkono na baba yake, ambaye huwa anamrejelea kwa heshima kama "Mzee", ana uhakika wa kupata asilimia 90 ya kura katika uchaguzi huo. Kainerugaba, ambaye anaongoza kundi la wazalendo wa Uganda (PLU), hapo awali alikuwa ametangaza kuwa angewania urais katika uchaguzi uliofanyika Januari mwaka huu, lakini baadaye akajiondoa na kumuunga mkono baba yake. Alikuwa na nafasi muhimu katika kampeni za kuhakikisha Museveni anachaguliwa tena Januari, huku akiamuru hatua kali dhidi ya wapinzani na kuzimwa kwa intaneti, kulingana na ripoti zilizozingira uchaguzi huo tata. Museveni, ambaye anaongoza chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), amekuwa madarakani tangu 1986. Wakosoaji wamekuwa wakiilaumu serikali yake kwa ukiukaji wa haki za binadamu, yakiwemo mateso, utekaji nyara na kuwazuilia watu kiholela, madai ambayo serikali imekanusha. Bobi Wine alikimbilia Amerika mapema mwaka huu, akisema alihofia maisha yake baada ya kupinga ushindi wa Museveni akidai kulikuwa na visa vya udanganyifu. Mwanasiasa mwingine mkongwe wa upinzani, Kizza Besigye, amekuwa gerezani tangu 2024 na anakabiliwa na kesi ya uhaini. Licha ya afya ya Besigye kuendelea kudorora, utawala wa Museveni hauonekani kumakinikia kumwaachilia huru. Haijulikani iwapo Museveni mwenyewe atawania tena urais 2031 baada ya tangazo lake, huku serikali ikisema uamuzi huo utafanywa na rais pamoja na chama chake kwa wakati mwafaka. Mnamo 2031, Museveni atakuwa na umri wa miaka 86 na akiwania, atakuwa kati ya viongozi wakongwe zaidi ambao wamewahi kuwania wadhifa wa urais ulimwenguni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 27 Aug 2026 03:55:00

Ruto, Gachagua wang'ang'ania kura za Maasai huku Ole Lenku naye akikosana na ODM

VITA vya kisiasa vya kusaka kura za jamii ya Maa vinazidi kupamba moto kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wakiongeza juhudi za kutafuta uungwaji mkono katika jamii ya wafugaji. Maa ina ushawishi mkubwa katika kaunti za Kajiado, Narok na Samburu, na pia ina idadi kubwa ya wakazi katika baadhi ya maeneo ya Laikipia. Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinaonyesha kuwa kaunti hizo tatu zinaweza kuwa na zaidi ya wapigakura milioni 1.4 waliosajiliwa kufikia uchaguzi wa 2027. Kwa miaka mingi, siasa za Maa zilidhibitiwa pakubwa na mwanasiasa mkongwe William Ole Ntimama, aliyefariki Septemba 1, 2016. Baada ya kifo chake, eneo hilo lilibaki likimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ambaye alifariki Oktoba mwaka jana na kuacha pengo la kisiasa ambalo viongozi mbalimbali sasa wanajaribu kujaza. Hakuna mwanasiasa kutoka jamii hiyo ambaye ameweza kujaza nafasi iliyowahi kushikiliwa na Bw Odinga na Bw Ntimama. Juhudi za Seneta wa Narok Ledama Ole Kina kujijenga kama kinara wa Maa pia zinaonekana kudidimia, huku ushawishi wa familia ya Ntutu, inayojumuisha Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu na Mbunge wa Narok Kusini Kitilai Ole Ntutu, ukiendelea kupungua. Rais Ruto alitembelea Narok Jumanne na kuwataka wakazi kumpima kwa rekodi yake ya maendeleo. "Wakenya wanataka maendeleo wala si maneno matupu. Narok ni kaunti yenye utajiri wa kilimo na hakuna sababu kwa nini msipate barabara nzuri," akasema Rais. Alizindua ujenzi wa barabara ya Enengetia-Olkurto-Olposimoru yenye urefu wa kilomita 59 na kutaja miradi mingine ya barabara inayoendelea katika kaunti hiyo. Pia alisema Sh2.8 bilioni zitatumika kuunganisha nyumba 15,000 zaidi na umeme. Alisema nyumba 14,000 zimeunganishwa na umeme katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Kwa upande wake, Bw Gachagua ameendelea kuvutia jamii ya Maa kwa usaidizi wa Seneta wa Kajiado Seki Lenku na Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina. Alitembelea Narok Agosti 21, ambako alizuru Emurua Dikirr na kaburi la aliyekuwa mbunge Johana Ng'eno. Mbunge wa Kajiado ya Kati Memusi Kanchory alisema viongozi wanaounga mkono Serikali Jumuishi wanaunga mkono azma ya Rais Ruto ya kuchaguliwa tena 2027. "Hapa tuko kwa mihula miwili na tunafanya kazi katika Serikali Jumuishi, lakini kuna viongozi ambao wameazimia kutugawanya kwa sababu hawafurahishwi na ushirikiano wetu," akasema Bw Kanchory. Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, hata hivyo, amekosana na ODM na ametishia kutafuta chama kingine atakachotumia kuwania useneta wa Kajiado. "Tulipata ODM ikiwa dhaifu na kwa sababu tulimheshimu aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga, tuliimarisha chama hicho Kajiado. Kama vile madiwani wa UDA walivyojiunga na DCP, sisi pia tutaondoka na kujiunga na Linda Mwananchi," akasema Bw Lenku."ODM itafunga shughuli zake katika Kaunti ya Kajiado. Sisi ndio tulileta ODM hapa na kuifanya iheshimike," akaongeza. Kwa upande wake, Bw Gachagua amejitaja kama mtetezi wa maslahi ya Maa, hasa kuhusu suala la ardhi. "Raila Odinga amekuwa akiwatetea tangu zamani. Mungu amemchukua. Nataka mnifanye kuwa mtetezi wenu. Nitatetea na kusimamia maslahi yenu bila woga, hasa kuhusu suala la ardhi," akasema wakati wa ziara yake Kajiado Februari mwaka huu. Katika uchaguzi wa 2022, Raila alishinda Ruto katika kaunti zote tatu. Kajiado alipata kura 158,526 dhidi ya 148,439 za Ruto, Narok alipata 102,279 dhidi ya 92,894, huku Samburu akipata 41,737 dhidi ya 28,319.

read more