T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 24 Aug 2026 07:55:11

Sheria za uchaguzi zakwama bungeni 2027 ikikaribia

BUNGE la Kenya linakabiliwa na kibarua kigumu cha kupitisha kwa haraka sheria muhimu za uchaguzi, huku mapendekezo kadhaa yakikwama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027. Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula alikuwa ameahidi kuharakisha miswada hiyo, lakini mwaka mmoja baadaye hatua kidogo ndiyo imepigwa hali inayozua wasiwasi kuhusu maandalizi ya nchi kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeonya kuwa kutungwa au kubadilishwa kwa sheria za uchaguzi karibu sana na siku ya uchaguzi kunaweza kutatiza pakubwa mipango yake ya utekelezaji na ununuzi wa vifaa na huduma. Mageuzi mengi yanayohitajika yalitokana na mapendekezo ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) na yanahusu marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi, Sheria ya Makosa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Pia kuna Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi na kanuni zake, zinazolenga kuhakikisha wagombeaji na vyama vya kisiasa wanapata nafasi sawa katika mashindano. Miswada hiyo ilichapishwa mnamo 2024, ikapitishwa na Seneti na kuwasilishwa kwa Bunge la Kitaifa. Hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya IEBC kuhusu kuundwa kwa jopo la kuchagua makamishina panapotokea nafasi wazi ndiyo mafanikio makubwa pekee yaliyopatikana hadi sasa. IEBC inasema hali hiyo inakiuka mapendekezo ya Tume Huru ya Uchunguzi wa Uchaguzi (IREC), iliyoongozwa na Jaji mstaafu wa Afrika Kusini Johann Kriegler, kwamba mageuzi ya sheria za uchaguzi yafanywe angalau miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu. "Tabia hii inakinzana na mapendekezo ya Tume ya Kriegler kwamba mageuzi ya kisheria yafanywe angalau miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu," IEBC iliambia bunge. Bw Wetang'ula hakujibu maswali kuhusu hatua iliyopigwa katika kuharakisha miswada hiyo. Hata hivyo, Oktoba 2025 alisema Bunge lilikusudia kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi miwili au mitatu. Miongoni mwa miswada inayosubiri ni Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa 2024, ambao unapendekeza kampuni huru kufanya tathmini ya mchakato wa uchaguzi ndani ya mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu. Mswada mwingine unapendekeza adhabu ya faini ya hadi Sh2 milioni au kifungo cha miaka mitano kwa mtu anayefanya uchaguzi katika kituo ambacho hakijatangazwa rasmi kwenye gazeti la serikali. Pia unalenga maafisa wanaochelewesha bila sababu kutangaza matokeo au kuyabadilisha kimakusudi. Wakati huohuo, Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa unapendekeza kufutwa kwa Kifungu cha 14A, hatua ambayo inaweza kurahisisha wanasiasa kuunga mkono vyama pinzani bila kupoteza moja kwa moja nyadhifa zao za uchaguzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 24 Aug 2026 06:55:40

Wito Gavana Nassir awajibike baada ya mlinzi wake kuhusishwa na ufyatuliaji risasi

WANASIASA sasa wanamtaka Gavana Abdulswamad Nassir awajibike baada ya walinzi wake kuhusishwa na ufyatuliaji wa risasi uliowajeruhi vijana watatu Changamwe. Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Mombasa, Bi Stella Cherono, vijana hao walimshambulia Gavana Nassir alipokuwa katika hafla ya kuhamasisha wakazi kuhusu mradi wa kutoa mikopo kwa makundi Changamwe. Bi Cherono alisema vijana hao walianza kuimba nyimbo za kumkejeli Gavana huyo, wakimtaja kama kiongozi wa "muhula mmoja". Hata hivyo, baadhi ya viongozi wamejitokeza kumshutumu Gavana Nassir kuhusu tukio hilo na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliohusika. Bi Cherono alisema uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo umeanzishwa ili kubaini kilichotokea na waliohusika. Wanasiasa wakiongozwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Bw Hassan Omar, na Seneta mteule Bi Miraj Abdalla, walilaani tukio hilo wakisema wakazi wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu viongozi wao bila kutishiwa. "Kuna uhuru wa kuzungumza kwenye Katiba yetu. Jana nilikerwa sana. Naskia Gavana aliambiwa yeye ni wa muhula mmoja, na hiyo si siri, kila mtu anajua. Lakini akakasirika sana na ile hasira ikadhibitiwa na walinzi wake ambao walifyatua risasi na kujeruhi vijana wetu," alisema Bw Omar. Bw Omar, ambaye anawania ugavana Mombasa, alisema wakazi wa Mombasa wana haki ya kumkosoa Gavana bila kuhofia usalama wao. "Kila mtu hapa Mombasa atasema wewe ni gavana wa muhula mmoja. Tuone kama watapigwa risasi. Haiwezekani tuogope. Haiwezekani ukatuambia sisi tumesimama pamoja, mwingine anajenga na wewe unavunja," alisema. Walimtaka Gavana Nassir kuchukua jukumu kuhusu tukio hilo na kuhakikisha waliohusika wanawajibishwa. "Ukipiga watoto risasi unaharibia hii serikali. Na sisi wengine katika hii serikali hatuko na wewe. Usiwadhulumu wanyonge sababu ya umaskini. Serikali italinda hadhi ya maskini," alisema Bw Omar. Tukio hilo limezua mjadala kuhusu matumizi ya nguvu na uwajibikaji wa maafisa wa usalama wanaolinda viongozi wa umma, huku polisi wakiendelea na uchunguzi. Wiki kadhaa zilizopita, mlinzi wa Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, alinaswa kwenye kamera akifyatua risasi hewani wakati wa mkutano wa kisiasa. Watetezi wa haki za kibinadamu pia wamelaani tukio hilo na kumtaka Gavana Nassir awajibike. Haya yanajiri siku mbili baada ya tukio hilo, huku mmoja wa vijana waliojeruhiwa akinaswa kwenye kanda ya video akiwaomba wanasiasa kukoma kuingiza siasa katika kisa hicho. Kijana huyo, Sammy Owino, 24, alifichua kwamba awali alikuwa akifanya kazi katika serikali ya kaunti lakini baadaye alisimamishwa kazi. Hata hivyo, alisema alipata fursa ya kumwona Gavana Nassir na kumfuata ili kuzungumza naye, lakini vurugu zilizuka na risasi kuanza kufyatuliwa. "Mimi ndiye yule kijana nilipigwa risasi, na mahali imefikia nashukuru Mungu, hasa ndugu zangu ambao wamenishika mkono nikapata matibabu. Naomba hili swala lisiwekwe siasa kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa nafanya kazi kwa kaunti lakini kulikuwa na kutoelewana. Jana tulimfuata Gavana tukitaka kumuongelesha na alikuwa ameshatupokea, mara ghafla risasi zikaanza kupigwa. Risasi imeniingia," alisema kijana huyo. Alisema ameona kwenye mitandao ya kijamii wanasiasa wakitumia suala hilo kama mada ya kisiasa. Kijana huyo alisema Gavana Nassir ndiye kiongozi pekee aliyemtembelea hospitalini baada ya kujeruhiwa. "Usitumie siasa kwa swala langu. Mimi si mhalifu, mimi ni mnyang'anyi? Mimi ni mmbangaizaji, hatuibi watu chochote. Mimi naangalia maisha yangu, mamangu na watoto wangu. Sitaki siasa," alisema. Alisema anataka suala lake lichukuliwe kama tukio la kawaida la raia aliyejeruhiwa na si kama silaha ya kisiasa. Hata hivyo kiongozi wa chama cha Vibrant Democratic Party Bw Awiti Bollo aliitaka idara ya polisi kuwapokonya bunduki walinzi wa Gavana Nassir bunduki kwa kuhusika na ufyatuliaji risasi kiholela na kujeruhi vijana. "Hatutaki kuona vijana wa watu wakiumizwa sababu ya siasa na kusema Bw Nassir hatarudi mamlakani. Bw Nassir badala ya kujeruhi watoto wetu wapatie ajira wasafishe mji ambao umekuwa mchafu sana. Lakini kwenye uchaguzi mkuu wa 2027 utakiona cha mtema kuni, sababu umezoea kutetewa kinara wa ODM Bw Raila Odinga hayuko kupigia debe," alisema.

read more