T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 17 Aug 2026 07:55:16

Mwashako adai alikataa shinikizo, pesa na kuamua kubaki wantam

MBUNGE wa Wundanyi, Danson Mwashako, amefichua kwa mara ya kwanza sababu iliyomfanya kujiuzulu kutoka kwenye vuguvugu la wabunge wa Pwani (CPG), akisema alishinikizwa kukihama chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka na upinzani na kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza. Bw Mwashako, anayelenga kuwania kiti cha ugavana wa Taita Taveta katika uchaguzi mkuu wa 2027 kupitia chama cha Wiper, alisema alipewa sharti la kujiunga na serikali au kujiondoa kwenye uwenyekiti wa CPG. Hata hivyo, Mbunge huyo ambaye anahudumu kwa muhula wa pili alisema aliamua kubaki katika upinzani akisema uaminifu wake kwa Wiper na msimamo wa kisiasa wa wafuasi wake ulikuwa muhimu kuliko nafasi ya uongozi katika kundi la wabunge wa Pwani. "Nilichaguliwa kupitia tiketi ya Wiper mwaka wa 2017 na 2022, nikiwa kwenye chama hiki nahisi niko nyumbani kwangu. Hivi majuzi wamekuwa wakinishawishi kila siku nijiunge na serikali, lakini nimekataa. Hata wamenitishia, lakini nilisimama imara," alifichua kwenye mkutano wa kisiasa huko Kakuyuni. Bw Mwashako alisema shinikizo liliongezeka baada ya baadhi ya viongozi wa Pwani kuanza kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza, huku wengine wakimuuliza kwa nini hakutaka kujiunga nao. Alisema hata aliahidiwa msaada wa kifedha wa kugharamia kampeni zake za ugavana iwapo angehama Wiper na kujiunga na Kenya Kwanza. "Nililikataa hata hizo pesa zao. Nilikuwa mwenyekiti wa CPG kwa miaka mitatu, lakini Januari mwaka huu nikaamua kujiuzulu kwa sababu ya shinikizo. Niliambiwa ili niendelee kuwa mwenyekiti nilazima kuhama Wiper. Nikaamua kujiuzulu," alisema. Nafasi yake ilichukuliwa na mwakilishi wa wanawake wa Kilifi, Getrude Mbeyu. CPG ilianzishwa zaidi ya miongo miwili iliyopita kama jukwaa la viongozi waliochaguliwa kutoka Pwani kushirikiana kutetea maslahi ya eneo hilo, yakiwemo maendeleo na mgao wa rasilimali za kitaifa. Bw Mwashako alisema uamuzi wake wa kubaki upinzani ni kidemokrasia akiongeza kuwa wanasiasa wana haki ya kuwa na misimamo tofauti. "Kenya ni nchi ya kidemokrasia. Hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kujiunga na serikali," alisema. Alitoa mfano namna alitumwa na chama chake kwenda kumshawishi aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, kujiunga na Wiper baada ya kuhama kwenye chama tawala cha UDA. "Bi Jumwa alipoondoka UDA, walinituma nimshawishi kwa maneno matamu," alisema. Kauli yake inajiri wakati viongozi wanaomuunga mkono Rais William Ruto wakiongeza juhudi za kuimarisha ushawishi wao Pwani kuelekea uchaguzi wa 2027. Gavana wa Kilifi Gideon Mung'aro hivi majuzi alimtaja Bw Mwashako kama mmoja wa viongozi wachache wa Pwani ambao bado wako katika upinzani. "Juzi tulikutana kama wabunge na magavana wote wa Pwani huko Mombasa na tukakubaliana kushirikiana na Rais Ruto. Imebakia mbunge mmoja tu, Bw Mwashako, ambaye bado yuko upande wa upinzani," alisema. Bw Mwashako amekuwa akijiunga na kampeni za kisiasa za Linda Mwananchi inayohusishwa na viongozi wa upinzani Rigathi Gachagua na Bw Musyoka. Msimamo wa Bw Mwashako umeifanya kaunti ya Taita Taveta kuwa baadhi ya maeneo muhimu ya ushindani kati ya serikali na upinzani. Alisema anataka kuwa gavana ili kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi, zikiwemo uhaba wa maji, huduma za afya, elimu, kilimo na mzozo wa muda mrefu kuhusu mgao wa mapato yanayotokana na Hifadhi za kitaifa ya Wanyamapori zaTsavo. Bw Mwashako pia ameikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kutotimiza baadhi ya ahadi ilizowapa wakazi wa Pwani, akisema kujiunga na serikali kungeathiri uwezo wake wa kuiwajibisha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 17 Aug 2026 06:55:19

Kitany arai viongozi Bondeni wachape kazi hata wakiimba TuTam

MBUNGE wa Aldai, Marianne Kitany amewataka viongozi wa UDA Bonde la Ufa kukosa kulumbana huku akisisitiza yupo tayari kumenyana na mgombeaji yeyote anayesaka ubunge. Bi Keitany amesema kuwa rekodi yake ya maendeleo iko wazi na kwamba yupo tayari kumenyana na kiongozi yeyote lakini akasisitiza ubabe unaoendelea bondeni utatatiza kuchaguliwa kwa Rais William Ruto. "Siasa haihusu tena kulumbana na kutusiana, inahusu kazi ambayo umefanya. Mimi naamini kwamba nitachaguliwa tena Aldai kwa sababu ya kazi ambayo nimefanya na inaonekana," akasema Bi Kitany. Mbunge huyo alisema yupo tayari kuwania mchujo wa UDA na mgombeaji yeyote ambaye anamezea mate kiti chake kupitia chama hicho. "Saa hii wapinzani wangu wametoroka wote. Gavana wa sasa na mbunge wa zamani walikuwa wamesema watanipinga lakini sasa wamehepa hawana nia ya kuwania kiti hiki tena," akasema Bi Kitany. "Mimi niko UDA na siendi mahali popote na iwapo wanata kurudi kuwania basi niko tayari kupambana nao. Nikishindwa kwenye mchujo, sitaenda mahali popote, nitasalia tu UDA," akaongeza. Bi Keitany aliorodheshwa na TIFA kama mbunge ambaye ana utendakazi bora zaidi kati ya wabunge wanawake baada ya Naisula Lesuda wa Samburu Magharibi. Bw Sang' wiki jana alitangaza kuwa amejiondoa katika kiny'anganyiro cha ubunge baada ya kushauriana na Rais William Ruto na akimaliza muhula wake wa pili kama gavana, atakwea ngazi na kushiriki siasa za kitaifa. Mbunge huyo anayehudumu muhula wa kwanza alimkashifu Bw Sang' akisema utendakazi wake ni duni na hata iwapo angewania kiti hicho, hangeenda mahala popote. "Hospitali kadhaa hazifanyi kazi, hatuna mochari ya umma inayofanya kazi. Gavana mwenyewe ana shule za chekechea ambazo bado zimejengwa kwa udongo na hata bado tunayachota maji mtoni," akasema. "Mengi ambayo yametimizwa yanatokana na miradi ambayo imeanzishwa na serikali kuu. Hata sasa tunakuza miwa na kuwasilisha kiwanda cha Kibos," akasema. Gavana Sang' alisema kuwa hana nia ya kuwania kiti hicho cha ubunge na atamakinikia siasa za kitaifa. "Nina hiari kuwania cheo cha kisiasa na nilikuwa niwanie useneta au niwanie ubunge Aldai. Hiari hizi ni muhimu lakini baada ya kushauriana na Rais aliniambia nimakinikie kuchaguliwa kwake 2027. Kwa hivyo, nitakuwa nashiriki siasa za kitaifa wala sitagombea cheo chochote cha kisiasa," akasema Bw Sang'. Mwaka jana, Bw Sang alitangaza kuwa ifikiapo 2027 atakuwa na umri wa miaka 42 ambayo ni ya chini zaidi kwa mwanasiasa kustaafu. Hii ndiyo maana sasa alikuwa akilenga kiti cha ubunge wa Aldai. Bi Kitany alitaja kuwekwa lami kwa baadhi ya barabara, kuimarisha taasisi za elimu na kujengwa kwa masoko ya kisasa ambayo yamesaidia kuimarisha biashara katika eneobunge hilo.

read more