T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 14 Aug 2026 07:49:55

Mfumo wa kidijitali kusaidia wafugaji 30,000 wa ng'ombe wa maziwa

WAKULIMA wa miradi midogo ya ng'ombe wa maziwa watanufaika na mpango mpya wa kidijitali unaolenga kuwasaidia kupata huduma za kifedha, masoko rasmi na mikopo nafuu kwa kujenga rekodi za miamala za ukopaji zinazoweza kuthibitishwa. Farmer Visibility Project, ni mradi uliozinduliwa na Heifer International Kenya kwa ushirikiano na Mastercard, KCB Foundation na KCB Bank Kenya, na unalenga kuangazia changamoto za muda mrefu zinazokabili wakulima wa maziwa, zikiwemo biashara za fedha taslimu, ukosefu wa rekodi bora na ugumu wa kupata fedha. "Mpango huu wa majaribio wa miezi tisa unalenga wakulima wadogo 30,000 wa maziwa kote nchini na unatarajiwa kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa kuweka kidijitali uwasilishaji wa maziwa, malipo, akiba na ununuzi wa pembejeo," alisema Mkurugenzi wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome, wakati wa uzinduzi wa mpango huo Nairobi. Kulingana na Wairimu, wakulima wengi wa maziwa kwa sasa hutegemea miamala (transactions) isiyo rasmi, hali inayofanya iwe vigumu kwao kuonyesha historia ya kifedha inayohitajika na taasisi zinazotoa mikopo. Alisema kucheleweshwa kwa malipo ya maziwa na changamoto za fedha katika vyama vya ushirika pia zimewalazimu wazalishaji wengi kuuza maziwa kupitia njia zisizo rasmi, hali inayopunguza uwazi na kuwanyima fursa ya kupata masoko rasmi yanayolipa vizuri. Chini ya mradi huo, wakulima na vyama vyao vya ushirika watapewa mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali na elimu ya kifedha. Hali kadhalika, watasaidiwa kufungua akaunti za benki na kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali. [caption id="attachment_191120" align="aligncenter" width="300"] Mkulima akikama maziwa. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mpango huo unatarajiwa kuwezesha wakulima kujenga rekodi za kuaminika za miamala ambazo taasisi za kifedha zinaweza kutumia kuunda bidhaa zinazokidhi mizunguko ya uzalishaji na mahitaji ya fedha ya wakulima wa maziwa. Wairimu alisema mpango huo umeundwa kufanya wakulima waonekane zaidi katika mfumo wa kifedha na kutambuliwa kama wajasiriamali wanaoendesha biashara zinazoweza kuleta faida. "Wakulima wadogo ni wajasiriamali. Ni wamiliki wa biashara, wasambazaji, waajiri na wawekezaji katika jamii zao. Hata hivyo, wengi wao bado hawaonekani katika mifumo ya kifedha na masoko ambayo inaweza kuwasaidia kukua," alisema. Alidokeza kuwa mradi huo utawapa wakulima uwezo mkubwa wa kudhibiti data zao za biashara na kuwaunganisha na huduma za kifedha, masoko na fursa za kiuchumi. Chini ya ushirikiano huo, Mastercard inafadhili Heifer International Kenya kama mshirika mkuu wa utekelezaji, huku KCB Foundation na KCB Bank Kenya zikiwa washirika wa utekelezaji. Mastercard itatoa teknolojia yake ya Farm Pass kupitia jukwaa la Community Pass, litakalosaidia kuunda wasifu wa kidijitali wa wakulima, kufuatilia miamala na kuimarisha uhusiano katika mnyororo wa thamani, ikiwemo maeneo ya vijijini yenye upatikanaji mdogo wa huduma za kidijitali. Makamu Mkuu wa Rais wa Mastercard na Meneja wa Nchi za Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi, Shehryar Ali, alisema kuweka miamala ya wakulima katika mfumo wa kidijitali kutaimarisha ufuatiliaji na ujumuishaji wa kifedha. "Kwa uwekezaji wetu na matumizi ya suluhisho la Farm Pass, miamala ya wakulima itawekwa kidijitali, ufuatiliaji wake utaimarishwa na upatikanaji wa malipo na huduma za kifedha kurahisishwa," alisema. [caption id="attachment_191121" align="aligncenter" width="300"] Maziwa kwenye ndoo tayari kupelekwa sokoni. Picha|Sammy Waweru[/caption] Jukwaa hilo pia litawezesha malipo ya kidijitali, utoaji wa kadi na ununuzi wa pembejeo kupitia ushirikiano na taasisi za kifedha kama vile KCB Bank, huku wakulima wakijenga rekodi za kifedha zinazoaminika. KCB Foundation itasimamia uhamasishaji wa wakulima, kuimarisha vyama vya ushirika, kujenga uwezo, mafunzo ya elimu ya kifedha, ufuatiliaji na uratibu wa mradi. KCB Bank Kenya itawezesha wakulima kufungua akaunti, kutumia huduma za malipo ya kidijitali na kupata kadi, huku ikisaidia wafanyabiashara na mawakala kupokea malipo kwa njia ya kidijitali. Mkurugenzi Mkuu wa KCB Foundation, Mendi Njonjo, alisema ushirikiano huo unachanganya teknolojia na ujumuishaji wa kifedha ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa nchini. "Maendeleo endelevu ya jamii huanza kwa kuunda majukwaa yanayowawezesha watu kushiriki kikamilifu katika uchumi," alisema. Aliongeza kuwa mpango huo utasaidia wakulima kujenga biashara zinazostahimili misukosuko, kuongeza uzalishaji na kuboresha mapato ya jamii. Mradi huo unalenga kubadilisha mfumo wa malipo ya maziwa, kuimarisha vyama vya ushirika na kupanua huduma za kifedha za kidijitali katika sekta ya maziwa nchini iwapo utaenezwa kote nchini Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 14 Aug 2026 07:55:33

MAONI: Gachagua kinara wa upinzani ambaye Kenya inahitaji zaidi

MGALA muue, lakini haki yake umpe. Ni msemo unaoafiki zaidi kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua. Tangu atimuliwe kutoka wadhifa wa naibu rais karibu miaka miwili iliyopita, Gachagua amejitwika wajibu wa upinzani ambao Kenya inahitaji zaidi hasa kipindi hiki cha mageuzi. Ni kiongozi pekee aliyedhihirisha ujasiri wa kuikabili serikali ya Kenya Kwanza na Rais Ruto, kuikosoa, kuitisha majibu na kufichua masuala tata na ya kustaajabisha serikalini huku akiwaacha wahusika bila hiari ila kufunguka na kuungama kwa Wakenya. Mfano hai ni kuhusu mkataba wa mabilioni ulioshirikisha bilionea wa India na uliolenga miundomsingi muhimu kwa umma ikiwemo JKIA, ambao huenda ungesalia siri na kugharimu pakubwa vizazi vijavyo nchini, lau asingelifichua. Ufichuzi wake majuzi kuhusu hotuba ya rais kuzindua Ruwaza 2060, na katika tukio la kuhuzunisha na kuhofisha, lililohusu mauaji ya kikatili ya mwanamke, yaliyopangwa na kutekelezwa na kundi la maafisa wa polisi wanaohudumu! Gachagua alifichua hadharani kwamba, maafisa wa polisi walihusika na mauaji hayo ya kikatili pamoja na kiini chake huku akimtaka DCI kuwaeleza Wakenya ukweli la sivyo angewatambulisha maafisa husika. Saa chache baadaye, mkuu wa DCI kupitia taarifa alithibitisha madai ya Gachagua akitaja maafisa husika, vituo vyao vya kazi, mmiliki wa bunduki iliyotumika kukatiza maisha ya Dkt Mutiso na hata kiini chake. Isingelikuwa ni ufichuzi wa Gachagua, huenda Wakenya wangesubiri kwa muda mrefu au hawangejua kabisa ukweli huo wa kutisha, huku mauaji hayo, sawa na ya Wakenya wengine wengi, yakiishia kusahaulika. Ujasiri wa kukabili serikali, ufasaha wa kuzungumzia masuala yanayoathiri raia na usahihi katika ufichuzi wake ni sifa adimu ambazo zimemvutia wandani na maadui kwa usawa. Umpende au umchukie, ni vigumu kupuuza nafasi muhimu aliyojitwika ya kinara wa upinzani tangu afurushwe. Sio kwamba hana mapungufu yake, hali inayomfanya kuwa binadamu. Kiongozi wa upinzani hatarajiwi kuwa mkamilifu na kila dai analotoa si lazima liwe kweli kila wakati. Kenya kama taifa linaloongozwa na demokrasia inastahili upinzani usiochelea kuuliza maswali mazito, kukosoa utawala unapokwenda mrama na kushinikiza taasisi za kiserikali kuwajibika kwa umma. Demokrasia inaruhusu taasisi kama vile polisi na DCI uhuru kuendesha oparesheni na vilevile inatoa nafasi kwa upinzani thabiti kuhakikisha uangalizi na uwajibikaji. Kinyume cha matarajio kwamba angesahaulika upesi na jina lake kuzikwa katika kaburi la sahau, Gachagua amezidi kutamba katika ulingo wa kisiasa na hasa kama jicho la mwananchi wa kawaida serikalini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 14 Aug 2026 06:55:58

Mpango wa Kangaroo ulivyosadia kumuokoa mwanawe

PUNDE tu baada ya mkewe kujifungua, David Omollo alijikuta kati ya furaha na wasiwasi. Mkewe alijifungua ujauzito ukiwa na miezi saba badala ya muda wa kawaida wa miezi tisa.Hali hiyo ilichangiwa na uvimbe aliokuwa nao kwenye kizazi wa fibroids. "Mke wangu alijifungua salama sana bila kufanyiwa upasuaji lakini kwa sababu tulimpata mtoto kabla ya muda, muuguzi alisema kuwa anastahili kuwekwa kwenye incubator. Hata hivyo, nilikataa jambo hilo. Nilitaka kumlinda mwanangu nje ya hospitali," anasimulia mzazi huyo. Usimamizi wa hospitali hatimaye uliitikia wito wa David na kumshauri kufanya mpango wa Kangaroo Mother Care (KMC)ambapo ngozi zinatagusana. "Nilionyeshwa jinsi ya kuufanya mpango huo. Nilichukua likizo ya wiki mbili kazini na kutumia fursa hiyo kumweka mtoto wangu kwenye kifua wakati wote huku mke wangu alipokuwa akiendelea kupona. Usiku tulikuwa tukisaidiana. Nilikuwa baba mwenye furaha sana," anaeleza kwa tabasamu. Kwa pamoja, anasema kuwa walimfanyia mwanao mpango huo wa KMC katika kipindi cha miezi sita mfululizo. Wakati huo, David anasema kuwa mtoto wao alikuwa ameonyesha ishara za kuwa mchangamfu na kuwa na uwezo wa kula vyakula vingine kando na maziwa. "Mtoto wetu alipofikisha umri wa miezi mitano, tulianza kumlisha aina tofauti ya vyakula. Uzuri ni kuwa hakuwa akisumbua kula, alipenda kula vizuri. Pia alikuwa akilala vizuri sana kwenye kifua na hata kitandani tulipomaliza mpango wa Kangaroo," David anasimulia. Ili kufanya mpango wa KMC, mzazi anahitaji kiti au kitanda ambacho anaweza kukalia kwa muda mrefu sana bila kuchoka au kuhisi maumivu. Mzazi anayefanya mpango huu, anastahili kutoka tu kwenye kiti au kitanda hicho anapoenda msalaani. Mtoto anastahili kuvuliwa nguo na kuvalishwa tu kofia, nepi na soksi kisha mtoto anawekwa wima katikati ya matiti kisha anafunikwa na shuka iliyo na joto la kutosha kumzuia mtoto kupata baridi. Haya ni kwa mujibu wa muuguzi anayesimamia kitengo cha watoto walio chini ya umri wa mwezi moja katika hospitali ya Aga Khan University, Joyce Njoki Wanjohi. "Mpango wa Kangaroo Mother Care unashauriwa pindi tu mtoto anapozaliwa. Mtoto anastahili kuwekwa wima kwenye kifua cha mama bila nguo. Unastahili kuwa kwa muda wa kati ya saa 20-24 mfululizo lakini kutokana na sababu tofauti, baadhi ya wazazi hawawezi timiza muda huo. Hivyo hata dakika 60-90 kila siku bado zina faida," anaeleza muuguzi huyo. Lakini je, ni sayansi gani iliyo chini ya mpango wa KMC? "Kuna uhamisho wa bakteria zilizo na kinga kutoka kwenye ngozi ya mama au baba wa mtoto ambazo ni salama zinapohamishwa kwenye ngozi ya mtoto zinafanya kazi ya kumkinga mtoto. Hivyo, watoto wengi wanapofanyiwa mpango huu huwa hawapati maambukizi makali wakilinganishwa na wenzao ambao hawajawekwa kwenye mpango huo," anaeleza muuguzi. Mpango huo anasema kuwa una manufaa mengi yanayohusiana na ukuaji wa ubongo na mwili kwa kusaidia sana ustawi wa mtoto. Pia unapunguza msongo wa mawazo miongoni mwa watoto. "Kunakuwa na ubora wa mtoto anavyokuwa kiuzito, urefu na pia mzingo wa kichwa jambo ambalo ni muhimu sana likiboreshwa miongoni mwa watoto wa njiti. Pia kunakuwa na kinga bora na kupunguza maambukizi makali," anasema Bi Joyce. Aidha anaeleza kuwa mpango wa KMC huongeza unyonyeshaji. "Punde tu mtoto anapowekwa kwenye titi, mpango huo hufanya miujiza kwa sababu kunakuwa na uzalishaji wa homoni ya oksitosin inayosaidia mtiririko wa maziwa. Mara nyingi unaona mama anapomshikilia mtoto na maziwa yanatiririka kwa sababu kuna uhusiano kati ya mama na mtoto," anaeleza. Licha ya kuwa mpango wa KMC kwa kiasi kikubwa unafanywa na kina mama, muuguzi huyo anasema kuwa, kina baba pia wanashauriwa kuufanya. "Kumshika mtoto wako kuna faida kadhaa na hivyo unahisi mtoto wako si mgonjwa sana. Pia kunakuwa na ushirikiano bora kati ya mtoto na mzazi. Wakati uo huo, mzazi anakuwa na matumaini kwa sababu yeye pia ni miongoni mwa wanaomtunza mtoto. Anapoona mabadiliko kwenye afya ya mtoto, anapiga ripoti kwa wahudumu wa afya," anaeleza. Mpango wa Kangaroo Mother Care unafanywa katika kiwango kikubwa kwenye mazingira ya hospitali ambapo mama wa mtoto anakusudiwa kutokuwa na kazi yoyote ya kufanya isipokuwa kumlea mtoto. Hata hivyo, muuguzi huyo anasema kuwa watoto walio na uzani wa chini wanaporuhusiwa kutoka kwenye hospitali haswa zile za umma, wakiwa na kilo 1.8, wazazi wao hushauriwa kuendelea kuwafanyia mpango huo kwa muda mrefu kulingana na uwezo wao wakiwa nyumbani. "Hospitali tofauti za umma, zina vyumba vya Kangaroo Mother Care ambapo akina mama hukaa, kula na kuwa na wanao muda wa saa 24 kila siku. Pia kunahimizwa kuwa mzazi wa kiume aende hospitalini na kumsaidia mama," anasema. Mpango huo unatumika pakubwa nchini Kenya haswa katika hospitali za umma. Kulingana na UNICEF, mpango huu wa KMC, ulibuniwa katika nchi ya Colombia kuwasaidia watoto wa njiti kukuwa wakati ambapo vifaa vya kuwalelea havikuwepo au vilikuwa vichache. "Tafiti nyingi za kisayansi zinaonyesha kuwa Kangaroo Mother Care ni bora zaidi kuliko mtoto anapowekwa kwenye incubator. Mpango huu umedhihirisha kuwa muhimu sana na ulio na faida kwa mtoto," muuguzi anaeleza. Kulingana na data kutoka shirika la Afya Duniani, WHO, kufikia mwaka wa 2024, kulikuwa na asilimia 17.2 ya vifo katika kila watoto 1000 waliozaliwa. Watoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa ya ujauzito, maambukizi ya watoto walio chini ya siku 28 na matatizo wakati wa uzazi ni miongoni mwa sababu za vifo katika kipindi hicho kote duniani. "Kiwango cha vifo vya watoto wachanga sana nchini Kenya ni vifo 21 katika kila watoto 1000 wanaozaliwa. Mara nyingi, vifo hivi hutokea katika kipindi cha siku 28 za mtoto kuzaliwa. Ni muhimu sana kwetu kuukumbatia mpango wa Kangaroo Mother Care kwa sababu umeonyesha kuwa na faida kadhaa," anashauri Bi Joyce. Kwa baba huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 54, japo mkewe aliaga dunia miezi tisa tu baada ya kujifungua, anasema kuwa mpango wa Kangaroo Mother Care ulimuokoa mwanae ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 18. "Kangaroo Mother Care ilimuokoa mwanangu. Japokuwa yeye ni mtoto wa njiti, ni kijana hodari aliye na nguvu na anapenda kazi zinazohitaji nguvu nyingi. Mwaka huu atajiunga na chuo anuai kusomea kozi ya ujenzi," anasema mzazi huyo wa watoto wanne.

read more