T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 14 Sep 2026 10:10:53

Francis Atwoli: Miaka 25 akipambania wafanyakazi; muhula wa sasa utaenda hadi 2031

ALIANZA kama kijana wa miaka 18 aliyekuwa na kazi katika shirika la posta na mawasiliano. Hakujua kwamba hatua yake ya kwanza ya kuwakilisha wafanyakazi wenzake ingebadilisha maisha yake na kumweka katika uongozi kwa zaidi ya nusu karne. Leo, jina la Francis Atwoli ni kubwa katika ulimwengu wa wafanyakazi Kenya. Kwa miaka 25 amekuwa akiongoza Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu-K), akihudumu katika awamu za kisiasa za marais tofauti na misukosuko ya kiuchumi iliyobadilisha maisha ya mamilioni ya Wakenya. Na Machi mwaka huu, wafanyakazi walimwambia bado hawataki aondoke. Atwoli alichaguliwa bila mpinzani kwa muhula wa sita wa miaka mitano katika mkutano wa wajumbe wa Cotu uliofanyika Tom Mboya Labour College, Kisumu. Muhula huo utaendelea hadi 2031. Kwa mwanamume ambaye amekuwa katika uongozi wa shirika hilo tangu 2001, uchaguzi huo ulikuwa zaidi ya ushindi mwingine. Ulikuwa thibitisho la uimara wa uongozi wake ndani ya shughuli za wafanyakazi. Lakini nyuma ya jina la Atwoli kuna safari ndefu. Safari yake katika vyama vya wafanyakazi ilianza baada ya kumaliza shule ya sekondari. Aliajiriwa na East African Posts and Telecommunication Administration akiwa na umri wa miaka 18. Ndani ya miezi miwili tu, alichaguliwa bila mpinzani kuwa mwakilishi wa wafanyakazi katika tawi la Nairobi la Union of Posts and Telecommunication Employees. Akiwa na miaka 21, alichaguliwa kuwa katibu wa tawi la Nairobi. Hapo ndipo safari yake ya muda mrefu katika harakati za wafanyakazi ilipoanza kwa nguvu. Mwaka 1967, alijiunga rasmi na harakati za wafanyakazi, safari ambayo Cotu baadaye iliitaja alipoadhimisha miaka 50 katika harakati hizo mwaka 2017. Kwa Atwoli, uongozi haukuwa suala la cheo pekee.Ulikuwa kuhusu uwezo wa wafanyakazi kujitetea. Alitumwa Italia kusomea masuala ya ajira katika Turin College of Labour Studies, ambako alipata nafasi ya kupanua uelewa wake kuhusu harakati za wafanyakazi duniani. Aliporudi Kenya, aliendelea na shughuli za chama.Mwishowe, msimamo wake ulimgharimu kazi. Kwa mujibu wa wasifu wa Cotu, alistaafishwa mwaka 1986 kwa kile kilichoelezwa kuwa kushiriki katika shughuli za chama cha wafanyakazi. Lakini kuondoka kazini hakukumaliza safari yake.Kulikuwa mwanzo wa hatua nyingine. Atwoli baadaye akawa Katibu Mkuu wa Kenya Plantation and Agricultural Workers Union (KPAWU). Alijenga jina katika sekta ya kilimo, hasa katika masuala yaliyohusu wafanyakazi wa mashambani. Kufikia 2001, alikuwa tayari amejijengea ushawishi mkubwa katika harakati za wafanyakazi. Mwaka huo, mpenzi huyo wa rhumba alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Cotu baada ya kuungwa mkono na vyama 26 kati ya 29 vilivyokuwa wanachama wa shirika hilo. Huo ulikuwa mwanzo wa enzi yake. Na miaka 25 baadaye, bado yuko katika kiti hicho. Ingawa Cotu ni shirika la wafanyakazi, Atwoli hakuwahi kujitenga kabisa na siasa za Kenya. Shirikisho hilo lilifanya kazi pamoja na upinzani wa National Rainbow Coalition (Narc) mwaka wa 2002, uliokuwa ukimuunga mkono Mwai Kibaki katika uchaguzi wa urais. Kibaki alishinda uchaguzi huo na kumaliza utawala wa Kanu uliokuwa umechukua miaka 40. Tangu wakati huo, Atwoli amekuwa mtu ambaye kauli zake kuhusu siasa za Kenya zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu. Huwa anaunga mkono au kukosoa serikali kulingana na masuala yaliyo mbele yake huku akisisitiza lazima Cotu ifanye kazi na serikali iliyo mamlakani kwa maslahi ya wafanyakazi. Lakini pia amesisitiza kwamba Cotu ni shirika la wafanyakazi na si chama cha kisiasa. Kwa mujibu wa msimamo rasmi wa Cotu, wanachama wake wana uhuru wa kuunga mkono vyama tofauti, huku shirika likishirikiana na serikali iliyoko madarakani kwa masuala yanayohusu wafanyakazi. Hapo ndipo moja ya mambo yanayomfanya Atwoli kuwa mtu wa kipekee yanapoonekana. Anaweza kuwa mkosoaji wa serikali katika suala moja na kuiunga katika suala jingine mradi tu linahusu maslahi ya wafanyakazi. Kwa miaka yake yote Cotu, suala la mishahara limekuwa mojawapo ya ajenda zake kuu. Atwoli amekuwa akisisitiza umuhimu wa mshahara wa chini unaomwezesha mfanyakazi kuishi kwa heshima.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 14 Sep 2026 07:55:41

Viongozi wa upinzani waeleza wasiwasi kuhusu kuenea kwa ghasia kuelekea 2027

VIONGOZI wa upinzani wakiongozwa na vinara wa Wiper Patriotic Front, Bw Kalonzo Musyoka, Democratic Party Bw Justin Muturi na mwenzao wa DAP-Kenya Bw Eugene Wamalwa, wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama nchini, wakionya kuwa ghasia za kisiasa zinaweza kuhatarisha uchaguzi mkuu wa 2027. Viongozi hao walinukuu tukio la hivi majuzi kaunti ya Embu ambapo Naibu Rais Kithure Kindiki alilazimika kukimbilia usalama wakati wa mkutano wa hadhara baada ya kuzuka kwa ghasia. Walisema tukio hilo limeibua maswali kuhusu usalama wa viongozi na Wakenya wa kawaida. Bw Musyoka aliwataka Wakenya kuombeana amani, huku akiikosoa idara ya usalama kwa kile alichokitaja kuwa ni kumdhulumu Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji kufuatia tukio hilo. "Kama viongozi, tunalaani tukio hilo. Kuuzingira nyumba ya mbunge ni jambo la kusikitisha… kwa sababu tumeambiwa kwamba wakazi walisikia kuwa kulikuwa na pesa zikigawiwa, hivyo wakakimbilia kwenye mkutano kupata sehemu yao. Hilo ndilo lililosababisha vurugu, lakini kwa nini kumlaumu mbunge?" aliuliza. Bw Musyoka alisema aliwahi kumtetea Bw Mukunji kama wakili wakati mbunge huyo alishtakiwa kwa kujihusisha na ugaidi. "Alifikishwa mahakamani na kushtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi," alisema, akiongeza kuwa Bw Mukunji hapaswi kudhulumiwa. Alisema Bw Muturi atamtetea mbunge huyo. Bw Musyoka alihoji hali ya usalama nchini, akisema tukio lililomhusisha Naibu Rais linaonyesha kuwa hata maafisa waandamizi wa serikali wako katika mazingira hatarishi. "Tuombeane. Kwa kweli, kwa wakati kama huu, nchi yetu iko katika hali mbaya. Unapomwona Naibu Rais wa Jamhuri akikimbilia msituni kwa usalama, lazima ujiulize, usalama uko wapi? Ikiwa Naibu Rais anakimbilia msituni kwa usalama, raia wa kawaida ataenda wapi?" aliuliza Bw Musyoka. Pia alirejelea tukio la hivi majuzi ambapo msafara wa viongozi wa upinzani ulipigwa mawe walipoingia Garissa. "Tulikuwa na tukio Garissa, lakini tulikaribishwa vizuri sana Kaskazini Mashariki. Sasa tuko katika eneo la Pwani kuzungumza na Wakenya kuhusu changamoto zinazoikabili nchi hii," alisema. Bw Wamalwa alisema viongozi wa upinzani wameazimia kuendelea kutembelea maeneo mbalimbali nchini licha ya uhasama waliokumbana nao katika baadhi ya maeneo. Alifananisha kuingia kwao Garissa na kuingia kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) Kismayu, Somalia, akisema walikumbana na upinzani kutoka kwa makundi aliyodai yalikuwa yamehamasishwa dhidi yao. "Tulihangaika kuingia katika eneo hilo, kwa sababu hii ni timu ya Serikali Mbadala ya Umoja, upinzani wa kwanza kuingia Kaskazini Mashariki. Hata hivyo, serikali haikutaka tuende kueneza ujumbe wetu Kaskazini Mashariki," alisema. Bw Wamalwa alidai kuwa makundi yaliyowakabili yalikuwa yamehamasishwa na Serikali, madai ambayo hayakuweza kuthibitishwa kwa njia huru. Alisema makabiliano kati ya upinzani na tukio la Embu yanapaswa kuwa onyo dhidi ya matumizi ya ghasia katika siasa. "Hakuna mtu anayeweza kudhibiti uhuni," alisema Bw Wamalwa, akitaja Haiti ambako alisema wanasiasa waliwahi kutegemea magenge kabla ya kuyapoteza kabisa mamlaka ya kuyadhibiti. "Hatutaki kwenda katika njia hiyo; tunataka nchi yenye amani na uchaguzi wa amani. Wale walio serikalini, wale wanaotaka kupanda chui wa ghasia, mwishowe mtaliwa na huyo chui kwa sababu hamtakuwa na uwezo wa kudhibiti uhuni au ghasia," alisema. Bw Wamalwa aliwataka Wakenya kudumisha amani huku nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu wa 2027. "Ni lazima tuombee nchi hii, tuwe vyombo vya amani. Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, zikiwa zimesalia miezi 10 pekee kabla ya uchaguzi. Wakenya wote waruhusiwe kuwachagua kidemokrasia viongozi wanaowataka madarakani," alisema. Aliwataka viongozi kuruhusu wanasiasa kufanya kampeni kwa uhuru katika maeneo yote ya nchi bila kujali misimamo yao ya kisiasa. "Iwe uko muhula wa pili au wa kwanza, ni lazima tuwe mabalozi wa amani na tuchague yeyote tunayemtaka kidemokrasia. Hiyo ni haki yenu. Viongozi pia wanapaswa kuwa huru kutembelea sehemu yoyote ya nchi kutafuta kura," alisema. Bw Muturi alisema mazingira ya kisiasa nchini yamezidi kuwa yenye vikwazo, akidai kuwa maafisa wa usalama walizunguka kanisa ambako viongozi wa upinzani walikuwa wameenda kuomba. "Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, kanisa linazingirwa na maafisa wa usalama wenye silaha kwa sababu viongozi wa upinzani wameenda kuomba," alisema. "Hata wakati wa siku za giza za mfumo wa chama kimoja, haikuwahi kuwa hivi. Wakenya, tuombe kwa Mungu. Wakenya lazima wawe na uhuru wa kuwa na misimamo yao, kuieleza na kushirikiana na yeyote wanayemtaka. Hiyo ndiyo demokrasia," alisema Bw Muturi. Alimtetea Bw Mukunji, akisema mbunge huyo hapaswi kulaumiwa kwa vurugu zilizotokea Embu. Bw Muturi alidai kuwa zaidi ya watu 20,000 walikusanyika baada ya kusikia kuwa pesa zilikuwa zikigawiwa katika mkutano huo. Aliitaka serikali kuhakikisha usalama wa kutosha kwa wakenya wote na viongozi wa kisiasa huku nchi ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

read more