T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 14 Sep 2026 06:55:02

Shahbal aanza kurindima ngoma akilenga ugavana Mombasa

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal ameanza kufufua mtandao wake wa kisiasa katika kaunti ya Mombasa akijitayarisha kwa kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2027, huku akimuonya Rais William Ruto dhidi ya kuteua mgombea mmoja wa ugavana katika eneo hilo. Bw Shahbal alisema hatua hiyo inaweza kumnyima kura katika kaunti hiyo akimsihi ajifunze kutoka kwa makosa ya marehemu Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Bw Shahbal alimuonya Rais Ruto dhidi ya mipango ya kisiasa inayoweza kuwaondoa wagombea wengine katika kinyang'anyiro cha ugavana ili kumuunga mkono mgombea mmoja anayependekezwa na ikulu. Alisema kuwa kuwepo kwa wagombea wengi kutamnufaisha Rais kwa kuwa kila mmoja atakuwa akifanya kampeni na kuwahamasisha wapiga kura. "Ikiwa kuna watu wengi katika kinyang'anyiro, Rais atapata kura nyingi kwa sababu wote watafanya kampeni kwa ajili yake. Lakini ikiwa ni mtu mmoja, ambaye ni mgombea wa Rais hapa Mombasa, wanampotosha Rais," alisema. Bw Shahbal, ambaye hivi majuzi alipuuza ushauri wa Rais Ruto wa kutogombea kiti cha ugavana wa Mombasa, alikutana na zaidi ya wanachama 300 wa kundi lake la "Shahbal Movement" katika mkutano ulioandaliwa chini ya kaulimbiu ya "Mombasa is calling" kujadili namna ya kufufua mtandao wake wa kisiasa mashinani. Alisema mkutano huo haukuwa uzinduzi rasmi wa kampeni yake, bali ulikuwa mwanzo wa maandalizi ya kuimarisha mtandao wake kabla ya kuanza kuwafikia wananchi mashinani. "Huu ni mkutano wa viongozi wetu wa 'Shahbal Movement'. Bado sijafanya mkutano wa mashinani. Tutakapoenda kwa wananchi, mambo yatakuwa tofauti kabisa. Nimewaambia watu wangu kwamba kwa miezi mitatu ijayo tunajitayarisha. Hatuna haraka. Tsunami itaanza Januari mwakani," alisema. Mfanyabiashara huyo aliwashutumu baadhi ya wanasiasa wanaounga mkono mfumo wa kugawana maeneo ya kisiasa, akisema wanataka kupewa njia rahisi ya ushindi badala ya kwenda mashinani kuwashawishi wapiga kura. "Upuuzi huu wa kugawana maeneo umeanzishwa na watu wanaoogopa kwenda mashinani kukutana na wananchi. Wanataka usalama; wanataka kupewa njia rahisi ya ushindi," alisema. "Ikiwa una imani na uongozi wako, nenda kwa wananchi uwaambie ulichowafanyia nao watakuchagua. Kwa nini una hofu kubwa kiasi cha kutaka kuwazuia watu wengine kugombea?" Bw Shahbal pia aliwakosoa viongozi wa UDA wanaodai kuwa wanaweza kumhakikishia Rais idadi kubwa ya kura bila kuwepo kwa ushindani. "Nina hakika watu wa UDA wananisikiliza. Wanampotosha Rais. Hakuna yeyote kati yao anayeweza kuhakikisha kwamba wapiga kura watatoka bila ushindani," alisema. Alitaja Nyanza kama mfano, akidai kuwa baadhi ya wagombea wanaopata tiketi ya ODM bila ushindani wa ndani hupoteza ari ya kufanya kampeni.  "Hili ndilo kosa tulilofanya Nyanza. Mara tu mtu anapopewa cheti cha ODM, anapoteza hamu, anarudi nyumbani na kulala kwa sababu tayari ameshinda. Hivyo ndivyo Bw Odinga alipoteza kura Nyanza," alisema. Bw Shahbal pia alidai kuwa tiketi ya ODM imekuwa ikitumika Mombasa kuwashinikiza wagombea kuunga mkono chama hicho au kukosa tiketi. "Safari hii wanaweza kubaki na cheti chao. Sisi tuna mipango," alisema. Kauli zake zinajiri wakati ambapo wanasiasa kadhaa wameanza kujipanga kwa uchaguzi wa ugavana wa Mombasa wa 2027. Miongoni mwa wanaotajwa katika kinyang'anyiro hicho ni Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar, Gavana wa sasa Abdulswamad Nassir wa ODM, Mbunge wa Nyali Mohammed Ali na aliyekuwa Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo. Wiki iliyopita, Bw Omar aliunga mkono uamuzi wa Bw Shahbal kugombea, huku akipinga mikataba ya kisiasa au mfumo wa kugawana maeneo ambao unaweza kuwalazimisha baadhi ya wagombea kujiondoa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 14 Sep 2026 05:55:48

Watatu wanaotumia Tiktok kuwalaghai akina dada wanyakwa

WATU wanaoshukiwa kutumia TikTok kuwavuta vijana katika mitego ya uhalifu wamekamatwa na polisi jijini Nairobi, huku uchunguzi ukionyesha huenda kuna wahalifu wanaowalenga Wakenya mitandaoni. Washukiwa hao, Emanuel Bosire Arisa, Brian Gatheru Nderitu na mtoto mmoja, wanazuiliwa kwa siku 21 huku wapelelezi wakikusanya ushahidi dhidi yao. Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), washukiwa hao walikuwa wakiendesha ukurasa wa TikTok usiojulikana walioutumia kuwasiliana na waathiriwa kabla ya kupanga kukutana nao ana kwa ana. Mmoja wa waathiriwa ni Nzumari, jina limebadilishwa kwa sababu ni mtoto, ambaye alikutana na washukiwa hao baada ya kwanza kumsifu kupitia TikTok na baadaye kumshawishi kuhamishia mazungumzo WhatsApp. Mazungumzo hayo yaligeuka kuwa ya kimapenzi kabla ya washukiwa kumwalika Ruai, Nairobi, akiamini angeenda kujiburudisha. Hata hivyo, inadaiwa walimpeleka eneo lililotengwa ambako walimnyanyasa kingono na kumpora simu. Washukiwa hao pia walidaiwa kumlazimisha kutoa nambari yake ya siri ya M-Pesa. Baadaye walimtishia mama yake wakimtaka atume pesa zaidi na kumuonya kuwa wangemtupa Nzumari iwapo hangetii. Hatimaye walimwacha katika eneo asilolijua akiwa amesononeka. DCI ilisema washukiwa hao wametambuliwa na waathiriwa watano katika visa tofauti vilivyoripotiwa Buruburu, Embakasi na Ruai. Afisa wa DCI wa Ruai Henry Kinyua alisema polisi wamepokea visa sita vyenye mtindo unaofanana huko Ruai tangu Julai. Kisa kingine kiliripotiwa Imara Daima na viwili Buruburu. "Baada ya anayelengwa kuwaamini, mtu huyo humwaalika walale kwake au kwenda kujiburudisha. Lakini mwaathiriwa anapofika, hugeukwa kisha huibiwa na hata kudhulimiwa kimapenzi," akasema Bw Kinyua. Polisi walipata simu sita kutoka kwa washukiwa hao pamoja na makoti mawili yenye kofia yaliyodaiwa kutumiwa kuficha utambulisho wao wakati wa uhalifu. Bw Kinyua alisema mmoja wa washukiwa alikuwa akimtumia mdogo wake kuwachukua waathiriwa, kwa kuwa umri wake uliwafanya wasiwe na mashaka. Alisema washukiwa hao pia walitumia picha na video zinazoonyesha maisha ya kifahari kwenye mitandao kuwavutia waathiriwa. "Tulipofungua kurasa hizo tuligundua kuwa kijana huyo anachapisha sana maisha ya kifahari, hali iliyowavutia watu kwa mtu huyu anayeishi maisha ya kifahari ilhali kumbe ni mhalifu," akasema. Mwanasaikolojia wa watoto na vijana Winnie Ndung'u alisema vijana wako katika hatari ya kutumiwa na wanyanyasaji kwa sababu akili zao bado zinaendelea kukomaa. "Wanatumia ukweli kwamba akili ya mtoto bado haijakomaa kikamilifu ili kufanya maamuzi thabiti na huanza kuwavutia kwa mambo wanayopenda kabla ya kuwanyanyasa," akasema. Ripoti ya UNICEF ilionyehsa kuwa asilimia 67.3 ya watoto walipitia unyanyasaji. Kati yao, asilimia 25.5 hawakujua mahali pa kuripoti, asilimia 22.1 waliona aibu, huku asilimia 14.6 wakiogopa kupata matatizo iwapo wangezungumza.

read more