T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 12 Nov 2026 05:55:07

Iran yakwamilia madini ya nyuklia, yaambia Amerika ikiichokoza tena 'itakipata'

TEHRAN, Iran: IRAN imesema haitaruhusu hata chembe kimoja cha madini yake ya nyuklia yaliyorutubishwa kusafirishwa nje ya nchi na kuonya kuwa Amerika itakabiliwa vikali iwapo itafanya mashambulizi mengine dhidi yake. Mkuu wa masuala ya usalama Iran, Mohsen Rezaei, alisema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Mayadeen cha Lebanon kinachounga mkono Iran. Kauli yake inajiri wakati maafisa wa Amerika wanapunguza shinikizo za kutaka hatua zaidi za kijeshi zichukuliwe dhidi ya Iran. Wachanganuzi wanasema Rais Donald Trump amekuwa akitumia lugha ya adabu na kutuma ishara ya maridhiano tangu chama chake cha Republican kishindwe katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 3. Rezaei alisema hakuna mazungumzo yanayoendelea kwa sasa kati ya Tehran na Washington. "Shambulizi lolote jipya la Amerika litajibiwa kwa kulenga vituo vyake vya kijeshi vilivyo mbali," akasema. Aliongeza kuwa Kiongozi Mkuu wa Dini Iran Mojtaba Khamenei ametoa amri kuwa urani iliyokaribia kiwango cha kutumika kutengeneza silaha za nyuklia isisafirishwe nje ya nchi. Maafisa wawili wakuu wa Iran walithibitisha mnamo Mei kuwa kulikuwa na agizo hilo. "Tunahitaji madini hayo yaliyorutubishwa ili kutengeneza meli zinazotumia nyuklia," akasema Rezaei. Aliongeza kuwa Tehran tayari imeifahamisha Moscow kuwa madini hayo yatasalia Iran na kwamba serikali itayatumia yenyewe. Urusi ilikuwa imejitolea kuondoa urani Iran kama sehemu ya makubaliano yanayoweza kupunguza wasiwasi wa Amerika kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran. Hata hivyo, Moscow ilisema uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo ni wa Iran. Shirika la Kimataifa la Kawi ya Atomiki (IAEA) linakadiria kuwa Iran ilikuwa na kilo 440.9 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 kabla ya Israel na Amerika kushambulia vituo vyake vya nyuklia Juni 2025. Kiwango hicho ni kikubwa zaidi ya kinachohitajika kwa matumizi ya kawaida ya kiraia. Hata hivyo, haijulikani ni kiasi gani cha urani hiyo kilinusurika baada ya mashambulizi hayo. Israel, Amerika na mataifa mengine ya Magharibi yamekuwa yakiishutumu Iran kwa kutaka kutengeneza silaha za nyuklia, madai ambayo Tehran imekuwa ikiyakanusha. Washington imesisitiza kuwa masuala ya nyuklia lazima yawe sehemu ya mazungumzo yoyote ya awali yanayolenga kumaliza vita kati ya mataifa hayo mawili. Wiki iliyopita, afisa mmoja wa ngazi ya juu Iran alisema kuwa Tehran ilikuwa imetuma pendekezo kuhusu mpango wake wa nyuklia kwa Amerika kupitia Qatar. Hata hivyo, afisa huyo alisema Iran iko tayari kujadili pendekezo hilo baada ya Washington kutimiza masharti saba ambayo Tehran imewasilisha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 12 Nov 2026 04:55:24

Watu wa 'wash wash' wamefikiwa? Bunge laanzisha hatua kukabili magenge ya utakatishaji pesa

WABUNGE wameanzisha hatua za kuimarisha vita dhidi ya wahalifu wanaoficha fedha zinazotokana na uhalifu kwa kuzibadilisha kuwa sarafu za kidijitali ili kuficha chanzo chake. Pendekezo la kurekebisha sheria ya kukabiliana na ulanguzi wa fedha linalenga kupatia idara za uchunguzi mamlaka zaidi ya kufuatilia, kuzima na kutwaa mali ya kidijitali inayohusishwa na uhalifu. Hatua hiyo inawalenga pia wanaojulikana kama 'wash wash' au 'sharp boys', ambao baadhi yao hutumia mifumo ya kifedha na teknolojia kuficha fedha zinazotokana na shughuli haramu. Sarafu za kidijitali ni fedha zinazohamishwa kwa njia ya kielektroniki bila kutegemea mifumo ya kawaida ya benki. Miamala yake hurekodiwa kupitia teknolojia ya blockchain, ambayo hutumika kuhifadhi na kuthibitisha taarifa za kuhamisha fedha. Mnamo Jumanne, wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria waliunga mkono pendekezo la Shirika la Kufuatilia na Kurejesha Mali (ARA) la kurekebisha Sheria ya Mapato ya Uhalifu na Kupambana na Ulanguzi wa Fedha. Marekebisho hayo yanapendekezwa kupitia mswada wa mwaka 2026 ambao kwa sasa unachunguzwa na kamati hiyo kabla ya kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi. ARA inataka ufafanuzi wa mali katika sheria hiyo upanuliwe kujumuisha sarafu za kidijitali na mali nyingine inayohifadhiwa kupitia teknolojia ya kisasa. Kwa mujibu wa shirika hilo, hatua hiyo itatoa msingi wa kisheria kwa maafisa wa uchunguzi kutambua, kufuatilia, kuzima na kutwaa mali hiyo inapohusishwa na uhalifu. "Upanuzi wa ufafanuzi wa mali utatoa uhakika wa kisheria kwamba mali kama sarafu za kidijitali inaweza kutambuliwa, kufuatiliwa, kuzuiwa, kutwaliwa na kurejeshwa inapohusishwa na shughuli za uhalifu," sehemu ya pendekezo hilo inasema. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara, alisema marekebisho hayo yataziba mianya inayotumiwa na wahalifu kuficha mapato yao. Alisema sheria hiyo itawezesha idara za uchunguzi kufuatilia fedha iliyofichwa katika mifumo ya kidijitali kama inavyofuatilia fedha zilizowekwa kwenye akaunti za benki au mali ya kawaida. Pendekezo hilo linajiri siku chache baada ya maafisa wa Amerika kutwaa sarafu za kidijitali za thamani ya zaidi ya Sh97 milioni zinazohusishwa na mtandao wa ulaghai wa mikopo ya masomo uliohusisha raia wa Kenya. Operesheni hiyo, iliyopewa jina la Ghostbusters, ilikuwa sehemu ya uchunguzi wa kitaifa wa Idara ya Sheria ya Amerika kuhusu udanganyifu uliotumia wanafunzi hewa kujipatia fedha za masomo. Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mohamed Amin, alisema zaidi ya maafisa 500 wamepata mafunzo maalumu ya uchunguzi wa kifedha katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

read more